Ripoti hiyo iliyochunguza athari za miaka 60 ya ushirikiano wa kimataifa katika udhibiti wa dawa za kulevya inasema hatua za pamoja za nchi zimepunguza madhara ya kijamii na kiuchumi yanayosababishwa na dawa haramu.

Rais wa Bodi hiyo Profesa Sevil Atasoy amesema, “nchi zimeelewa kwamba njia bora zaidi ya kulinda afya na ustawi wa raia wao na kukidhi mahitaji yao ya kitabibu na kisayansi ni kupitia hatua zilizoratibiwa kwa pamoja. Mikataba mitatu ya kimataifa ya kudhibiti dawa za kulevya, ambayo inaungwa mkono karibu na mataifa yote duniani, inatoa mfumo wa pamoja wa kuchukua hatua za ushirikiano ili kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya duniani.”

Profesa Atasoy amesema kwa zaidi ya miaka 60 mikataba ya kimataifa imewezesha kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya huku ikihakikisha upatikanaji wa dawa muhimu kwa matumizi ya tiba na utafiti wa kisayansi.

Dawa za kulevya za aina ya Cocaine zanaswa katika Bandari ya Kingston, Jamaika, mnamo Machi 2023.

Dawa za kulevya za aina ya Cocaine zanaswa katika Bandari ya Kingston, Jamaika, mnamo Machi 2023.

Ushirikiano unafanyikaje?

Akifafanua zaidi juu ya majukumu yao Mwenyekiti huyo wa bodi ya INCB amesema “Jukumu letu ni kuimarisha juhudi za ushirikiano wa nchi na kanda kupitia kazi zetu. Kupitia mikataba hiyo Serikali zinatakiwa kutupa taarifa za kutuwezesha kusimamia kikamilifu kilimo, uzalishaji, utengenezaji na utumiaji wa bidhaa zinazodhibitiwa kwa lengo la kuzuia utoroshwaji wake. Kwa sababu ya ufanisi wa mfumo wa makadirio na tathmini, kiwango cha ubadilishaji wa vitu vilivyotengenezwa ambavyi vinaweza kutumika kwa njia haramu ni vya chini sana.”

Ripoti inaeleza kuwa mfumo wa makadirio na tathmini unaotumiwa kufuatilia uzalishaji, utengenezaji na biashara halali ya dawa umefanikiwa kwa kiwango kikubwa, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uelekezaji wa dawa halali kuingia katika soko haramu. 

Kupitia majukwaa ya kidijitali kama PEN Online na PICS, nchi hubadilishana taarifa kwa wakati halisi kuhusu usafirishaji wa kemikali zinazoweza kutumika kutengeneza dawa haramu. Mwezi Machi 2025, mfumo wa PEN Online ulisaidia kuzuia tani tatu za kiambata cha fentanyl zisielekezwe kwenye utengenezaji haramu.

Aidha, ushirikiano huo unahusisha sekta binafsi, mamlaka za forodha na posta, pamoja na kampuni za kemikali, ili kudhibiti vihatarishi na dawa mpya za sintetiki. 

Takribani serikali 200 na wadau wa kimataifa wanatumia zana za mpango wa GRIDS kuimarisha uratibu na ubadilishanaji wa taarifa.

Matumizi ya mihadarati yaongezeka duniani

Unsplash/Sharon McCutcheon

Matumizi ya mihadarati na ulanguzi ya dawa za kulevya inahitaji mshikamano wa kimataifa

Changamoto bado zipo

Nchi zenye kipato cha chini na cha kati zinaendelea kukumbwa na changamoto ya upatikanaji na unafuu wa bei ya dawa za kutuliza maumivu zenye opioid kama morphine, licha ya uwepo wa akiba ya kutosha kimataifa.

Kikanda, ripoti inaonesha ongezeko la matumizi ya dawa barani Afrika, huku soko la dawa ya kulevya ya Cocaine  huko Amerika Kusini likikua kwa kasi. 

Nchi za Asia Mashariki na Kusini-Mashariki zinaendelea kukabiliwa na tishio la methamphetamine, na Asia Kusini ikiwa soko kubwa zaidi la watumiaji wa opioid duniani.

Bodi hiyo imesisitiza kuwa kulinda afya ya watu dhidi ya hatari za dawa haramu ni jukumu la pamoja la kimataifa na imezitaka nchi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kuvuka mipaka katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya duniani.

Tembelea hapa kusoma ripoti hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *