Akilihutubia Baraza la Haki za Binadamu hii leo mjini Geneva, Kamishna Mkuu Türk amesema “Afghanistan ni kaburi la haki za binadamu. Mfululizo wa amri na sheria zilizotangazwa na mamlaka za Taliban tangu walipochukua madaraka mwaka 2021 zina athari mbaya sana kwa watu wa Afghanistan, hasa wanawake na wasichana.”
Amri mpya yapanua wigo wa hukumu ya kifo na kubana uhuru
Türk ameonya kuwa amri mpya iliyosainiwa mwezi uliopita na kiongozi wa Taliban inapanua wigo wa aina ya makosa yanayostahili adhabu kali kinyume na wajibu wa kimataifa wa Afghanistan.
“Amri hiyo inaongeza idadi ya makosa yanayoweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo,” amesema. “Inaruhusu matumizi ya adhabu za viboko kwa makosa mengi, hata ndani ya nyumba, jambo linalohalalisha ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Pia inahalalisha uhalifu wa kukosoa uongozi wa Taliban na sera zao, kinyume na uhuru wa kujieleza na kukusanyika.”
Kamishna Mkuu amewataka watawala hao kufuta amri hiyo na kuhakikisha sheria zote zinaendana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, huku akieleza kuwa mauaji ya hadharani bado yanaendelea kinyume cha sheria za kimataifa.
Baadhi ya watu milioni 2.5 waliorejea Afghanistan walilazimika kuondoka Iran na Pakistan kufikia sasa mwaka huu. Wengi waliripotiwa kuwa walikuwa wakielekea katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi la Jumapili.
Ubaguzi wa kijinsia wa kiwango cha kutisha
Kwa mujibu wa Türk, wanawake na wasichana nchini Afghanistan wanakabiliwa na ubaguzi uliokithiri unaofikia kiwango cha mateso ya kimfumo.
“Mamlaka za Taliban, kwa hakika, zimeharamisha uwepo wa wanawake na wasichana katika maisha ya umma,” amesema, akitaja marufuku ya elimu ya sekondari na juu, pamoja na ajira nyingi.
Ubaguzi huo pia unaathiri huduma za afya, uhuru wa kutembea na kushiriki katika masuala ya kijamii.
Ameeleza mfumo huo kuwa “unakumbusha ubaguzi wa rangi uliokuwa Afrika Kusini au Apartheid, lakini kwa misingi ya kijinsia badala ya rangi,” na kuunga mkono juhudi za kutambua rasmi ubaguzi wa kijinsia kama uhalifu chini ya Mkataba unaopendekezwa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Ubinadamu. “Kufafanua ubaguzi wa kijinsia ni hatua muhimu katika kuumaliza,” amesisitiza.
Ukandamizaji wa maisha ya kila siku na vyombo vya habari
Katika miezi ya hivi karibuni, mamlaka zimeimarisha utekelezaji wa sheria ya Kukuza Maadili na Kuzuia Maovu.
Kwa mujibu wa Türk, hatua hizo zinajumuisha “kudhibiti urefu wa ndevu za wanaume, kulazimisha uvaaji mkali wa hijabu kwa wanawake, kuhitaji wanawake kuandamana na mlezi wa kiume, kupiga marufuku muziki na picha za viumbe hai, na kusisitiza sala za lazima”.
Tangu tarehe 7 Septemba 2025, wanawake wa Afghanistan wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wakandarasi wamezuiwa kuingia katika majengo ya Umoja wa Mataifa nchini humo, hatua aliyoitaja kuwa “isiyokuwa na mfano na ya kushtua.”
Wakati huo huo, vyombo vya habari vinafanya kazi chini ya udhibiti mkali na shinikizo la kifedha, vikikatazwa kurusha muziki au kuchapisha maudhui yanayoonekana kupingana na tafsiri ya mamlaka ya sheria ya matumizi ya sharia. Wanahabari wanawake wanakabiliwa na vikwazo “karibu visivyowezekana katika kutekeleza kazi yao.”
Wakimbizi, umaskini na wito wa uwajibikaji
Türk pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya kibinadamu, akisema mamilioni ya Waafghanistan wanaishi katika umaskini uliokithiri bila chakula cha kutosha, maji safi, elimu, huduma za afya na ajira.
“Idadi kubwa ya wakimbizi wanaendelea kurejea Afghanistan, wengi wao wakirudishwa kwa nguvu na nchi jirani, hasa Pakistan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” amesema. “Wengi wao wanafika wakiwa na mali chache sana, bila huduma za afya na elimu, na bila matarajio ya ajira.”
Aliongeza kuwa anasikitishwa na taarifa kwamba nchi nyingine pia zinachukua hatua za kuwarejesha wakimbizi kwa lazima.
Akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ametaja hatua ya kutolewa kwa hati za kukamatwa mwezi Julai 2025 na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, kama maendeleo chanya.
Alihimiza Mataifa kuchunguza na, inapobidi, kuwafungulia mashtaka wale wote waliokiuka sheria za kimataifa wakati wa miongo ya mzozo nchini Afghanistan, akisisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa lazima iendelee kushinikiza mamlaka za Taliban kuheshimu wajibu wao wa haki za binadamu.