Tangu mwaka 2017 zoezi la kurejea kwa hiari limekuwa likiratibiwa kupitia makubaliano ya pande tatu kati ya serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR.

Lakini wakati baadhi wakichagua kuanza upya maisha yao nyumbani, wengine bado wanahitaji ulinzi wa kimataifa.

Afisa wa Uhusiano wa Nje wa UNHCR nchini Tanzania Bahia Egeh katika mahojiano maalum na Edouard de Bray wa UN News, kuhusu mwenendo wa wakimbizi hao kurejea nyumbani anafafanua kwa kina mchakato unavyokwenda, changamoto na msaada wanaowapa wakimbizi wanaorejea na wanaosalia kambini.

 Katika kambi za wakimbizi za Kigoma magharibi mwa Tanzania, maelfu ya familia za wakimbizi wa Burundi zinakabiliwa na uamuzi mgumu, kusalia kambini Tanzania au kurejea nyumbani Burundi. Anasema Bahia Egeh Afisa wa Uhusiano wa Nje wa UNHCR nchini Tanzania ambaye pia anasimamia shughuli za utafutaji rasilimali kwa niaba ya wakimbizi na waomba hifadhi waliolazimika kuyahama makazi yao.

Ameongeza kuwa tangu zoezi la kurejea nyumbani lilipoanza mwaka 2017, wakimbizi wengi wameamua kurudi nyumbani lakini wengine bado wana wasiwasi  na baadhi wanasema hawawezi  kamwe kurudi Burundi.

Katika mahojiano  na UN News Bahia amesema mchakato wa wakimbizi hawa kurejea nyumbani kwa hiari haukuanza leo wala jana ulianza 2017 na unafanyika kwa makubaliano maalum baada ya tathmini kuonesha kuwa hali ya usalama nchini Burundi imetengamaa kwa wakimbizi kurejea.

Lakini Egeh anasisitiza jambo moja muhimu kurejea lazima kuwe kwa hiari “Hata kama UNHCR haijaanza kuwezesha safari, iwapo mkimbizi wa Burundi ataamua, niiko tayari, nataka kurudi nyumbani, tunamshauri kwanza. Hiyo ndiyo tunaita kurejea kwa hiari bila msaada.”

Mwanamke anayebeba hati katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania, akiwa amezungukwa na wakimbizi wengine, akikazia hali ya wakimbizi wa Burundi na juhudi za kurudisha nchini kwa hiari.

© UNHCR/Maimuna Mtengela

Mwanamke mkimbizi wa Burundi akiondoka katika kikao cha kutoa taarifa za jamii kuhusu kurejea nyumbani kwa hiyari, akiwa ameandaliwa vifaa katika Kambi ya Nyarugusu, Magharibi mwa Tanzania.

UNHCR inawasaidia wanaoamua kurejea nyumbani

Bi. Egeh amemweleza De Bray kwamba wanaochagua kurejea kwa msaada, UNHCR husaidia kusafirisha familia zao kwa usalama hadi mpakani na kutoa kifurushi cha msaada wa kurejea ili kurahisisha ujumuishwaji wao upya katika jamii wafikapo Burundi.

“Tunahakikisha wanasafiri salama na mizigo yao, ili wanaporejea waweze kujumuika tena katika jamii zao.” UNHCRBahia Egeh

Ameongeza kuwa idadi ya wanaorejea amesema imekuwa ikibadilika kwa miaka mingi “Tukiangalia mwenendo tangu 2017, ulianza kwa nguvu. Kisha kipindi cha COVID kulikuwa na kupungua kwa wanaorejea. Baadaye idadi ilishuka, kisha ikaongezeka tena.”

Sio wakimbizi wote wanaoweza kurudi kwa usalama amesema Bi. Egeh kwani miongoni mwa wakimbizi wa Burundi waliobaki Tanzania, inakadiriwa kuwa kati ya 10,000 hadi 17,000 bado wanahitaji ulinzi wa kimataifa.

“Kwenye vituo vya kuondokea tunakofanya usajili, tuna dawati maalum la ulinzi. Hapo tunathibitisha kama uamuzi ni wa hiari na kuhakikisha kwamba wale wanaohitaji ulinzi wa kimataifa nchini Tanzania hawajumuishwi kwenye misafara ya kurejea.”

Hivi sasa, changamoto mpya zinaibuka. Katika kambi ya Nduta ambayo ndio hasa kambi ya wakimbizi wa Burundi, mamlaka ya Tanzania imetangaza mpango wa kuifunga kabisa kambi hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, De Bray alitaka kujua endapo hatua hiyo inaongeza chachu ya hofu kwa wakimbizi
“Kuna wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa wakimbizi kuhusu kurejeshwa kwa nguvu au hatua za shinikizo. Kama UNHCR tunaendelea kusisitiza kwa serikali kuzingatia makubaliano ya pande tatu kwamba kurejea kuwe kwa usalama na heshima, na kuheshimu misingi ya wakimbizi ya ulinzi.”

Mwanamke mmoja anashauriana na mfanyakazi wa UNHCR katika kituo cha usaidizi wa kurudishwa nchini Tanzania, ambapo habari na ushauri hutolewa kwa wakimbizi wa Burundi.

© UNHCR/Maimuna Mtengela

Mfanyakazi wa UNHCR akizungumza na mkimbizi wa Burundi katika Kambi ya Nyarugusu, Kigoma Magharibi mwa Tanzania.

Ukata wa fedha waongeza adha

Kwa wale wanaobaki kambini, maisha yanazidi kuwa magumu. Ufadhili wa kibinadamu duniani umepungua kwa kiasi kikubwa.

Egeh anatoa mfano dhahiri katika kambi ya Nyarugusu ambayo ndio kubwa zaidi mkoani  Kigoma.

“Nilipofika miaka miwili iliyopita, kulikuwa na vituo 10 vya afya. Leo, kuna vituo viwili tu vilivyo wazi. UNHCR bado inajaribu kuendesha hospitali kuu. Ni changamoto kubwa kwa wakimbizi hapa Nyarugusu.”

Hata kwa wanaofikiria kurejea, changamoto za ujumuishwaji upya katika jamii zinawatia hofu hasa masuala ya ardhi na makazi nchini Burundi. “Ardhi na makazi ni moja ya sababu zinazowafanya wasitesite kurudi. Huenda hawana ardhi ya kutosha au wakakumbana na matatizo ya kurejeshewa makazi yao.”

UNHCR inasema imekuwa ikitoa taarifa kuhusu mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi iliyopo nchini Burundi ili kusaidia wanaorejea kushughulikia changamoto hizo kwa njia ya amani.

Lakini uendelevu wa kurejea unahitaji msaada wa kifedha si tu Tanzania, bali pia ndani ya Burundi, Bi.Egeh amesihi “Kama mtafadhili, tafadhali fadhilini pia nchini Burundi. Saidieni juhudi za ujumuishaji upya ili kurejea kuwe endelevu na watu waweze kuanza kujenga upya maisha yao nyumbani.”

Kwa UNHCR, msimamo unabaki kuwa ule ule. “Kurejea lazima kuwe kwa usalama na heshima. Na lazima kuwe kwa hiari na kwa taarifa sahihi na shirika hilo linasema litaendelea kupinga hatua zozote za shinikizo kwa wakimbizi.”

Wakati mabasi yakiendelea kuondoka kambini kuelekea mpakani, kila familia inalazimika kufanya uamuzi wake kati ya kutokuwa na uhakika, na matumaini ya kuanza upya maisha nyumbani, kwa maelfu ya wakimbizi wa Burundi walioko Tanzania, huo ni uamuzi binafsi na wenye athari kubwa kwa mustakabali wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *