Katika karakana yenye kelele za injini na migongano ya zana za kazi hapa katika kambi ya Yambio jimboni Equatoria Magharibi, mwanamke mmoja shupavu, Meja Tigist Ferede mwenye umri wa miaka 46, anabadili mtazamo wa kazi zilizotawaliwa na wanaume. Meja Ferede ni fundi mitambo wa magari (makanika) kutoka kikosi cha Ethiopia, amekuwa nguzo muhimu kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS). 

Yeye hashiki mtutu na kusimama mstari wa mbele kwenye doria, bali anahakikisha kila gari linalotoka kambini liko imara kwa ajili ya safari ndefu na zenye hatari, kwani hitilafu ndogo ya gari inaweza kuzuia uokoaji wa raia walio hatarini.

Meja Ferede ameeleza uzoefu wake akisema. 

“Nimetumikia jeshi kwa zaidi ya miaka 20. Hii ni misheni yangu ya pili katika Umoja wa Mataifa. Misheni yangu ya kwanza nilienda Sudan. Ilikuwa na changamoto kutokana na hali mbaya ya hewa na mwingiliano na jamii ya wenyeji haukuwa rahisi, lakini nilipokuja hapa kwa misheni yangu ya pili, imekuwa rahisi zaidi kwa sababu hali ya hewa ni nzuri na watu ni wakarimu. Kila gari ninalotengeneza limebeba matumaini. Yanapofika salama, najua nimetimiza wajibu wangu kwa ajili ya amani. Nawapenda watu wa hapa kwa sababu sote ni Waafrika, haswa kwa Sudan Kusini, tuna mambo mengi yanayofanana kwani ni majirani zetu.”

Ni katika gwaride maalum la kutunuku medali. Kutokana na mchango wake huo mkubwa, ametunukiwa nishani ya heshima ya Umoja wa Mataifa, hapa anaeleza furaha yake.

“Leo ni siku ya kipekee kwa sababu tumepokea nishani ya Umoja wa Mataifa kwa huduma yetu nchini Sudan Kusini, hivyo, nina furaha kwa hatua hiii. Kuvaa nishani hii kunanikumbusha kuwa hakuna jukumu dogo katika kulinda amani.”

Viongozi wa jimbo la Equatoria Magharibi wametambua mchango mkubwa wa walinda amani hao katika kuleta utulivu kwenye maeneo yenye machafuko ikiwemo Tambura. Kaimu Gavana wa jimbo hilo, Marona Joseph, amewapongeza askari hao.

“Nimetambua wazi kuwa mmechangia katika kuimarisha amani, hasa katika eneo la Tambura na maeneo mengine mliyoko. Serikali ya jimbo inapoomba msaada wenu, mmekuwa mkijibu kwa haraka sana.”

Ushirikiano huu kati ya walinda amani na serikali, umekuwa chachu ya kurejesha usalama kwa wananchi. Kamanda mkuu wa vikosi vya UNMISS, Luteni Jenerali Mohan Subramanian amesisitiza umuhimu wa kuwaheshimu walinda amani wote, raia na wanajeshi, wanaofanya kazi bila kuchoka.

“Idadi kubwa ya watu ambao wangekuwa wamefariki tangu mwaka 2021, sasa wapo hai kutokana na kazi nzuri iliyofanywa kikosi cha Ethiopia. Hadi sasa, askari 142 wa Ethiopia wamepoteza maisha yao wakitumikia bendera ya Umoja wa Mataifa, na tunapaswa kukumbuka kujitolea kwao.”

Jenerali huyo amewakumbuka pia askari tisa waliofariki wakiwa kazini ndani ya misheni ya UNMISS.

Uwepo wa Meja Ferede na wote wanaohakikisha “magurudumu ya magari ya amani” yanazunguka nchini Sudan Kusini, unatoa faraja, msaada, na matumaini kwa jamii zilizokumbwa na vita. Meja Ferede amethibitisha kuwa amani haijengwi tu kwa bunduki, bali pia kwa spana na injini zinazofanikisha huduma zinawafikia walio na uhitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *