Wakati wa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi, tarehe 28 Februari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema hakuna mbadala wa mazungumzo kwenye hiki kinachoendelea sasa cha mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na  Marekani, Israel na Iran. “Hali ya sasa inaleta tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”

Katibu-Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza katika mkutano rasmi, akiwa na bamba la jina lililoandikwa 'KATIBA-MKUU' na maofisa wengine wameketi nyuma yake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kwa dharura Februari 28 kujadili kuhusu Iran

Akihutubia Baraza hilo jijini New York, Marekani Katibu Mkuu amelaani “mashambulizi makubwa ya kijeshi” yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yaliyokiuka uhuru na mipaka ya Bahrain, Iraq, Jordan, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.

Kiwango cha  uharibifu

Amewaambia wajumbe kuwa takribani miji 20 kote Iran — ikiwemo Tehran, Isfahan, Qom na Tabriz — imeripotiwa kushambuliwa. 

“Milipuko mikubwa imeripotiwa katika eneo la Tehran linalojumuisha ikulu ya rais na makao ya Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, ambaye kwa mujibu wa vyanzo vya Israel ameuawa,” ingawa Katibu Mkuu amesema hawezi kuthibitisha taarifa hiyo.

Vyanzo vya habari Iran

Guterres amenukuu vyanzo vya habari vya Iran vikisema kuwa watu wasiopungua 85 waliuawa katika shambulio la anga lililolenga shule ya wasichana huko Minab, huku shule nyingine mjini Tehran pia ikishambuliwa. 

Iran imefunga anga lake na “inakaribia kuzima kabisa mtandao wa intaneti.”

Vyanzo vya habari vya Israeli

“Vyanzo vya Israel viliripoti watu 89 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran, huku athari mbaya pia zikiripotiwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu,” amesema Guterres.

Ameendelea kusema kuwa nchi za Ghuba zilidaka makombora mengi yaliyorushwa, lakini Falme za Kiarabu ziliripoti raia mmoja kuuawa na mabaki ya kombora lililodunguliwa.

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani

Guterres pia ametaja taarifa za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora nchini Iraq, mabaki ya makombora kuanguka Lebanon na Syria, pamoja na dalili kuwa Iran huenda ikafunga Mlango wa Bahari wa Hormuz kwa usafiri wa kimataifa wa majini. 

Fursa ya diplomasia imeyoyoma

Kuongezeka huku kwa mvutano kunafuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yaliyopatanishwa na Oman, huku mazungumzo ya kiufundi yakipangwa kufanyika Vienna, Austria.

“Ninasikitika sana kwamba fursa hii ya diplomasia imepotezwa,” amesema Guterres huku akitoa wito wa “kusitishwa mara moja kwa mapigano,” 

Katibu Mkuu amehimiza pande zote kurejea kwenye mazungumzo, hasa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. 

Mbadala wa mazungumzo utaleta madhara makubwa

“Ninatambua kuwa Rais wa Marekani ameripotiwa kuzungumza na viongozi wa Saudi Arabia, Qatar, na Falme za Kiarabu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran naye ameripotiwa kuzungumza na wenzake katika nchi za Ghuba, (GCC) na Iraq. Kila jitihada lazima ifanyike kuzuia kuongezeka zaidi kwa mvutano,” amesema Katibu Mkuu

Ameyasihi mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuheshimu sheria za kimataifa, kulinda raia kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa, na kuhakikisha usalama wa nyuklia, akionya kwamba mbadala wake unaweza kuwa mgogoro mpana zaidi wa kikanda wenye madhara makubwa.

Marekani yaelezea lengo la operesheni Epic Fury 

Afisa wa serikali ya Marekani akizungumza katika mkutano wa kidiplomasia, akiwa na bamba la jina linalosomeka 'UNITED STATES', akifuatiliwa na maafisa wengine wawili.

Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mike Waltz akihutubia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama kuhusu Iran na Mashariki ya Kati.

“Huu ni wakati katika historia unaohitaji msimamo thabiti wa kimaadili,” amesema Balozi Mike Waltz ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, akisisitiza kuwa Rais wa Marekani Donald Trump amekabiliana na wakati huo ipasavyo.

Amesisitiza kuwa Operesheni Epic Fury jina lililopatiwa operesheni hiyo ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, ilielekezwa kwenye malengo “maalum na ya kimkakati”: kuvunja uwezo wa makombora yanayotishia washirika wa Marekani, kudhoofisha rasilimali za kijeshi za majini zinazotumika kuvuruga usalama wa eneo la kimataifa majini, na kusambaratisha mifumo inayosambaza silaha kwa makundi ya wanamgambo washirika.

Balozi Waltz amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kwamba “utawala wa Iran hauwezi kamwe, kabisa, kuitishia dunia kwa silaha ya nyuklia.”

Ukimya wa kinachoendelea Iran ni  ushiriki wa uhalifu huu – Iran

Mwanadiplomasia wa kiume kutoka Iran (Jamhuri ya Kiislamu ya) akizungumza katika mkutano wa kimataifa, akisoma kutoka kwa hati kwenye jukwaa na bamba la jina la nchi yake.

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Amir Saeid Iravani akihutubia Baraza la Usalama.

Fursa ikawadia kwa Balozi Amir Saeid Iravani, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa kuhutubia wajumbe wa Baraza ambapo amesema, “kwa ukweli rahisi na usiopingika:Israel na Marekani zimeishambulia Iran. Zimekiuka sheria za kimataifa na Mkataba wa United Nations. Lazima ziwajibishwe.”

Amesema Iran iko tayari kabisa kwa mazungumzo na diplomasia ili kumaliza mvutano  unaoendelea, lakini “iwapo uchokozi huo unaendelea, Iran itaendelea kutekeleza haki yake ya asili ya kujilinda — kwa uthabiti, kwa uwiano, na bila kusita — hadi uchokozi huo utakapokoma.”

Balozi Iravani amesema, “Baraza la Usalama linapaswa kuchukua hatua — sasa — na kusitisha mara moja vitendo hivi vya uchokozi. Ukimya ni ushiriki katika uhalifu huu.”

Mwakilishi huyo wa Iran katika hotuba yake yenye kurasa 12 alizungumza kabla ya Mwakilishi  wa Israeli na kusema kuwa “tunakataa kabisa na kulaani vikali hoja za uongo na za kupotosha zitakazotolewa na mwakilishi wa Israeli.”

Amedai kuwa historia ya Israeli imejengwa juu ya uchokozi, uvamizi, mauaji ya halaiki, ukiukwaji wa kimfumo wa sheria za kimataifa, na matumizi ya mara kwa mara ya nguvu.

“Kwa kuzingatia historia hiyo, madai ya utawala huo hayana uaminifu wowote. Hakuna mwanachama mwenye kuwajibika wa Baraza hili atakayechukulia madai hayo kwa uzito,” ametamatisha Balozi Iravani.

Tulichofanya leo ilikuwa ni kwa maslahi mapana

Mwanamume aliyevaa suti akitoa hotuba katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, akiwa na bamba lililoandikwa 'ISRAEL' mbele yake.

Mwakllishi wa Kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Danny Danon akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Kwa miaka 47, utawala wa Kiislamu nchini Iran umeongoza umati wa watu kupaza sauti wakisema kifo kwa Israel, kifo kwa Marekani,” amesema Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Danny Danon alipoanza hotuba yake ndani ya Baraza la Umoja wa Mataifa.

“Haya si maneno ya hasira ya kundi dogo la wenye msimamo mkali,” amesisitiza akiongeza kuwa,  “huu ni uhasama unaoidhinishwa na dola.”

Balozi Danon ameema wakati kauli hizo zikiendelea kusikika, urani iliendelea kuzalishwa, mashine za mitambo ya nyuklia ilizunguka, makombora yalitengenezwa na vituo vikafukiwa kabisa chini ya ardhi.

Hatua ya lazima

“Leo, kwa kushirikiana na Marekani, Israel ilichukua hatua kuzuia tishio la kimaangamizi kabla halijawa hali isiyoweza kurekebishwa,” amesisitiza.

Amesisitiza kuwa Israel ilichukua hatua kwa sababu ya dharura, kwani utawala huo haukuacha njia nyingine ya busara  na kwamba operesheni hizo za  pamoja zitaendelea iwapo tishio hilo litaendelea kuwepo.

Balozi Danon amedai kuwa utawala huo umeunda silaha za nyuklia kwa kupuuza waziwazi sheria za kimataifa, “umeua raia wake wenyewe na kukandamiza upinzani, umeongeza hazina ya makombora na kuwapa silaha washirika wake katika eneo hilo, na umetangaza nia ya kuifuta Israel kwenye ramani.”

Diplomasia ilikuwa imefikia mwisho wake, amesema, akisisitiza kuwa Iran ilitakiwa kusitisha urutubishaji wa urani na kuruhusu ukaguzi kamili. “Iran haikufanya lolote kati ya hayo,” amesema.

“Walikuwa wanajenga uwezo wa kulazimisha hali isiyoweza kubadilishwa huku tukibinywa. Hiyo si mustakabali ambao Israel itakubali.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *