Dar es Salaam. Umri ni namba ndivyo unavyoweza kusema kutokana na gwiji wa muziki wa DRC- Congo, Koffi Olomide (70), kupishana miaka 27 na mkewe, Cindy Le Coeur (43), waliyefunga ndoa ya kiserikali hivi karibuni baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu.

Vyombo mbalimbali vya habari nchini DRC Congo vimeripoti kwamba wawili hao wamefunga ndoa katika sherehe ya faragha iliyofanyika Februari 28, 2026 ikihudhuriwa na ndugu, marafiki na baadhi ya watu wa karibu kwenye muziki.

Kwa miaka mingi, Koffi na Cindy wamekuwa wakionekana pamoja jukwaani na kwenye video za muziki kupitia bendi yao maarufu ya Quartier Latin International.  Cindy Le Cœur, katika mahojiano ya hivi karibuni alisema walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2006 alipojiunga na bendi ya Koffi, Quartier Latin International, kama mwimbaji na mkurugenzi wa lebo hiyo.

Aliongeza kwamba uhusiano wao wa kimapenzi ulianza rasmi mwaka 2008, ukaanzisha ukaribu wa miongo miwili ya upendo kabla ya ndoa yao ya kiserikali.

Awali, baadhi ya mashabiki waliwatazama kama bosi na mfanyakazi wake, lakini nyuma ya pazia walikuwa wapenzi licha ya kutoonyesha dalili zozote hadharani.

Cindy alijiunga na Quartier Latin mwaka 2007 na akawa moja ya wasanii tegemeo ndani ya bendi hiyo. Uwezo wake wa kuimba kwa hisia na kuhimili jukwaa ulimvutia Koffi, nguli wa muziki wa Rumba na Ndombolo.

Hii ni ndoa ya nne ya Koffi Olomide ambaye ana watoto kadhaa kutoka kwa wanawake tofauti. Mke wake wa kwanza alikuwa Marianne Makosso, ambaye walipata naye watoto wawili. 

Baadaye alipata watoto watatu na mke wake wa pili, Stephanie Godee ambaye baadae waliachana. Kisha akaanza uhusiano na mke wake wa tatu, Aliane, mwanamitindo wa zamani kutoka Ufaransa, mwaka 1990 jijini Paris. 

Walifunga ndoa Aprili 15, 1994 na kupata watoto watatu, akiwemo Didi-Stone Naïke, ambaye ni mwanamitindo maarufu na balozi wa L’Oréal Paris nchini Ufaransa.

Baada ya miaka 27 ya ndoa, Aliane aliomba talaka mwaka 2021 kufuatia tetesi za migogoro ya ndoa na madai ya ukosefu wa uaminifu, ikiwemo uvumi wa uhusiano wa Koffi na mshirika wake wa muziki Cindy Le Coeur ambaye kwa sasa ndiye mke wa nne.

Oktoba 2022 wakapeana talaka katika mahakama ya Bobigny, Ufaransa. Mwaka 2024, Koffi alithibitisha hadharani kuwa amepewa talaka na akatangaza kutoka kimapenzi na Cindy, akisema anataka atambulike kama mwenzi wake halali. Mgogoro huo uliathiri pia familia yao, hasa Didi-Stone ambaye alionekana kumuunga mkono mama yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *