Mbeya. Mahakama ya Rufani imemuachia huru Augustino Mbonile aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji, baada ya kubaini kuwa shahidi muhimu wa upande wa mashitaka alitoa ushahidi pasipo kula kiapo kinyume na sheria.

Mbonile alikuwa amehukumiwa mwaka 2022 na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kwa kosa la kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 84. Baadaye, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ilithibitisha hukumu hiyo alipokata rufaa. Hata hivyo, hakuridhika na akaendelea kupigania haki yake katika Mahakama ya Rufani, ambayo Machi 2, 2026 ilibatilisha hukumu hiyo na kuamuru aachiliwe huru mara moja.

Msingi wa Kesi

Kwa mujibu wa mashitaka, tukio hilo lilidaiwa kutokea Februari 7, 2022 saa 5:00 usiku katika kijiji cha Iponjola, wilayani Rungwe. Ilielezwa kuwa siku hiyo mzee huyo alikuwa amelala nyumbani kwake bila kufunga mlango, akimsubiri mjukuu wake wa kike aliyekuwa ameenda kwenye maziko arejee.

Katika ushahidi wake, alidai kuwa mtu alirukia kitandani kwake na mwanzoni alidhani ni mjukuu wake. Hata hivyo, mtu huyo alitaka ampatie Sh30,000 na alipopewa fedha hizo, noti moja ilidondoka chini. Wakati wa kuitafuta, mtu huyo aliwasha tochi na kupitia mwanga huo alimtambua kuwa ni Mbonile.

Alidai kuwa baada ya hapo alibakwa na baadaye kutolewa nje kwa lengo la kuuawa, lakini majirani akiwemo mjukuu wake walifika na ndipo mtuhumiwa akatoroka. Baadaye alieleza tukio hilo kwa mjukuu wake na kwa mtoto wake wa kiume (shahidi wa tatu), ambaye aliwajulisha viongozi wa eneo hilo na hatimaye mtuhumiwa kukamatwa.

Hata hivyo, Mbonile alikanusha shtaka hilo tangu mwanzo.

Baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe na hukumu kuthibitishwa na Mahakama Kuu, Mbonile alikata rufaa Mahakama ya Rufani akidai kuwa mahakama za chini zilikosea kisheria na kimsingi kwa kumtia hatiani kwa kutegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye hakula kiapo.

Rufaa hiyo ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambao ni Rehema Mkuye, Sam Rumanyika na Ubena Agatho. Mrufani alijiwakilisha mwenyewe huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili waandamizi wa Serikali, Naomi Mollel na Hannarose Kasambala, wakisaidiwa na wakili Rajabu Msemo.

Awali upande wa Jamhuri ulipinga rufaa hiyo, lakini wakati wa usikilizwaji, wakili Mollel alikubaliana na hoja ya msingi ya mrufani kwamba shahidi wa kwanza alitoa ushahidi bila kula kiapo kinyume na kifungu cha 212 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachotaka shahidi kuapishwa kabla ya kutoa ushahidi.

Alieleza kuwa kwa kuwa shahidi huyo alikuwa ndiye mhimili wa kesi ya mashitaka, na ushahidi wake haukuzingatia matakwa ya kisheria, basi ushahidi huo haukuwa na thamani ya kisheria na ulipaswa kuondolewa kwenye kumbukumbu.

Uamuzi wa Majaji

Katika hukumu yao, majaji walichambua mwenendo wa kesi na kubaini kuwa shahidi huyo hakuwahi kuapishwa kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake wa msingi. Ingawa alijitambulisha kuwa ni Mkristo, mahakama haikuchukua hatua ya kumwapisha kama inavyotakiwa na kifungu cha 212(1) cha CPA.

Majaji walisisitiza kuwa kula kiapo ni sharti la lazima kisheria na kwamba ushahidi uliotolewa bila kuapishwa hauna thamani ya ushahidi. Hivyo waliamua kuuondoa ushahidi wote wa shahidi huyo katika kumbukumbu.

Walieleza kuwa mashahidi wengine wa upande wa Jamhuri walitoa ushahidi wa kusimuliwa, kwani walieleza kile walichoambiwa na mlalamikaji. Aidha, madai kwamba mrufani alikiri kosa mbele ya viongozi wa kijiji hayakuungwa mkono na ushahidi wa moja kwa moja kwa kuwa viongozi hao hawakuitwa mahakamani, na mrufani alikanusha kukiri.

“Ushahidi uliobakia hautoshi kumtia hatiani mrufani. Mashitaka hayakuthibitishwa pasipo kuacha mashaka,” walieleza majaji katika hukumu yao.

Kutokana na mazingira hayo, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na rufaa ya Mbonile, ikabatilisha kutiwa kwake hatiani, kufuta adhabu ya kifungo cha miaka 30 na kuamuru aachiliwe huru mara moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *