Katika Taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva na New York Fletcher amesema  “Athari za kibinadamu kutokana na ongezeko la ghasia Mashariki ya Kati zinazidi kuwa changamoto kubwa,” akisisitiza kuwa raia wanaendelea kubeba mzigo Mkubwa wa machafuko hayo. 

Amesisitiza kuwa “Raia lazima walindwe bila masharti.” Mashambulizi dhidi ya nyumba, hospitali, na shule yameripotiwa katika nchi kadhaa, zikiwemo Iran, Lebanon, na Eneo Linalokaliwa kimabavu na Israel la Palestina, yakizidisha hofu ya kuongezeka kwa watu wanaokimbia makazi yao na mateso.

Watu wanaendelea kukimbia huku misaada ikipungua

Amesema athari za kibinadamu zinaenea nje ya maeneo ya moja kwa moja ya mzozo. Nchini Lebanon mathalani, mashambulizi Kusini mwa nchi hiyo, Nabatiyeh, na Beirut yameua zaidi ya watu 50 na kuwafurusha maelfu. 

Zaidi ya watu 60,000 sasa wapo katika makazi ya pamoja, huku wengine wakisalia mitaani baada ya amri za kuwahamisha kutolewa katika zaidi ya miji na vijiji 100. 

Katika eneo linalokaliwa kimabavu na Israel la Palestina, vikwazo vya operesheni vimepunguza sana upatikanaji wa msaada, huku uhamishaji wa wagonjwa ukisitishwa na mipaka muhimu kufungwa. 

Fletcher amesema zaidi ya wagonjwa 18,000 ikiwa ni pamoja na watoto 4,000 bado hawawezi kupata matibabu maalum. 

“Vikwazo vya ufikiaji vinaathiri operesheni za kuokoa maisha,” a mesema, akionya kuwa nafasi ya kibinadamu inazidi kupungua.

Afghanistan na Pakistan zinakabiliwa na changamoto

Mgogoro huo pia unazidisha shinikizo la kibinadamu katika nchi jirani. Afghanistan, ambako zaidi ya watu milioni 22 tayari wanahitaji msaada, imeshuhudia uhasama mpya ukilazimisha zaidi ya watu 60,000 kuhama makazi yao. 

Mvutano wa kikanda unaweza kuzidisha mgogoro uliopo wa uhakika wa chakula,” ameonya Fletcher akibainisha hatari zinazoweza kuathiri watu milioni 17. Nchini Pakistan, mashambulizi dhidi ya vituo vya Umoja wa Mataifa na uwezekano wa ukosefu wa utulivu Iran unaweza kusababisha harakati kubwa za watu kuelekea Baluchistan, na hivyo kuzidisha mzigo katika nchi inayohifadhi wakimbizi 1.3 milioni.

Hatua za kimataifa zinakabiliwa na changamoto 

Mawimbi ya mgogoro Mashariki ya Kati yanavuruga operesheni za kibinadamu duniani. Kufungwa kwa anga na njia za usambazaji kumesababisha kukwama kwa safari za misaada na kuzuia ugavi. 

“Ikiwa njia za nishati au knjia za baharini zitaendelea kuvurugwa, bei za chakula zitapanda na mifumo ya afya itabanwa,” Fletcher ameonya. 

Shirika linahifadhi akiba na kutafuta njia mbadala za usambazaji, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa fedha za dharura kupitia Mfuko wa Dharura wa Kibinadamu. Wakati huo huo, migogoro Sudan, Ukraine, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC inaendelea, ikionesha haja ya kuendelea kwa ushirikiano wa kimataifa.

Sheria za kimataifa ziko hatarini

Fletcher amesisitiza athari kubwa za kupungua kwa heshima hasa kwa sheria za kibinadamu za kimataifa. 

“Kila mara miundombinu ya raia inaposhambuliwa na misaada inapofanywa ya kisiasa, nafasi ya hatua za kibinadamu hupungua,” amesema. Ametoa wito wa kujitolea upya kwa hatua za kibinadamu zisizopendelea na ulinzi wa raia. 

“Sheria za kimataifa bado ni kinga bora dhidi ya mzunguko wa ghasia na vita. Tutasimama imara.” 

Huku mivutano ya kimataifa ikiongezeka, viongozi wa kibinadamu wanaonya kuwa kushindwa kulinda raia kunaweza kuzidisha ukosefu wa utulivu na kurefusha mateso katika eneo hilo na kwingineko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *