MAJIBU ya maswali kuhusu wapi Dabi ya Dar es Salaam kati ya Azam FC dhidi ya Yanga katika Ligi Kuu itachezwa yamepatikana baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa kupisha maboresho yanayolenga Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027.

Dabi hiyo itakayochezwa Machi 15, 2026 imehamishiwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam ambapo Azam itakuwa mwenyeji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema mchezo huo wa kwanza dhidi ya Yanga katika ligi utachezwa Uwanja wa Azam Complex.

“Mechi hiyo itachezwa hapa uwanja wa nyumbani na siyo kwa Mkapa kama ilivyozoeleka, hivyo tunawakaribisha sana mashabiki waje kushuhudia mechi kubwa na nzuri,” alisema Zaka Zakazi.

Msimu uliopita mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara zilizokutanisha timu hizo zilipigwa uwanjani hapo. Ile ya duru la kwanza Azam iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Gibril Sillah, kisha duru la pili Yanga ikashinda 2-1. Mabao ya Yanga yalifungwa na Pacome Zouzoua na Prince Dube wakati Azam mfungaji ni Lusajo Mwaikenda.

Kwa sasa Azam inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 23, wakati Yanga ikiongoza na pointi 29, zote zimecheza mechi 11.

Kabla ya dabi hiyo, zote zitashuka dimbani mara tatu, zikiwamo mechi mbili za ligi na moja Kombe la Shirikisho (FA).

Machi 5, Yanga itacheza dhidi ya Singida Black Stars wakati Azam ikipambana na Tanzania Prisons, katika mechi za Ligi Kuu Bara zote zikiwa ugenini.

Machi 8, zote zitakuwa nyumbani katika hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA), Yanga ikicheza dhidi ya Polisi Tanzania na Azam dhidi ya Mbeya Kwanza.

Machi 11, Azam itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, kisha Machi 12, Yanga pia itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Tanzania Prisons, hizi ni mechi za Ligi. Baada ya hapo, ndiyo dabi yao Machi 15.

Mwanaspoti iliwahi kuzungumza na kocha wa kikosi hicho Florent Ibenge na alisema kuwa: “Malengo yetu ya juu ni kuwa katika nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi, lakini ya chini ni kupunguza tofauti ya pointi kati yetu na Simba na Yanga walio juu yetu.

“Kwa sasa hatutakiwi kuwa na utofauti mkubwa wa pointi, labda ziwe nne tofauti na msimu uliopita zilikuwa 15, ni nyingi sana. Azam haitakiwi kuwa na hali kama hiyo. Tunatakiwa kufanya kazi sana kutimiza malengo yetu haya,” alisema Ibenge ambaye hivi sasa kikosi chake cha Azam kimeachwa pointi sita na Yanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *