Mexico. Kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation, Nemesio Oseguera Cervantes, maarufu El Mencho, amezikwa jana Jumatatu katika jeneza la dhahabu linalong’aa, likiwa limezungukwa na mashada makubwa ya maua na ulinzi mkali.
Mazishi hayo yamevutia hisia mchanganyiko ya heshima, hofu na sintofahamu kwa wakazi wa jimbo la Jalisco.
Jeneza hilo lilielezwa kuwa la kifahari lenye mvuto wa macho, likiwa na umbo la kisasa na pembe zilizochongwa kwa ustadi.
Mng’ao wake uliakisi mwanga, likifanya mazishi yawe kielelezo cha utajiri na hadhi ya kipekee ya kiongozi aliyezikwa.
Jeneza la kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation, Nemesio Oseguera Cervantes, maarufu El Mencho
Gharama ya jeneza hili, lililopakwa dhahabu (gold-plated), inakadiriwa kufikia dola 20,000 za Marekani (takribani Sh50 milioni).
Ofisa mmoja wa Serikali alithibitisha kuwa mazishi yamefanyika katika makaburi ya Zapopan, kitongoji cha Guadalajara, jiji la pili kwa ukubwa nchini Mexico.
Mamia ya watu waliandamana katika msafara wa mazishi, wengi wakiwa wamebeba miamvuli myeusi huku bendi ikipiga muziki wa asili wa Mexico unaojulikana kama banda.
Ofisa huyo aliomba kutotajwa kwa sababu hakuwa na idhini ya kuzungumzia eneo hilo, huku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ikikataa kuthibitisha eneo la mazishi kwa sababu za usalama.
Msafara uliobeba jeneza la kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation, Nemesio Oseguera Cervantes, maarufu El Mencho
Usalama ulikuwa wa hali ya juu zaidi: wanajeshi na polisi wa shirikisho walitawanyika kando ya makaburi na njia za kuingilia, vyombo vya angani vilikuwa vinafuatilia eneo, na vitengo vya haraka vya kujibu dharura vilikuwa tayari.
Mashada makubwa ya maua yaliwekwa bila majina kama ilivyo kawaida, baadhi yakiwa na picha ya jogoo, ikielezea jina lake la utani “Bwana wa Majogoo.”
Jeneza la aliyekuwa kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation, Nemesio Oseguera Cervantes, maarufu El Mencho
El Mencho aliuawa zaidi ya wiki moja iliyopita na jeshi la Mexico wakati wa operesheni ya kumkamata.
Alifariki dunia kutokana na majeraha ya risasi, kulingana na cheti cha kifo kilichopatikana kwenye vyombo vya habari.
Kifo chake kilipelekea ghasia katika majimbo takribani 20 nchini Mexico.
Genge la Jalisco New Generation ni moja ya makundi yenye nguvu zaidi nchini Mexico, ikiwa inahusishwa na biashara ya dawa za kulevya, utekaji nyara, na mashambulizi makubwa.
Jeneza la aliyekuwa Kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation, Nemesio Oseguera Cervantes, maarufu El Mencho likiwa nje.
Uhalifu wa makundi haya umechangia ukosefu wa usalama katika maeneo mengi nchini humo, huku operesheni za kijeshi na polisi zikiendelea kumlenga kiongozi huyo aliyeheshimika kwa hila na hofu kutoka kwa wafuasi na maadui zake.