MBEYA City imeendelea kuwa na matokeo ya kusuasua kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kuchapwa bao 1-0 na Fountain Gate kwenye mechi kali ya kufunga mzunguko wa kwanza kwa timu hizo iliyopigwa leo Machi 3, 2026 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mbeya City ambayo ipo chini ya kocha mzoefu, Mecky Maxime, haijafanya vizuri kwenye mechi za hivi karibuni ambapo iliikaribisha Fountain ambayo nayo haipo vizuri kwenye ligi.

Hata hivyo, pamoja na ubora wa timu zote ulioonekana dakika tisini za mechi hiyo, Mbeya City itatakiwa kujilaumu yenyewe kutokana na kukosa nafasi kadhaa za wazi ambazo zingeweza kuwapa ushindi nyumbani.

Nyota wa Fountain, Sadick Ramadhani, alifanikiwa kuifungia timu hiyo bao pekee dakika ya 78 kwa kichwa safi baada ya mabeki wa Mbeya City kuzembea kuokoa mpira wa krosi.

Huu ni ushindi wa nne inaupata Fountain Gate msimu huu baada ya kucheza mechi 15 ikiwa imepoteza nane na kutoka sare tatu, ikipanda nafasi mbili kutoka 15 hadi 13 ikifikisha pointi 15 ikiwa na wastani wa kupata pointi moja kila mechi.

Kwa upande wa Mbeya City, matokeo haya yamezidi kuiweka kwenye wakati mbaya zaidi ikishuka nafasi moja kutoka ya 13 hadi 12 ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 15, imeshinda tatu na sare nne na kupoteza nane.

Mbeya City msimu huu haijashinda mechi yoyote nyumbani kati ya saba ilizocheza, imetoka sare nne na kupoteza tatu, huku Fountain ikishinda mechi ya kwanza ugenini msimu huu kati ya nane ilizocheza, sare mbili na kupoteza tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *