
Unguja. Wakati ikiadhimishwa siku ya mazingira Afrika, Serikali imetaka kuongeza kasi ya kuhifadhi mazingira kwa kupanda na kutunza miti na udhibiti wa matumizi ya mifuko ya plastiki.
Pia, imewataka wananchi kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, matumizi bora ya ardhi kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji pamoja na kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya mazingira kwa umma.
Machi 3 ya kila mwaka, Bara la Afrika huadhimisha siku ya mazingira Afrika.
Hayo yamebainishwa leo Machi 3, 2025 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni wakati akitoa kauli ya Serikali kwa waandishi wa habari Zanzibar kuhusu siku ya mazingira Afrika.
“Kwa kutumia jukwaa la siku hii ya kielelezo ya mazingira ya Afrika, natoa rai kwa wananchi wote kuongeza kasi ya kuhifadhi mazingira kwa shughuli mbalimbali ikiwemo, upandaji na utunzaji miti, kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na matumizi bora ya ardhi,” amesema Masauni.
Pia, ametaka viongozi wa mikoa na halmashauri kuhamasishana na kuelimisha jamii kwenye masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira hususani kutumia nishati mbadala wa mkaa, majiko banifu pamoja na njia sahihi za kuhifadhi taka.
“Tanzania yetu ni hii moja hatutakuwa na sehemu nyingine zaidi ya hii, hivyo suala la hifadhi ya mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo,” amesema Masauni.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘Uhakika wa upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa mazingira ili kufikia Malengo ya Ajenda 2063.”
Masauni amesema kwa kutambua uhalisia huo, Serikali imedhamiria kufungamanisha kwa vitendo masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.
Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 Tanzania inaweza kuwa na watu takriban milioni 120, ikimaanisha kuwa mahitaji ya rasilimali, makazi, ajira, maji, huduma ya afya, nishati pamoja na huduma za kiikolojia itahitajika kuwa mara mbili ya sasa.
Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina watu milioni 61.7, na hivyo kuwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.
“Tukumbuke kuwa huduma zote hizo zitakazotakiwa kuwa mara mbili zaidi ya sasa kwa kipindi hicho zitatokana na ardhi hiihii ya nchi yetu ambayo haitaongezeka hata hatua moja,” amesema.
Nao baadhi ya wadau wa mazingira wamesema ipo haja kuweka msukumo katika kuhifadhi mazingira, kwani bado elimu ya mazingira inaonekana bado kuhitajika kwa kiasi kikubwa.
“Suala la mazingira ni mtambuka, kuna elimu kubwa inahitajika sio tu kwa wananchi hata taasisi mbalimbali bado kuna uharibifu wa mazingira hasa katika shughuli mbalimbali za maendeleo,” amesema Masoud Makame mdau wa mazingira Zanzibar