Arusha. Mwili wa mwanafunzi wa darasa la nne, Shule ya Msingi Terrat, Daniel Massawe (11) umeagwa mkoani Arusha huku Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Sinoni Jimbo Kuu la Arusha, Firmini Rudovic akisema hakuna wa kulaumiwa kwa kifo chake.
Daniel alifariki dunia Februari 27, 2026 wakati akivuka korongo kwenda shuleni na mwili kuopolewa umbali wa mita 500 kutoka eneo la tukio.
Leo Jumanne, Machi 3, 2026, imefanyika misa ya kuuaga katika Kigango cha Mtakatifu Mathias Mulumba Terrat ambapo Padri Rudovic amesema: “Kunapotokea matukio ya namna hii mara nyingi tunatafuta wa kumlaumu, tusitafute mtu wa kulaumu kwenye hili jambo tuendelee kumwombea, Daniel tukijua ameenda mbinguni.”
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Terrat jijini Arusha wakitoa salamu za mwisho kwa mwili wa mwenzao, Daniel Joseph Massawe wakati wa misa iliyofanyika leo,mwanafunzi huyo alifariki kwa kusombwa na maji wakati akielekea shuleni siku ya Ijumaa wiki iliyopita. Picha na Filbert Rweyemamu
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mashariki Kata ya Muriet, Emmanuel Sanare akitoa salamu za rambirambi amewataka wananchi kuchukua tahadhari kabla ya kuwaruhusu watoto wao kwenda shule au wahakikishe wamewafikisha hasa katika kipindi cha msimu wa mvua.
“Niwaombe walimu katika kipindi hiki cha msimu wa mvua mahudhurio yanapokuwa si mazuri mfahamu wazazi wamechukua tahadhari za kiusalama kwaajili ya kuwalinda watoto wao,” amesema Sanare.
Misa ya maziko inatarajiwa kufanyika Kijiji cha Manda Chini, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro kesho Jumatano Machi 4, 2026.