
Mbeya. Hivi kama mama utaumia kiasi gani unapomkuta papo hapo, mpenzi wako anambaka mtoto wako mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja? Hii ndio hali alikutana nayo mama huyu mkazi wa Kijiji cha Mawelu, Chunya mkoani Mbeya.
Unajua katika utetezi wake mbakaji alisemaje, alikana kufanya kitendo hicho akidai siku ya tukio alirudi Chunya akitoka kuchukua dawa za kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi (ARV), akapitia baa kupata kinywaji, kisha akarudi zake nyumbani.
Tukio hilo lilitokea Desemba 19, 2017 katika eneo la Mnazi Mmoja, kitongoji cha Mawelu Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Baada ya Mahakama ya Wilaya ya Chunya kusikiliza ushahidi, ilimtia hatiani Jullius Joseph na kumhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela, akakata rufaa Mahakama Kuu akagonga ukuta na sasa amekwaa tena kisiki Mahakama ya Rufani.
Ni kutokana na uzito wa ushahidi hasa kwa kuwa alikutwa moja kwa moja akiwa ameshambaka mtoto huyo na alikuwa anampaka mafuta arudie mara ya pili, Mahakama ya Rufani jijini Mbeya, imebariki kifungo cha maisha alichopewa.
Hukumu hiyo ambayo imewekwa katika tovuti ya Mahakama leo Machi 3, 2026, ilitolewa Februari 27, 2026 na jopo la majaji watatu – Rehema Kerefu, Lucia Kairo na Deo Nangela wa Mahakama ya Rufani walioketi Mbeya.
Tukio lilitokeaje
Kulingana na kumbukumbu za shauri hilo, ushahidi unaonyesha kuwa siku ya tukio saa 12:00 jioni, mama wa mtoto ambaye alikuwa shahidi namba 1 wa Jamhuri, alikuwa akiishi hapo Mnazi Mmoja na watoto wake, akiwamo aliyebakwa.
Muda huo wa saa 12:00 jioni, mama huyo aliondoka kwenda kisimani kuchota maji na kuwaacha watoto wake mapacha wa kiume na wa kike nyumbani kwa jirani yake aitwaye Ndele Ponali na aliporudi alibaini mmoja hayupo alipowaacha kwa mama Rahabu.
Ni kulingana na ushahidi wake, mama Rahabu alimwambia ni Joseph alikuwa amemchukua mtoto huyo na kwamba anakwenda naye katika duka la kuuza pombe za jadi kununua mafuta.
Mama huyo haraka alikwenda katika duka hilo, lakini hakumuona mwanamme huyo wala mtoto wake ndipo alipoamua kwenda moja kwa moja nyumbani kwa mwanamume huyo na akiwa nje ya nyumba alimsikia mtoto wake akilia ndani.
Alipochungulia ndani kupitia dirishani, alimuona mtoto wake huyo wa amelala akiwa uchi katika kipande cha ubao, huku mwanamme huyo naye akiwa uchi, huku akiwa anampaka mafuta mtoto huyo sehemu za siri.
Akiwa katika hali ya taharuki aliingia ndani ya nyumba hiyo akipiga mayowe ya kuomba msaada na haraka alimchukua mtoto na wakati huohuo mwanamme huyo naye alivaa nguo zake haraka na kutoroka kijijini kwa miezi sita.
Mama huyo alieleza wakati anamchukua mtoto wake, mwanamme huyo alikuwa tayari amembaka na alikuwa anajiandaa kurudia na alipomchunguza mtoto wake sehemu za siri, alimkuta na manii, matone ya damu, mafuta na michubuko.
Alitoa taarifa kwa shahidi wa 4 wa Jamhuri, Gerald Ng’umbi ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa kitongoji ambaye aliitisha mkutano wa wanakijiji ili wasaidie kumtafuta Joseph na baadaye suala hilo likatolewa taarifa Polisi.
Mtoto alipatiwa Fomu ya Polisi (PF3) na alipelekwa hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa uchunguzi ambao ulifanywa na Moris Mdoe aliyekuwa shahidi wa pili wa Jamhuri ambaye alithibitisha mtoto huyo kuingiliwa na kitu butu sehemu za siri.
Kwa kuwa mbakaji huyo alitoroka eneo la tukio, mama wa mtoto huyo alipewa namba ya jalada la shauri (RB number) ambapo Mei 2018 mwanamme huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kumbaka mtoto huyo.
Mashahidi wengine wa Jamhuri wakiwamo majirani, ushahidi wao uliunganika na ule wa mama wa mtoto na kueleza namna walivyomkuta mtoto na manii.
Alivyojitetea kortini
Katika utetezi wake mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Chunya, mwanamme huyo alikiri kumfahamu mama wa mtoto huyo na kueleza kuwa ni jirani yake na kudai kuwa alikuwa ni mpenzi wake.
Alijiweka kando na tuhuma alizokuwa anakabiliwa nazo na kupinga ushahidi wa shahidi namba 1,3 na 4 na kudai walitoa ushahidi wa uongo na amebambikiwa kosa hilo kutokana na chuki baada ya yeye kujiunga na programu ya TASAF.
Mahakama ya Wilaya ya Chunya ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha jela, kifungo ambacho kimeendelea kumng’ang’ania hata alipokata rufaa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Katika sababu za rufaa katika mahakama ya rufani, mwanamme huyo alidai mahakama za chini zilishindwa kuzingatia sababu zake za rufaa, kesi ya Jamhuri haikuthibitishwa na Jamhuri kushindwa kuita mashahidi wa msingi kortini.
Uamuzi wa jopo la majaji
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo mbele ya majaji watatu, mrufani alijiwakilisha mwenyewe bila wakili huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Lordgud Eliaman, ambaye kimsingi alipangua sababu hizo za rufaa.
Katika hukumu yao, majaji hao walisema kuhusu hoja kuwa mahakama za chini kutozizingatia sababu zake za rufaa, madai hayo hayaungwi mkono na kumbukumbu za mwenendo wa shauri hilo kwani hoja zake zilizingatiwa.
Hoja ya pili na ya tatu alidai kuwa kesi ya Jamhuri haikuthibitishwa katika viwango vya bila kuacha mashaka kwa sababu Ndele Ponali na mtoto aliyembaka hawakuitwa kutoa ushahidi na pia umri wa mtoto haukuthibitishwa kortini.
Majaji hao walisema baada ya kupitia kumbukumbu za mahakama, wameridhika kuwa mahakama mbili za chini zilizingatia kikamilifu ushahidi wa pande mbili na kwamba upande wa Jamhuri ulithibitisha shitaka bila kuacha mashaka.
Walirejea ushahidi wa shahidi namba 1 wa Jamhuri ambaye ni mama wa mtoto, ambaye alieleza mwanzo mwisho wa nini kilichotokea.
Walikubaliana na hoja za wakili wa Serikali kuwa kulingana na kifungu cha 152 cha sheria ya Ushahidi, hakuna idadi kamili inayotajwa ya mashahidi wanatakiwa kuthibitisha taarifa bali kinachoangaliwa ni uzito wa ushahidi.
Majaji hao walisema matendo ya mrufani ikiwamo kutoroka eneo la tukio kwa miezi sita kama ushahidi unavyoeleza ni ishara tosha kuwa ana hatia ya kutenda kosa hilo hivyo hawaoni sababu ya kubatilisha kifungo anachokitumikia.