
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf ametangaza mipango ya kukijenga upya chama hicho kupitia maridhiano ya ndani yatakayolenga kumaliza migogoro ya muda mrefu iliyokikumba.
Mbali na hilo, amesema anatarajia kufanya marekebisho ya katiba ya chama, hususan katika eneo la kuwatambua na kuthamini mchango wa viongozi waliowahi kukitumikia. Kwa mujibu wa Mirambo, viongozi waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CUF hubaki kama wanachama wa kawaida baada ya kumaliza muda wao wa uongozi, bila kupewa heshima inayostahili kulingana na mchango wao.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 3, 2026 katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Makao Makuu ya chama hicho Buruguruni jijini Dar es Salaam, Mirambo amesema kipaumbele chake kikuu ni kukijenga chama na kukiondoa katika migogoro ya ndani.
Amesema wakati akiomba kura kwa wajumbe hao, aliweka wazi kuwa hana makundi ndani ya chama na kwamba dhamira yake ni kuwaunganisha wanachama wote.
Hivyo, ameahidi kuwa moja ya majukumu yake makubwa baada ya kuchaguliwa ni kuimarisha umoja na mshikamano.
“Baada ya kuchaguliwa nilitoa kauli mbili; kwanza kufanya maridhiano ndani ya chama na pili kufanya ziara mikoani kuwatembelea wanachama, kuamsha ari mpya, kuongeza idadi ya wanachama na kuwahamasisha waliokata tamaa kurejea katika mstari,” amesema.
Amefafanua kuwa maridhiano hayo yanawalenga pia wale waliojiweka kando, akisisitiza umuhimu wa kuwarudisha ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa chama.
Amesema lengo la CUF si kubaki chama kikuu cha upinzani, bali kushika dola.
“Tunafikiria kwenda kuchukua dola na ili tufikie hatua hiyo, tunahitaji kuunganisha makundi yote. Hakuna haja ya kuendelea kuwa na makundi tangu mwaka 2010; umefika wakati wa kuyavunja na kuacha kuyaendeleza,” amesema.
Amebainisha kuwa makundi yamekuwa yakikigharimu chama na kudhoofisha juhudi za kukijenga. Na katika mkakati wa kuimarisha umoja, amesema uteuzi wa viongozi utafanyika kwa kuzingatia uwezo na sifa binafsi, bila kujali itikadi au makundi wanayotoka.
Amesema tayari wameanza kutekeleza mkakati huo kwa kuwateua baadhi ya viongozi waliokuwa katika uongozi wa mtangulizi wake, Profesa Ibrahimu Lipumba, akiongeza kuwa hata katika ofisi za chama hakuna mabadiliko makubwa ya watendaji.
“Tutaendelea kufanya kazi na viongozi waliokuwapo kwa kuwa lengo letu ni moja. Hakuna mgogoro unaoweza kumalizika bila maridhiano ya mezani,” amesisitiza.
Kuhusu wanachama waliokihama chama kutokana na changamoto za uongozi uliopita, amesema milango iko wazi kwao kurejea na kushiriki katika mapambano ya kukijenga upya chama hicho.
“Lazima tufanye maridhiano, tusameheane na kupata suluhu ya kudumu ili tusonge mbele kwa taswira moja inayoonyesha dhamira ya dhati ya ofisi kuu,” amesema.
Ameongeza kuwa endapo chama kitaimarisha umoja, hata changamoto za kifedha zinazowakabili kwa sasa zitapungua kwa kuwa wadau na wafadhili watajitokeza kukiunga mkono.
Kuenzi viongozi waliopita
Akizungumzia namna ya kumuenzi Profesa Lipumba, Mirambo amesema kamati ya uongozi itakutana na kujadili jambo kubwa la kufanya kwa heshima yake, kabla ya kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye Baraza Kuu kwa ajili ya kupitishwa rasmi.
Amesema Profesa Lipumba katika kipindi cha miaka 27 ya uongozi wake ndani ya CUF, amewaandaa na kuwalea viongozi wengi waliokitumikia chama hicho katika nyadhifa mbalimbali.
“Tutapitisha maamuzi yetu ndani ya kamati ya uongozi kisha tutayapeleka Baraza Kuu ili kuamua rasmi namna ya kumuenzi ndani na nje ya chama. Ni lazima tupange vizuri, suala la kumuenzi ni muhimu; kutomuenzi ni kuibua tena migogoro,” amesema Mirambo.
Amesema kutomtambua kiongozi aliyewahi kuongoza chama ni chanzo cha migogoro na ameahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi, ataweka utaratibu wa kuhakikisha mchango wa viongozi waliopita unatambuliwa na kuthaminiwa rasmi.
Kwa mujibu wa Mirambo, viongozi watakaotambuliwa ni pamoja na wenyeviti na makatibu wakuu wote waliowahi kukiongoza CUF. Amesema hatua hiyo itawekwa kwa maandishi ili iwe sehemu ya kumbukumbu na utamaduni wa chama.
“Tutaweka bayana kwenye maandishi kuwa huyu ndiye mwenyekiti aliyepita. Hata katika vikao vyetu tutaangalia namna ya kuboresha utaratibu ili waweze kuhudhuria pale afya zao zinapowaruhusu. Hawa ni wenzetu na dhamira yetu ni moja,” amesisitiza.
Amefafanua kuwa ili utaratibu huo uwe halali na endelevu, lazima kufanyika marekebisho ya katiba ya chama, kwa kuwa kwa sasa hakuna kifungu kinachowatambua rasmi viongozi waliowahi kukitumikia chama hicho.
“Lazima tuweke mfumo wa wazi. Usipoenzi, nawe huenziwi. Natarajia kufanya mazuri na nitakapoondoka niwe sehemu ya mfumo huo huo. Haiwezekani kuendelea bila utaratibu thabiti wa kujenga kizazi kijacho; tutawaenzi kwa mujibu wa katiba waliotutangulia,” amesema.
Ameongeza kuwa hata viongozi waliowahi kuondoka ndani ya chama hicho kutokana na changamoto au tofauti za kiutendaji, hawatapuuzwa, bali watawekewa utaratibu wa kutambuliwa bila ubaguzi.
Katika hatua nyingine, Mirambo amewaomba Watanzania kukiunga mkono chama hicho, akisema kina uwezo wa kuongoza dola.
“Tuna watu wenye uwezo wa kuingia Ikulu ya Tanzania Bara na ya Zanzibar. Niwaombe Watanzania waondokane na dhana kwamba hatuwezi kuunda Serikali; watuamini,” amesema.
Demokrasia
Akizungumzia suala la demokrasia, Mirambo amesema kwa Tanzania inakabiliwa na changamoto huku akisisitiza kuwa ukuaji na uimara wake hauwezi kupatikana kwa wakati mmoja bila jitihada za makusudi kutoka kwa wadau mbalimbali.
Amesema ni muhimu kuhakikisha mwananchi anapopata fursa ya kuzungumza, hususan katika mikutano ya hadhara, analindwa na kusikilizwa kwa uhuru bila vikwazo.
Kwa mujibu wake, eneo hilo bado linahitaji maboresho ili kuimarisha misingi ya demokrasia.
Kuhusu hali ya uchumi, Mirambo amesema wananchi wengi bado wanakabiliwa na ugumu wa maisha licha ya uwekezaji mkubwa wa miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa (SGR) na ununuzi wa ndege.
Amesema miradi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, lakini wananchi wengi hawana uwezo wa kumudu huduma zinazotolewa.
“Kwa sasa kuna matabaka, wachache ndiyo wana uwezo wa kunufaika moja kwa moja na huduma hizo, lakini Watanzania wengi bado wanahitaji uchumi huo uwafikie moja kwa moja na kuwasaidia kuboresha maisha yao,” amesema.
Amesisitiza kuwa moja ya njia za kuwainua wananchi ni kuanzisha na kuimarisha miradi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja, ili itengeneze mzunguko wa kipato kwa wananchi wenyewe.
“Miradi ya kiraia huleta fedha kwa wananchi. Kwa mfano, inapofanyika semina ya uzalendo kwa vijana, hushirikisha vijana hao na kuwapatia kipato. Inapaswa kufika wakati vijana waweze kuboresha maisha yao hata kwa kubadilisha mavazi wanayovaa, jambo ambalo kwa sasa linashindikana kutokana na hali duni ya uchumi wao,” amesema.
Ameongeza kuwa vijana wengi hawana matumaini ya kesho bora na bado wanaishi kwa kutegemea wazazi wao.
Hivyo, amesema ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira yatakayowezesha vijana kumiliki mali na kujitegemea kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Mirambo amesema ana mpango wa kuimarisha jumuiya za vijana, wanawake na wazee ndani ya chama hicho ili kujenga msingi imara wa uongozi na ushiriki mpana wa wanachama.
“Tutafanya uchaguzi kuanzia ngazi za chini hadi taifa ili kupata viongozi imara. Baada ya hapo, tutawapa fursa, hususan vijana, kujitokeza na kuonekana katika majukwaa ya kitaifa,” amesema.