Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahsusi kwa Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kujilinda kunapotokea misukosuko duniani.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Machi 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Maelekezo hayo ya mkuu wa nchi yametokana na mashambulizi yanayoendelea Mashariki ya Kati ambako Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuweka jiwe la msingi Mradi wa Ujenzi wa Matanki ya kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Machi 03, 2026.
Hata hivyo, Iran nayo ikalazimika kulipiza kisasi kwa Israel huku ikizilenga mali za Marekani zilizopo katika ukanda huo.
Mzozo huo ulioanza Jumamosi iliyopita, umesababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani ukizingatia kwamba, Mashariki ya Kati inachangia asilimia 20 ya mafuta katika soko la dunia.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo, Rais Samia ameitaka Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta huku akisisitiza hifadhi hiyo itaisaidia nchi inapotokea misukosuko duniani kama ilivyo wakati huu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo ya Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Machi 03, 2026.
“Wizara ya Nishati, iimarishe akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kujilinda dhidi ya misukosuko ya kimataifa na nishati ikiwamo mabadiliko ya bei katika soko la dunia.
“Kama tunavyoona misukosuko iliyotokea wiki iliyopita na tunayoendelea nayo, tayari imeshapandisha bei ya mafuta kwa asilimia 13 mpaka jana, sasa hatujui leo na siku zinazokuja, lakini tumuombe Mungu watu wale wakae juu ya meza wazungumze, wakubaliane, misukosuko iishe ili dunia irudi katika hali ya kawaida kuendesha uchumi wa nchi zetu,” amesema Rais Samia.
Kutokana na mabadiliko hayo, Rais Samia amesisitiza kwamba, ni vema kukawa na mradi kama huo wa matanki ili kujihakikishia usalama wa nishati ya mafuta nchini.
Mbali na hilo, ameitaka Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi huo wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta unakamilika kwa wakati na kwa viwango huku akiweka msisitizo huo kwa makandarasi wa mradi huo.
Vilevike, ameitaka TPA kwa kushirikiana na taasisi nyingine kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji vipimo na ubora wa mafuta kuanzia yanaposhushwa hadi hatua za usambazaji ili kuongeza uwazi na kulinda mapato ya Taifa.
Wakati huohuo, Rais Samia amesema uamuzi wa kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari umeongeza ufanisi, mapato ya Serikali na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu.
Rais Samia amesema mafanikio yanayoonekana sasa ni matokeo ya uamuzi wa kimkakati wa kuingia ubia na wawekezaji binafsi katika baadhi ya magati ya Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema tangu Serikali iingie ubia na Kampuni ya DP World pamoja na EA Gateway, ufanisi wa bandari umeongezeka, meli zinazohudumiwa zimeongezeka na mapato ya forodha yamepanda kwa kiwango kikubwa.
“Mapato ya Serikali kupitia kodi za forodha yameongezeka kutoka Sh7.3 trilioni mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh12.31 trilioni mwaka 2024/25. Huu ni ushahidi kuwa ushirikishwaji wa sekta binafsi umeongeza tija na kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa fedha zilizookolewa kupitia maboresho ya uendeshaji sasa zinaelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo ya bandari, ikiwamo mradi huo wa matanki ya mafuta utakaosaidia kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi nishati na kukabiliana na misukosuko ya bei katika soko la dunia.
Rais Samia amesema Tanzania imekusudia kutumia jiografia yake kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bahari, akitaja kuwa maboresho ya bandari, reli ya kisasa (SGR) na barabara yameongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kimataifa.
“Zamani tulikuwa tunapokea meli ndogo ndogo, lakini sasa tunapokea meli kubwa zaidi. Na tutakapojenga Bandari ya Bagamoyo, hakuna meli ambayo Tanzania haitoweza kuipokea,” amesema na kuongeza;
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Machi 03, 2026.
“Matokeo ya ushirikishwaji wa sekta binafsi yapo wazi bandari yetu inahudumia shehena kubwa zaidi, ufanisi umeongezeka na biashara zimefunguka ukilinganisha na tulivyokuwa, kubwa zaidi kumeongezeka kasi ya mpango mkakati wa uendelezaji wa bandari zetu mpango unaenda mpaka mwaka 2040, lakini utekelezaji wake ulikuwa unaenda polepole kwa kushirikisha sekta binafsi utekelezaji wake unaenda kwa kasi kubwa.”
Rais Samia ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi wa matanki ya mafuta kutaimarisha usalama wa nishati na kutekeleza ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya 2025/30 ya kuimarisha miundombinu ya kisasa ya usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa muhimu.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wizara yake imeendelea kuimarisha mnyororo wa sekta ya uchukuzi kwa kuhakikisha reli ya kisasa (SGR) inaanza kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Dodoma, Morogoro na mikoa mingine ili kupunguza msongamano bandarini.
Amesema ushirikiano na sekta binafsi umeongeza kasi ya uondoshaji mizigo na kuongeza mapato ya mamlaka za bandari siku hadi siku.
“Serikali tangu ilipoingia ubia na DP World na EA Gate Way kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli katika baadhi ya magati Bandari ya Dar es Salaam, ufanisi umeongezeka na kumekuwa na ongezeko la meli zinazoshusha mizigo, mizigo imeongezeka na mapato yameendelea kuongezeka,” amesema Mbarawa.
“Ninaomba nikuhakikishie Wizara itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya uchukuzi.”
Spika wa Bunge, Azzan Zungu amesema ukuaji wa uchumi umeongezeka kutoka asilimia 3.1 hadi 6.2, akieleza kuwa, uwekezaji katika miundombinu ya bandari ni kichocheo muhimu cha kufikia lengo la ukuaji wa asilimia 8 hadi 9.
“Uwekezaji wa DP World ulipigiwa kelele sana, lakini leo mpaka mwaka jana TPA mapato yao ilikuwa bilioni 800 mpaka trilioni 2 wanaweza sasa kuchangia uchumi kwa mapato wanayoyapata, nchi inasonga mbele na uwekezaji uliowekwa Tanzania.”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiagana na wananchi mara baada ya kuwahutubia kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni Mnadani Jijini Dar es Salaam, Machi 3, 2026.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mradi uliozinduliwa leo utaongeza uwezo wa Taifa kuhifadhi mafuta na kuimarisha usalama wa nishati, huku akibainisha kuwa ongezeko la shehena na meli bandarini limeleta changamoto ya foleni ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya bandari.
Mradi wa matanki hayo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania kuhudumia nchi jirani zikiwemo Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku ukichochea zaidi nafasi ya nchi kuwa kitovu cha biashara kikanda na kimataifa.