Dodoma. Serikali imesema licha ya kutoa fursa kwa vijana kupata mafunzo ya uanagenzi bila gharama, mwitikio bado ni hafifu.

Hata hivyo, imetangaza mkakati wa kuwaunganisha zaidi ya vijana 6,000 katika fursa za kimataifa, ambapo awamu ya kwanza vijana 1,000 watakwenda kufanya kazi nchini Qatar.

Kauli hiyo imetolewa Jumanne Machi 3, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu wakati akizindua mafunzo ya uanagenzi awamu ya nane kwa mwaka 2025/26 katika Chuo cha Don Bosco Technical Training Centre Dodoma, kwa niaba ya vyuo 46 vinavyotekeleza programu hiyo nchini.

Waziri Sangu amesema Serikali imetenga Sh4.3 bilioni katika bajeti ya 2025/26 kusaidia vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo ya muda mfupi na urasimishaji wa ujuzi, lakini akaeleza masikitiko yake kuwa wengi hawachangamkii fursa hiyo.

Amesema mkakati huo ni wa kudumu na kwamba vijana wakiona wenzao wakifanikiwa katika ajira au kujiajiri, watahamasika kujiunga ili kujenga ubora unaokubalika katika soko la ajira. “Mwitikio ni hafifu, lakini hawa wachache wakipata mafunzo bora na kukubalika kwenye masoko, wengine watafuata, kama ilivyo kwa baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu wanaokimbilia fursa hizi,” amesema.

Amewataka vijana kujenga uaminifu, ubunifu na kujiamini katika zama za sayansi na teknolojia, badala ya kuogopa mabadiliko. Pia ametangaza kuwa katika bajeti ijayo Serikali itaongeza fedha ili kufikia malengo makubwa zaidi.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa vyuo vinavyotekeleza programu hiyo, Mkuu wa Chuo cha Don Bosco Dodoma, Justin Mulebya, amesema vyuo vinaendelea kubuni mbinu bora za kuhakikisha vinatimiza malengo ya Serikali kwa kuwa gharama muhimu tayari zimetolewa.

Hata hivyo, ameomba Serikali itenge bajeti ya kuwawezesha wahitimu kupata vifaa vya kuanzia kazi ili kuwasaidia kujitegemea na kuvutia wengine kujiunga na mafunzo hayo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa waajiri wa sekta binafsi, Joseph Kimweri, amesema ubora wa mafunzo unaotolewa unatosha kuwaingiza vijana kwenye soko la ajira, lakini akashauri kuimarishwa zaidi kwa mafunzo ya ukarimu hasa kwa sekta ya hoteli.

Amehimiza vijana kuwa na mawazo bunifu na ndoto kubwa, wakilenga siyo tu kuajiriwa bali pia kuajiri wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *