Unguja. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar imesema imewezesha vikundi 6,700 vya wajasiriamali Unguja na Pemba kupitia programu ya Dk Mwinyi Boasting Fund.

Kupitia programu hiyo, imetoa mikopo nafuu ya Sh2.8 bilioni,  yenye lengo la kuwawezesha kiuchumi wajasiriamali wanawake katika vikundi mbalimbali.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Machi 3, 2026 na Waziri wa wizara hiyo, Anna Athanas Paul katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea mafanikio ya siku 100 za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, uliofanyika katika ukumbi wa Idara Habari Maelezo Zanzibar.

“Mikopo hiyo ya riba nafuu inatolewa kwa wajasiriamali wadogowadogo kwa kima cha Sh500, 000 kwa mtu mmoja mmoja ambaye amejiunga na kikundi kwa lengo la kumuinua kiuchumi,” amesema. 

Pia, amesema wizara hiyo imefanikiwa kuwaunganisha wanawake kwa pamoja kupitia majukwaa ya shehia ili kufikia fursa za masoko ya bidhaa wanazozitengeneza.

Mbali na hilo, wizara hiyo imesema imeanzisha madawati ya jinsia katika vikosi maalumu vya SMZ ikiwemo Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM).

Amesema, madawati hayo yameanzishwa kwa lengo la kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake ndani ya vikosi hivyo.

Amefafanua kuwa, wanawake wanaokutana na vitendo vya unyanyasaji watapata nafasi ya kuelezea changamoto zao kwenye dawati hilo na kuzitafutia ufumbuzi.

Vilevile amesema, wizara hiyo imepokea kesi 212 za mvutano wa malezi baada za wazazi kuachana, hivyo ametoa wito wa ustahamilivu katika ndoa ili wasiwatese watoto ambao ni waathirika wakubwa baada ya ndoa kuvunjika.

Waziri Anna amewataka wananchi kuwalea watoto wenye mazingira magumu kwa lengo la kupata furaha na upendo wa jamii badala ya kuwapeleka kwenye vituo vya kulelea watoto.

Amesema, watoto hao wanapokuwa katika vituo hivyo wanakosa furaha na hawapati malezi ya jamii.

Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhani Abdallah amesema ni wakati sahihi kwa wanaume kuwawezesha wanawake na sio kuwaona kuwa ni chombo cha starehe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *