Marekani. Moja ya katuni inayokubalika wakati wote ni ‘Tom and Jerry’. Mbali na maudhui yake kuwavutia wengi, kipo kilichoifanya ionekana bora ikiwemo muziki uliotumika nyuma ya katuni hiyo.
Muziki huo ulitengenezwa na msanii Scott Bradley, ambaye alipambana kwa kila hali kutafuta nafasi hiyo ambayo wasanii wengi walitamani kuipata.
Scott Bradley alizaliwa mwaka 1891 nchini Marekani. Tangu utotoni alipenda sana muziki, hasa upigaji wa kinanda na muziki wa classical. Alijifunza muziki kwa bidii na baadaye akaanza kazi yake kama mpiga kinanda na mpangaji wa muziki, akishiriki katika maonyesho mbalimbali pamoja na filamu za mwanzo za Hollywood.
Ingawa alikuwa na kipaji kikubwa, mafanikio hayakuja haraka kwani wakati huo muziki wa katuni haukupewa uzito mkubwa.
Miaka ya 1930 mambo yakaanza kubadilika alipofanikiwa kupata kazi katika studio kubwa ya filamu ya Metro-Goldwyn-Mayer (MGM). Huko alianza kutengeneza muziki wa katuni mbalimbali, akijijengea sifa ya kuwa mtunzi aliyekuwa tofauti na wengine.
Bradley aliweka background mbalimbali katika picha zake na za watu mashughuli. Ambapo alitumia sauti tofauti ikiwemo mshangao, kuanguka, kukimbia pamoja na muziki uliyokuwa ukisisimua hisia za watu.
Picha ya Scott Bradley mtayarishaji wa muziki kwenye Tom and Jerry
Mwaka 1940, watayarishaji wa katuni William Hanna na Joseph Barbera walikuwa wakianzisha katuni mpya kuhusu paka na panya waliokuwa wakifukuzana. Walihitaji kitu cha kipekee kitakachofanya katuni hiyo ichekeshe hata bila mazungumzo mengi.
Ndipo jina la Scott Bradley likapendekezwa kutokana na ubunifu wake uliokuwa tayari umeonekana ndani ya MGM. Bradley alipewa nafasi ya majaribio kutengeneza muziki katika sehemu za mwanzo za katuni hiyo.
Alikaa na kinanda chake, akitazama kila tukio katika katuni hiyo. Kisha akaandika muziki ambao uliendana kabisa na vitendo vya Tom and Jerry jambo ambalo liliwashangaza waandaaji wa katuni hiyo.
Baada ya jaribio hilo kukubalika na timu nzima ya waandaji wa katuni hiyo, Bradley aliteuliwa rasmi kuwa mtunzi mkuu wa muziki wa Tom and Jerry. Aidha kwakua kidole kimoja hakivunji chawa Bradley aliamua kushirikiana na wanamuziki wengine kutengeneza na kuchanganya muziki wa classical na Jazz ili kutengeneza sauti tofauti ambayo iliendana na harakati zote za Tom and Jerry.
Aidha kutokana na ubunifu huo miaka kadhaa mbele Tom and Jerry ilipata mafanikio makubwa duniani na kushinda tuzo kadhaa za Academy Awards. Huku muziki wa Bradley ukitajwa kuwa moja ya siri kubwa ya mafanikio hayo.
Scott Bradley aliendelea kufanya kazi hiyo kwa miongo kadhaa hadi alipostaafu. Msanii huyo alifariki dunia Aprili 27, 1977 akiwa na umri wa miaka 85 huku sababu ya kifo ikiwa ni uzee na wala hakuugua maradhi yoyote.
Mbali na kutengeneza muziki kwenye Tom and Jerry, Bradley pia alihusika kutengeneza muziki katika katuni nyingine nyingi za studio ya MGM, zikiwemo Droopy, Barney Bear, Screwy Squirrel pamoja na Happy Harmonies.