Marsabit Kaunti, iliyoko Kaskazini mwa nchi ya Kenya, iko mpakani na nchi ya Ethiopia. Kaunti hii ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini Kenya baada ya ile ya Turkana wakazi wake wengi ni wafugaji, na mbali na changamoto za mabadiliko ya tabianchi wanawake wa hapa wamepitia masahibu ya ukeketaji au kwa lugha ya kiingerza Female genital mutilation (FGM). 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA) chini ya Ufadhili kutoka Muungano wa Ulaya nchini Kenya wanatekeleza mradi uitwao Komesha FGM SASA 

Kila muathirika wa ukeketaji anayo hadithi ya kusimulia na ndio maana kwa namna ya kipekee mradi huu unawatumia waathirika hao, kuwaelimisha wanajamii wenzao ili kuondokana na tamaduni ya ukeketaji. Prisca Lekuraki ni mmoja wao. 

“Mimi nilipitia magumu sana, baada ya kukeketwa nilipata shida sana, ni Mungu ndio amenisaidia mpaka nimefika hapa. Nilipoenda kujifungua mtoto wangu wa kwanza nilipata shida sana, kila nikienda kuzaa nikawa napitia shida sana, sasa hivi nina watoto watatu na nikajifunga nisizae tena. Niliona vile nimeumia nikasema siwezi kukubali binti yangu naye aumie hivyo. Na hiyo ndio ilinifanya niamke niungane na wengine kuhamasisha kukataa ukeketaji.”

Ameongeza kuwa katika tamaduni zao wanamila nyingi nzuri sana na wanaweza kuziendeleza na kuachana na hii mila moja ya ukeketaji kwani ni mbaya na inamadhara. 

Prisca amepongeza mradi wa Komesha FGM SASA wa UNFPA kwa kuwasaidia kuwafikia wale ambao awali ilikuwa ni vigumu kuzungumza nao.

“Kuna mahali wametufikisha na tumeona mafanikio, hapo awali tulikuwa tunaweza kwenda kwa wamama, vijana na watoto ila wale watu ambao ilikuwa inatushinda kuwafikia ilikuwa ni wazee. Lakini hii kukutana na wazee, wamama na wanakijiji kwa ujumla imesaidia, kwasababu nilikutana na wakina mama wakaniambia ile kitu mlikuwa mnasema tumeona ni uhalisia na tumeona inaweza kufanyika.”

Mwingine aliyeathirika na ukeketaji ni Nasarai Learo anasema ukeketaji umechukua nguvu zake.

“Mimi sina nguvu kama yule mama ambaye hajakeketwa, nilienda kuwaambia wamama wasikekete watoto wao, lakini wakaniambia wananifahamu na nilipoolewa nilkuwa mdogo sana na wao ndio walionishika nikatetetwe nikiwa mdogo. Lakini mimi niliwaeleza mimi sikuwa najua hiki kitu ni kibaya lakini sasa hivi nimekuwa na elimu na nimejua ubaya wake.”

Nasarai anaamini kuwa iwapo jamii itapata elimu basi itabadilika

“Jamii yetu sanasana haina elimu, tukiona jamii yetu watu wachache ndio wamesoma na wengi wakisoma watapata hiyo elimu zaidi na watakuja kuikomesha FGM. Mimi naamini kwamba miaka 10 inayokuja mambo ya kukeketa wasichana hatutasikia tena.” 

Elimu ya kutokomeza ukeketaji inatolewa katika maeneo mbalimbali ikiwemo masokoni, katika vikao vya jumuiya na mashuleni. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *