Ikiwa leo ni siku ya tano tangu Marekani na Israeli zianze mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran, na kisha Iran kujibu mashambulizi, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema  hali si hali kwani watu wanaendelea kufurushwa sio tu ndani ya Iran, bali pia nchi jirani kama vile Lebanon kwani mashambulizi yamesambaa maeneo ya Mashariki ya Kati, huduma za afya nazo zikitwamishwa.

Karolina Lindholm Billing, Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, UNHCR akiwa  yuko katikati ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut kwenye kituo cha serikali ambako watu wanakimbilia kusaka hifadhi amesema tayari kuna watu takribani 300 waliokimbia mjini Beiruti tangu jana kufuatia mashambulizi kutoka Israeli. 

Walebanon wengine kwa mujibu wa UNHCR nchini Syria wamekimbilia Syria.

Unaweza kujiuliza taifa lililovamiwa ni Iran, lakini kulikoni Lebanon inashambuliwa? Hii ni kwa sababu wapiganaji wa kundi la Hezbollah walioko kusini  mwa Lebanon wameshambulia Israeli kufuatia kuuawa kwa Kiongozi wa Iran

UNHCR imejizatiti kushikamana na Lebanon

Bi. Billing kupitia video ya UNHCR iliyochapishwe mtandao wa X zamani Twitter akizungumza huku video ikionesha hekaheka za wakimbizi wakitembea na wengine wakipokea misaada anasema, katika kipindi cha saa chache, maelfu ya watu wamefurushwa makwao kusini mwa Lebanon, vitongoji vya kusini mwa Beirut an pia bonde la Bekaa.Familia zimeacha kila kitu makwao, kwa ushirikiano na serikali ya Lebanon, tumefika haraka kusaidia familia ambazo zilikuwa zinasaka usalama.

Hakikisho la usaidizi kwa Lebanon kutoka UNHCR linawekwa bayana na Bi. Billing akisema, UNHCR iko tayari kuongeza usaidizi wetu, lakini mshikamano endelevu wa kimataifa unahitajika kusaidia Lebanon wakati huu muhimu ili familia za wakimbizi, walebanon na wakimbizi wapate ulinzi, msaada na utu. Na zaidi ya yote raia walindwe wakati wote. UNHCR itaendelea kushikamana na raia wa Lebanon.”

Watoto nchini Lebanon wakumbwa katikati ya mzozo

Watoto saba wameuawa na wengine 38 wamejeruhiwa katika saa 24 zilizopita kufuatia kuongezeka kwa mapigano nchini Lebanon, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Umma ya taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini Lebanon, Marcoluigi Corsi, amesema mashambulizi mapya ya anga yamesababisha watu takribani 60,000 kukimbia makazi yao, wakiwemo watoto 18,000, huku zaidi ya familia 12,000 zikikimbilia kwenye zaidi ya makazi 300 ya dharura nchini kote. UNICEF imelaani vifo hivyo na kuonya kuhusu athari kubwa kwa watoto. 

Tayari shirika hilo limeongeza kwa haraka msaada wake wa dharura kwa kupeleka timu za kutoa msaada haraka katika makazi ya wakimbizi ili kusambaza vifaa vya kuokoa maisha, pamoja na kusambaza dawa muhimu katika vituo vya afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Umma.

Mama anamshika mtoto wake mchanga karibu katika shule ya umma huko Mount Lebanon, Lebanon, kama sehemu ya msaada wa dharura wa UNICEF kwa familia za wakimbizi wanaotafuta makazi.

© UNICEF/Fouad Choufany

Mtoto wa kike amebebwa na mama yake wakiwa kwenye shule iliyogeuzwa kuwa makazi huko eneo la Mlima Lebanon, mashariki mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

Halikadhalika, UNICEF imepanua huduma za vitengo vya afya tembezi hadi 37 ili kutoa matibabu, chanjo na huduma za afya kwa familia zilizokimbia makazi yao. 

Msaada wa hospitali kwa watoto wachanga na wanaohitaji uangalizi maalum umeimarishwa, huku msaada wa kisaikolojia, huduma za ulinzi wa mtoto na elimu ya mtandaoni ukipewa kipaumbele katika makazi ya dharura.

Wahudumu wa afya wapoteza maisha Iran na Lebanon

Huko nchini Iran kwenyewe Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO Kanda ya Mashariki mwa Mediteranea Dkt. Hanan Balkhy, ameonya kuwa kusambaa kwa mzozo huo kunagharimu raia ukanda mzima

Kupitia ukurasa wa X, Dkt. Balkhy amesema mashambulizi katika zaidi ya miji 130 nchini Iran yamesababisha mamia ya vifo vya watu, huku watumishi wa afya wakiwa miongoni mwa waliopoteza maisha.

Huko Lebanon wahudumu wa afya watatu waliuawa na sita walijeruhiwa wakati wakienda kuhudumia majeruhi karibu na Tyre ambapo amesema sheria za kimataifa za kiutu katu hazisuruhusu mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya.

Hadi sasa hakuna mitambo ya nyuklia iliyovuja

Tukimulika shaka na shuku kuhusu kuvuja kwa mitambo ya nyuklia nchini Iran, hii leo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati  ya Atomiki, IAEA, Rafael Grossi ametoa hofu akisema kulingana na uchambuzi wa picha za satelaiti za hivi karibuni zilizopo, IAEA haioni uharibifu wowote katika vituo vyenye nyenzo za nyuklia nchini humo na hivyo hakuna hatari ya kuachiliwa kwa mionzi kwa sasa hata kwenye vituo vya Isfahan, Natanz na Bushehr.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *