Asubuhi ya Ijumaa, Januari 23, 2026 kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam kulikuwa na tukio kubwa na la kipekee. Kulikuwa na hali ya utulivu ambayo iliambatana na huzuni pamoja na kumbukumbu zilizotawala vichwa vya watu wengi. Ilikuwa ni tukio la kihistoria ambapo watu walikusanyika sio tu kwa ajili ya kuomboleza, bali kukumbuka maisha ya mtu ambaye alileta mabadiliko.
Wanasayansi, wananchi, wana diplomasia, wanafunzi na wataalamu wa masuala ya mazingira walishirikiana na watoto waliokua wakilisikia tu jina la Jane Goodall wakati wote wa makuzi yao. Wengine walimuona alipokuwa akizunguka mashuleni akihamasisha uanzishaji wa vilabu vya mazingira ili kueneza dhana ya elimu ya mazingira (Roots and Shoots).
Watu hawa walikusanyika kumuenzi mwanamke shujaa ambaye maisha yake yaliondoa mpaka kati ya sayansi na utu, binadamu na asili, na kati ya Tanzania na dunia. Huu haukuwa mkusanyiko tu, bali ulikuwa uthibitisho kwamba baadhi ya kumbukumbu zinaendelea kuishi hata pale uhai unapokoma.
Mama Getruda Mongella (katikati), mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall- Tanzania (katikati) akiwa pamoja na baadhi ya ndugu na marafiki zake wakati wa hafla ya kumbukizi ya Dk Jane Goodall.
Tanzania, mahali alipoanzia safari yake
Akifungua hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jane Goodall Tanzania, Frederick Kimaro, alisema Dk Jane Goodall aliibadili dunia si kwa kuishinda asili, bali kwa kuisikiliza.
Alisema kazi yake ilionyesha kuwa sayansi si kitendo cha kawaida, bali ni jitihada ya kibinadamu inayohitaji huruma, subira na kujali. Ingawa ushawishi wake ulienea duniani kote, Tanzania ilibaki na nafasi ya kipekee moyoni mwake.
Gombe haikuwa tu kituo cha utafiti. Ilikuwa sehemu muhimu ya maisha yake. Hapo ndipo alipojifunza kuielewa asili na kujitambua yeye mwenyewe. Akizungumza katika ukumbi huo uliokuwa umejaa watu wa rika na taaluma mbalimbali, Kimaro alisema kuwa, urithi wa Dk Jane Goodall hauonekani tu katika juhudi kubwa alizofanya kwenye uhifadhi wa misitu na mazingira, bali pia kwa watu aliowatia moyo, ujasiri na kuwapa matumaini mapya kupitia kazi zake.
Kutoka mtafiti hadi mwanaharakati
Akizungumzia hadithi ya Dk Goodall kutoka mtafiti hadi mwanaharakati wa mazingira, Emmanuel Mtiti, Mkurugenzi wa Programu wa Taasisi ya Jane Goodall Tanzania, aliyewakilisha pia sauti za jamii ambazo hazikuweza kuhudhuria hafla hiyo alisema kuwa, Dk Goodall alikuja Tanzania kama mtafiti.
Lakini siku moja, baada ya kushiriki warsha kuhusu changamoto za mazingira, alizunguka katika hifadhi ya Gombe kwa ndege na kuona kwa macho yake kasi ya uharibifu wa misitu iliyokuwa imezunguka hifadhi hiyo. Alihuzunika sana alipoona msitu alioufanyia utafiti kwa miongo kadhaa ulikuwa umesongwa na uharibifu.
Jambo hilo lilibadilisha kabisa mawazo yake, ambapo alitambua kuwa uhifadhi hauwezi kufanikiwa kwa kuzingatia wanyamapori pekee huku ukiwaacha pembeni watu wanaoishi karibu nao. Kutokana hilo, alianzisha mpango wa TACARE (Take Care) ambao ni mradi unaohamasisha juhudi za kulinda uhifadhi kupitia jamii ukisisitiza uwajibikaji, utu na umiliki wa pamoja.
Mtiti alieleza kwa mifano hai mafanikio ya falsafa hiyo kwa kueleza kuwa, katika kijiji cha Kalinzi, wakulima waliongeza uzalishaji wa kahawa na kipato chao kupitia mradi huo.
Katika kijiji cha Kazuramimba, wananchi walifanikiwa kupata hati miliki za ardhi ambazo zilirejesha usalama na heshima huku katika kijiji cha Mwamgongo mikopo midogo iliwezesha familia kuwasomesha watoto, katika kijiji cha Kidahwe huduma za uzazi wa mpango ziliimarisha afya na ustawi wa kaya, kijiji cha Ilagala, jamii zilishirikiana na wanasayansi kuandaa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nk.
“Hizi si takwimu tu za kwenye makaratasi, bali ni kwenye maisha ya watu.” alisema Mtiti na kusisitiza kuwa, maono ya Dk Goodall hayakuwa katika misitu pekee, bali kwa watu kujiona kuwa sehemu ya asili. Alijua kwamba siku moja hangekuwapo tena. Lakini lililokuwa muhimu kwake ni kwamba angeacha nyuma watu wenye uwezo wa kuendeleza kazi hiyo,”
Dk Nazar na ushuhuda wa kufunguliwa milango na Dk Goodall
Mmoja wa waanzilishi wa mpango wa Roots & Shoots, Dk Nazar Nicholas anasema mchango wa Dk Goodall katika maisha yake ulikuwa wa kipekee na hawezi kuusahau. Alisema zawadi kubwa aliyompa ni fursa ya kumfungulia milango ambayo hakujua ipo. Anasema kupitia Dk Goodall, alikutana na watu kutoka nchi mbalimbali na kujifunza kuwa uhifadhi ni jukumu la pamoja la binadamu wote.
“Wakati fulani alimuuliza angejisikiaje kukutana na watu kutoka nchi nyingi tofauti. Jibu lake, alikumbuka huku akitabasamu, lilidhihirisha lilikuwa katika kile alichomfundisha siku zote; alisema kwamba ingekuwa kama kukutana na familia.”
Katika hafla hiyo, ulizinduliwa rasmi Mtandao wa Wahitimu wa Roots & Shoots, jukwaa la kuendeleza uongozi wa vijana na kudumisha mshikamano ulioasisiwa na maono ya Dk Goodall. Pia ilipendekezwa kuanzishwa kwa mdahalo wa kila mwaka wa “Urithi wa Jane” ili kuendeleza mijadala kuhusu maadili aliyoyaishi.
Dk Goodall alivyojitoa na kufanya kazi bila kupumzika
Dk Anthony Collins, Mkurugenzi wa Utafiti wa Nyani aina ya Baboon katika Kituo cha Utafiti cha Gombe, alisema maisha ya Dk Goodall hayakuongozwa na wajibu aliokuwa nao bali dhamira yake. Nusu ya kwanza ya taaluma yake ilijikita katika utafiti wa sokwe, nusu ya pili ikamfanya kuwa sauti ya kimataifa ya uhifadhi na matumaini. Katika vipindi vyote hivyo, alifanya kazi kwa bidii na utulivu.
Hata alivyokuja Gombe ambapo palikuwa mahali pa utulivu, hakutaka kupumzika. Alirekodi ujumbe, alikamilisha kazi na alishiriki hadithi za matumaini. Siku ya mwisho ya maisha yake alifanya kazi kama kawaida. Usiku huo, alipumzika milele. Kwa waliompenda, ilikuwa pigo kubwa. Lakini pia ilikuwa taswira ya maisha aliyochagua, maisha ya kujitoa kikamilifu kwa ajili ya dunia.
Washiriki wakifuatilia hafla ya kumbukizi ya Dk Jane Goodall.
Sauti ya dunia iliyoacha funzo kwa wote
Urithi aliotuachia Dk Goodall unagusa dunia nzima ambapo kupitia yeye ulimwengu umepata funzo kubwa kuhusu asili. Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Suzana Ngogi Namondo, alisema Dk Goodall alikuwa miongoni mwa watu wachache waliobadili namna binadamu wanavyojitambua ambapo aliikumbusha dunia kuwa binadamu ni sehemu ya asili.
Bi. Namondo alisema kinachofanya urithi wa Dk Goodall uendelee kuishi ni kwamba kazi zake hazikuishia tu kwenye utafiti, bali ziligusa maisha ya jamii na kubadili elimu kuwa vitendo na wasiwasi kuwa uwajibikaji. “Dk Goodall ametuachia funzo kubwa ambalo litaendelea kuishi kwamba, uhifadhi hauwezi kufanikiwa bila jamii na maendeleo hayawezi kupatikana bila kuilinda asili.”
Alisema kuwa falsafa hiyo inaendelea kuishi katika shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kuanzia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa baionuwai mpaka uwezeshaji wa vijana na shughuli endelevu za kujiingizia kipato.
“Katika nyakati ambazo uharibifu wa mazingira umekithiri, ujumbe wa Dk Goodall kuwa ‘kila mtu ana nafasi na matumaini ni maamuzi tunayofanya kupitia vitendo’ unaendelea kuishi,” alisema Bi. Namondo.
Hekima ya bibi
Tukio lililotia huzuni kuteka hisia za watu wengi waliohudhuria hafla hiyo likafika ambapo mmoja wa wajukuu wa Dk Goodall, Merlin Van Lawick ambaye pia ni Mtaalamu wa Mawasiliano ya Sayansi ya Uhifadhi katika Taasisi ya Jane Goodall aliposimama na kuzungumza kwa niaba ya familia.
Merlin alitoa salamu za rambirambi zilizogusa wengi akimuelezea Dk Goodall kama mwanamke aliyemfundisha mambo mengi katika ukuaji wake. Alisema alikuwa si tu nembo ya kimataifa, bali mlezi na mwongozo wa familia.
Alieleza kuhusu siku alizotumia pamoja naye Gombe, ambako alikuwa akienda peke yake hadi mahali pa siri pa utulivu. Kila mara alirejea akiwa na simulizi za wadudu, ndege na visa vidogo vilivyokuwa vikiendelea msituni. Kupitia nyakati hizo, aliifundisha familia yake kwamba maisha ni mtandao uliounganishwa, wenye utajiri wa maajabu kwa wale wanaotazama kwa makini na kusikiliza kwa subira.”
Alisema alikuwa mlezi, mwongozo na chemchemi ya hekima isiyokauka. Mara nyingi alipenda kuzungumzia “safari yake ijayo,” akimaanisha kifo. Si kwa hofu, bali kwa udadisi. Aliamini kuwa kugundua ni zawadi kubwa zaidi ya maisha.
Binti wa Tanzania
Hisia ziliongezeka zaidi pale Angel Van Lawick alipofuatia kwa kusoma Sala ya Amani ya Dunia iliyoandikwa na Dk Goodall mwenyewe na kuufanya ukumbi ubaki katika tafakuri ya kimya. Kisha Georgina Magesa akatoa salamu ya heshima kupitia shairi lililobeba maono ya Dk Goodall kwa mistari laini na yenye matumaini.
Akigusia misitu, watoto na mustakabali wa dunia, Georgina aliwakumbusha waombolezaji kuwa Dk Jane Goodall hakuwa tu mtafiti wa asili, bali aliipenda kwa dhati. Alisema matumaini hayategemei umri, bali yanahitaji ujasiri.
Shairi lake liligusa ujumbe aliouhubiri Dk Goodall maisha yake yote kwamba wanyama si vitu bali ni viumbe hai na kwamba tunachokifanya kwa dunia tunakifanya kwa kizazi kijacho. Aidha, mabadiliko ya kweli huanza katika mioyo yenye ujasiri. Kufikia mwisho wa shairi hilo, ilikuwa wazi kuwa urithi wa Dk Goodall haukubaki kwenye kumbukumbu pekee, bali umegeuka kuwa ahadi inayobebwa na kizazi kipya.
Mmoja wa wajukuu wa Dk Jane Goodall na Mtaalamu wa Mawasiliano ya Sayansi ya Uhifadhi katika Taasisi ya Jane Goodall, Merlin Van Lawick akizungumza wakati wa hafla ya kumbukizi ya Dk Jane Goodall.
Dk Jane Goodall na uhusiano wa kipekee na Tanzania
Jumuiya za kimataifa nazo hazikuwa nyuma katika kumuenzi Dk Jane Goodall. Mkurugenzi wa Maendeleo wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bi. Anna Wilson, alieleza jinsi falsafa ya Dk Jane Goodall inavyoendelea kuongoza juhudi za uhifadhi duniani kote akiwakumbusha waombolezaji kuwa kulinda wanyamapori pekee hakutoshi.
“Tumejifunza kutoka kwa Dk Jane Goodall kwamba uhifadhi lazima uende sambamba na utu wa binadamu. Tukishindwa kulinda maisha na vipato vya watu, kutengeneza fursa na kuheshimu jamii za wazawa, juhudi zetu hazitafikia mafanikio kamili.” alisema Bi. Anna.
Kauli yake ilifungua tafakuri ya kina kuhusu uhusiano wa kudumu kati ya Dk Jane Goodall na Tanzania. Akizungumza kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Tanzania, Dk Noel Lwaga, alimwelezea Dk Jane Goodall si kama mtafiti, bali kama mwanafunzi mnyenyekevu, mshirika aliyeaminika na zaidi ya yote, rafiki wa karibu wa Tanzania.
“Alikuja kusoma kuhusu Sokwe, lakini alibaki kuwaelewa watu. Kupitia kazi yake, Gombe iliwekwa kwenye ramani ya dunia ya sayansi ya uhifadhi. Leo, urithi wake unaishi katika sera zetu za Taifa, katika uhifadhi unaoongozwa na jamii na kwa vijana waliowezeshwa kupitia Roots & Shoots,” alisema Dk Lwaga.
Dk Lwaga alithibitisha dhamira ya Serikali kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Jane Goodall Tanzania kulinda misitu ya Gombe na kuimarisha juhudi za uhifadhi nchini kote. “Kwa roho na matendo, Dk Goodall alikuwa binti wa Tanzania. Mwanamke ambaye huruma yake ilivuka mipaka na maono yake yakabadilisha vizazi.”
Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Jane Goodall, James Lembeli alieleza kuwa “Dk Jane Goodall hakuwa tu mwanasayansi na mhifadhi mashuhuri, bali alikuwa mwalimu, mlezi na mtu aliyeamini kwa dhati katika nguvu ya kila mmoja wetu, hasa vijana, kuleta mabadiliko.”
Mwenyekiti huyo alizungumzia dunia inayokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bioanuwai na changamoto za kijamii zinazoongezeka na kuwakumbusha watu kuwa maisha ya Dk Jane Goodall yalikuwa wito wa kuchukua hatua.
“Alitufundisha kulinda kilicho dhaifu, kuheshimu sayansi na maarifa ya asili ya jamii na kuwatendea viumbe wote kwa huruma. Zaidi ya yote, alitufundisha tusipoteze matumaini,” alisema Lembeli.
Akitoa ujumbe wake kwa vijana waliokuwapo kwenye hafla hiyo, Lembeli alisema “Dk Jane Goodall aliwaamini ninyi. Aliamini kuwa sauti zenu, maamuzi yenu na ujasiri wenu vitajenga kesho iliyo bora. Msisahau kwamba hata hatua ndogo inaweza kuleta mabadiliko makubwa.”
Katika hitimisho lake, Lembeli aliwahimiza watu kuondoka si tu na kumbukumbu, bali pia na dhamira. “Tuishi kwa kuzingatia maadili aliyoyaishi, udadisi, unyenyekevu, ujasiri na heshima kwa asili. Tuchukue matumaini yake tuyageuze kuwa vitendo kupitia uhifadhi, uwezeshaji wa jamii na uongozi wenye maadili.” Na kwa maneno hayo, alitoa salamu za mwisho: “Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.”
Maisha ya Dk Jane Goodall yanatukumbusha kuwa, matumaini si kusubiri tu. Ni kuchukua hatua. Ni kujali. Ni kuwajibika. Nchini Tanzania, ambako safari yake ilianzia, jukumu hilo linaendelea kuishi na limekita mizizi katika misitu, limebeba sauti za jamii, na limekabidhiwa mikononi mwa kizazi kijacho.