Katika kijiji cha Ijumbi, wilayani Muleba Mkoani Kagera Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, simulizi ya Ansfrida Prospeli ni sauti ya maumivu, lakini pia ya ushindi. Kwani kwa miaka kadhaa aliishi ndani ya ndoa yenye ukatili, kipigo, kufukuzwa usiku, na hata kupelekwa hospitalini baada ya kupoteza fahamu kutokana na kipigo. Leo, anasimama imara, akisema haki inawezekana.

“Alinipiga mpaka nikazimia nikashtuka nimeshafika hospitalini akaanza kunibembeleza kwamba mke wangu nakuomba unisamehe sitorudia tena. Lakini majirani waliona na walinishauri niende nikafungue kesi ila sikuwa na hela ya kufungua kesi nifanyeje.”

Hofu, majeraha na umaskini vilimfanya ashindwe hata kulima au kuchota maji. Akiwa hana pa kwenda, alikimbilia kwa mama mmoja wa kijijini kwake aliyempa hifadhi pamoja na watoto wake watatu. Alianza upya akifanya kazi hotelini kwa shilingi elfu tatu kwa siku sawa na dola senti 15, akikusanya kidogo kidogo ili kulipa kodi ya chumba kimoja.

Wanawake wawili wanaofanya kazi katika mazingira ya ofisi nchini Tanzania, mmoja ameketi na kutazama kamera, mwingine amekazia kuandika kwenye dawati lake.

Katika kijiji cha Ijumbi, wilayani Muleba Mkoani Kagera Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, simulizi ya Ansfrida Prospeli ni sauti ya maumivu, lakini pia ya ushindi.

Lakini mabadiliko ya kweli yalianza pale alipoelekezwa kwa mtandao wa wanawake wanasheria wa kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake, unaojulikana kama WILAC.

“Nikamuuliza WLAC ni nini? Akaniambia kule ni kupata ushauri. Basi nami nikamwambia huyo nipeleke. Mwanasheria akanipa utaratibu. Kiwango cha msaada kwa mwanasheria nilichokipata ni kikubwa sana. Kimenisaidia sana kunielekeza jinsi ya kupambania haki zangu.”

Kupitia msaada wa kisheria wa WLAC, Ansfrida alikata rufaa ya kesi yake ya matunzo toka kwa mumewe aliyemfukuza kwenye Mahakama ya Wilaya baada ya kutoridhika na maamuzi ya awali ya Mahakama ya Mwanzo. Hapo ndipo mizani ya haki ilipoanza kusogea upande wake, na kuanza kujijenga upya kiuchumi.

“Nilipata kiwanja, nikaanza kufanya shughuli zangu, nikajiunga na vikundi vya wakina mama, nikainua msingi kwenye kiwanja changu nikajenga nyumba yangu ya vyumba vitatu. Maisha yangu yako vizuri, watoto wangu wanasoma. Kwa kweli sina shida yoyote.”

Leo, nyumba yake ya vyumba vitatu imesimama pale ambapo zamani palikuwa na hofu. Watoto wake wanasoma. Biashara inaendelea. Na Ansfrida ana ujumbe mmoja, msaada wa kisheria unaweza kubadilisha maisha. Kutoka ukatili hadi haki, hii ni sauti ya mwanamke aliyesimama na kushinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *