Marekani. Uhusiano wa miaka mingi wa wanamuziki kutoka Marekani, Nelly, 51, na Ashanti, 45, umekuwa na simulizi nyingi tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, lakini unatoa funzo moja kubwa la maisha hasa kwa wapendanao.

Wawili hao walioshirikiana katika wimbo Body on Me (2008), wanatufundisha kwamba katika safari ya kutafuta furaha katika uhusiano au ndoa, kila mmoja ana fungu lake alilopangiwa. Unaweza kuzunguka kote, lakini mwisho wa siku utakwenda mahali ulipopaswa kuwepo.

Hapa tunamzungumzia Nelly aliyevuma na wimbo wake Dilemma (2002) akimshirikisha Kelly Rowland wa Destiny’s Child. Pia tunamzungumzia Ashanti aliyefunika katika kolabo zake na Fat Joe kupitia wimbo What’s Luv? (2002), na Ja Rule kupitia Always on Time (2001).

Mastaa hawa walianzisha uhusiano baada ya kukutana katika 45th Annual Grammy Awards mwaka 2003. Penzi lao lilipamba moto kwa miaka 10 hadi walipoachana mwaka 2013, wakiwa hawana mtoto wala hawakufunga ndoa.

Katika mahojiano na kipindi cha Sway in the Morning mwaka 2014, Ashanti alikiri kuwa Nelly alikuwa mpenzi wake wa kwanza wa kweli. Baadaye aliiambia Hot 97 kwamba hakuna ugomvi kati yao licha ya kuachana.

Hata hivyo, walikuja kurudiana mwaka 2023 baada ya miaka kadhaa ya utengano, jambo lililowashangaza mashabiki wengi. Hapo ndipo tunapata darasa huru kutoka kwao. Kivipi?

Akizungumza na Rasheeda na Kirk Frost mnamo Septemba 2023, Nelly alisema imewashangaza wote wawili kuona wamerudiana tena. Hakukuwa na shinikizo lolote, lakini kuna mambo wamejifunza na hawapo tayari kurudi tena katika makosa ya zamani.

NELL 01

“Lakini wakati mwingine kuachana kunafanya kuelewana zaidi. Sasa sote tunaweza kuulinda uhusiano wetu hata kwa wakati ujao. Tunajua tulikosea, ila tutasimamia hilo. Unajua ninamaanisha nini? Sisi sote ni wahanga wa jambo hilo,” alisema Nelly.

Ikumbukwe tetesi za wawili hao kurudiana zilikuwepo miezi kadhaa nyuma. Mei mwaka huo, Ashanti alimvuta Nelly jukwaani katika show yake huko Las Vegas katika Palms Casino Resort, ambapo walitumbuiza pamoja wimbo wao Body on Me (2008).

Kufikia Aprili 2024, Ashanti akiwa na umri wa miaka 43, alitangaza kuwa ana ujauzito wa mtoto wake wa kwanza. Hii ilikuwa habari kubwa na njema kwa mashabiki wengi walioguswa na tukio hilo.

NELL 02

Katika baby shower ya Ashanti iliyofanyika Julai 2024 huko Huntington, Nelly alimshukuru rafiki yake Fat Joe kwa kumsaidia kurudiana na mpenzi wake huyo, akisema alichukua jukumu la kuwaunganisha tena hadi kufanikiwa.

“Leo tumefanya baby shower. Nakupenda dada yangu (Ashanti), nina furaha sana kuwa nanyi hapa. Mungu ni mkuu,” anasema Nelly.

Hatimaye Julai 18, 2024, Ashanti alijifungua mtoto wake wa kwanza. Kwa upande wa Nelly, huyo ni mtoto wa tatu, kwani katika uhusiano mwingine tayari alikuwa na watoto wawili, Chanelle na Cornell, huku pia akiwalea watoto wawili wa dada yake Jaqueline Donahue aliyefariki mwaka 2005.

NELL 03

Ashanti alijifungua mtoto wa kiume na kumpa jina la Kareem Kenkaide, au kwa jina la utani KK. Ashanti alisema jina Kareem linaashiria ukarimu, wema, utu, uungwana, heshima na wingi wa baraka, huku Kenkaide likiwa heshima kwa baba yake mwenye jina hilo hilo.

“Baba yangu ana watoto wa kike pekee, hivyo Nelly alisema, ‘Nafikiri kumpa jina hilo ni jambo zuri sana.’ Hili lilikuwa wazo lake kabisa,” anasema Ashanti.

Katika mahojiano hayo na E! News, Ashanti pia alisema yuko tayari kuongeza mtoto mwingine na Nelly ili kuikuza familia yao.

NELL 04

“Tunaenda kuongeza mtoto mwingine. Kwa hakika nataka msichana wa kuweka mizani sawa, maana nyumbani nimezidiwa. Hivyo kupata msichana litakuwa jambo zuri,” anasema Ashanti.

Kuhusu hatua ya kuwa mama kwa ujumla, Ashanti anasema: “Ninahisi misisimko wa ajabu, kufurahishwa sana na kuwa mwenye unyenyekevu. Maisha yangu yamebadilika kabisa na kuwa bora. Ninahisi kutosheka, unajua? Kikombe changu kimejaa.

“Kuwa na mtoto kunakuza upendo na utu ambao mtu anakuwa nao. Na wakati mwingine mimi humshukuru sana mama yangu, binamu, shangazi na familia kwa kuwa nami kwa kipindi chote.”

Vilevile anaeleza jinsi hali hiyo inavyomfanya atake kusaidia wengine zaidi kuliko hapo awali.

NELL 05

“Sasa hivi mimi ni kama, ni nini kingine tunaweza kufanya? Je, tunaweza kushirikiana? Kuna nguo chafu hapa, tunaweza kufua pamoja? Ndivyo tunaishi wakati huu,” anasema.

Kwa hakika, fungu la Ashanti lilikuwa limepangwa kwa Nelly. Hebu fikiria, walikuwa pamoja kwa miaka 10 na hakupata mtoto, wakaachana kwa miaka 10 na hakupata mtoto, lakini walivyorudiana tu akapata mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 43.

Ikumbukwe kuwa kwa mara ya kwanza Ashanti alifanya vizuri kimuziki baada ya kusainiwa katika lebo ya Murder Inc. Records na kutoa albamu yake ya kwanza Ashanti (2002) iliyoshinda tuzo katika Grammy Awards 2003.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *