“Tuliona kuwa wanawake wapaswa kuungana na kusema wa kauli moja,” Nelly amesema. “Tunapokuwa pamoja tunakuwa na nguvu, na ile nguvu itatuma ujumbe wa shida tunayopitia kama wanawake wa Congo kutokana na vita na changamoto zingine.”
Shirika lake linakusudia kuhakikisha sauti za wanawake zinapokelewa na kusikika, si tu ndani ya nchi bali pia kimataifa.
Kujenga uwezo na haki za kisheria kwa wanawake
Kwa mujibu wa Nelly lShirika la Sauti ya Mama Mkongomani linafanya kazi kubwa ya kuwapa wanawake elimu na ujuzi wa kisheria lakini pia utetezi mahakamani.
“Tunawafundisha wanawake mambo mbalimbali upatanishi, utetezi wa haki za binadamu, na jinsi ya kujitetea dhidi ya ubakaji,” amesema. “Baada ya hapo, tunawasaidia kwenda mbele ya mahakama, wakiwasilisha kesi zao na kupata haki zao za kisheria. Sauti ya Mama Mukongomani inakuwa kama kikundi cha kuhamasisha viongozi kuona changamoto za wanawake na kubadilisha sheria zinazohusu wanawake.”
Kwa Nelly, kazi hii inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na vita inavyoendelea Mashariki mwa Congo.
“Vita vinazuia mwanamke kuendelea kupaza sauti zao. Wakati mwingine wanawake wanapokuwa katikati ya migogoro wanapata hofu na kushindwa kujitetea,” amesema.
Hii inamaanisha kwamba juhudi zao za haki za kisheria zinakabiliwa na vizuizi vingi vya usalama na siasa za kijeshi.
Ushirikiano na mashirika ya kimataifa
Shirika la Sauti ya Mama Mukongomani linashirikiana na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani DRC ujulikanao kama MONUSCO, ili kuimarisha utetezi na kuhakikisha matukio yanayohusisha wanawake na watoto katika maeneo ya vita yanarekodiwa na kufuatiliwa.
“Tunafanya utafiti, tunaorodhesha taarifa na kuwasindikiza wanawake ili waweze kupata msaada wa kisaikolojia na kisheria, na kuhakikisha haki inatendeka baada ya vita,” anasema Nelly.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwa na jumuiya ya kimataifa inayosaidia wanawake Wakongomani kupaza sauti zao. “Tunaomba Baraza la Usalama na mashirika ya kimataifa wangalie namna ya kuhakikisha wanawake wa Congo wanaishi kwa amani, watoto wao wanaenda shule, na wanawake wanapata haki sawa na wanawake wengine duniani,” amesema.
Nelly Mbangu Lumbulumbu, mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Changamoto za kisheria na upungufu wa mamlaka
Changamoto kubwa inayokabili shirika la Nelly ni ukosefu wa fursa na udhibiti wa kisheria katika baadhi ya maeneo.
Anasema “Hata kama wamama wanapokuwa wamejifunza na kupata elimu, mara nyingine wanapopaza sauti zao, wanakabiliwa na vizuizi vya vita na kushindwa kupata usaidizi kutoka mamlaka za serikali”.
Ameongeza kuwa mara nyingine wanawake wanajikuta wakibakwa au kufanyiwa ukatili bila kuwa na njia za kupata haki, jambo linaloathiri ustawi wao na wa watoto wao.
Hata hivyoshirika lake linajitahidi kurekebisha mfumo wa kisheria kwa kuwasilisha kesi mahakamani za kimataifa na kushirikiana na mashirika ya kimataifa kuhakikisha wahalifu wanakabiliwa na adhabu. “Tunafanya kazi ya kuurodhesha matukio, tunakagua matukio na kutuma ripoti kwa Mahakama ya Kimataifa ili kuhakikisha kuwa wale wanaokiuka haki za wanawake wanashughulikiwa,” amesema Nelly.
Ujumbe wa matumaini kwa wanawake
Mwisho, Nelly ametoa ujumbe wa kutia moyo kwa wanawake wote kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
“Neno langu kwa wanawake ni kuwa hawako peke yao. Tuko pamoja nao na tutaendelea kupaza sauti kwa ajili yao. Tunawatakia amani na tunajua amani itafika kwa wakati wake,” amesema.
Kwa kupitia Sauti ya Mama Mukongomani, wanawake wa Congo wanaendelea kujenga nguvu, kushirikiana na jumuiya ya kimataifa, na kupaza sauti zao dhidi ya ubaguzi, ubakaji na ukosefu wa haki.
Kazi ya Nelly na Shirika lake inatoa mfano wa jinsi wanawake wanavyoweza kushirikiana, hata katika maeneo yenye migogoro ya muda mrefu, kupaza sauti zao hadi duniani kote.