Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis inabainisha kuwa mashambulizi ya walowezi yamekuwa yakifanyika kwa uratibu wa kimkakati na mara nyingi bila kupingwa, huku mamlaka za Israel zikidaiwa kuwa na mchango wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja katika kuyawezesha.
“Ghasia za walowezi zimeendelea kwa namna iliyoratibiwa kimkakati, hali inayofanya iwe vigumu kutofautisha kati ya ghasia za serikali na za walowezi,” imeeleza ripoti hiyo.
Aidha, ripoti hiyo inaonya kuwa hali ya kutowajibishwa kwa wahusika imekuwa ikichochea na kuruhusu kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya Wapalestina.
“Katika kipindi cha miezi 12 hadi Oktoba 31, 2025, matukio 1,732 ya ghasia za walowezi yaliripotiwa ikiwa ni ongezeko kutoka matukio 1,400 katika kipindi kilichotangulia yakihusisha majeraha, uharibifu wa mali, vitisho na uharibifu wa makazi pamoja na mashamba”.
Watoto katika kambi ya wakimbizi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi wakiangalia malazi yaliyoharibiwa kufuatia mashambulizi ya hivi majuzi za kijeshi.
Mashambulizi ya kila uchao
Ripoti hiyo pia inaeleza kuongezeka kwa kile kinachoitwa “walowezi wanajeshi,” ambapo baadhi ya walowezi wamepewa silaha na mafunzo.
Katika msimu wa mavuno ya mizeituni mwaka 2025, mashambulizi 42 yaliripotiwa ndani ya mwezi mmoja, yakisababisha majeruhi 131 wakiwemo wanawake 14 na mtoto mmoja idadi kubwa zaidi kwa mwezi mmoja tangu mwaka 2006.
Mashambulizi ya kila siku kutoka kwa walowezi wenye silaha, wanajeshi, na walowezi wenye mafunzo ya kijeshi yamefanya msimu huo kuwa mbaya zaidi katika miongo kadhaa.
Wanawake na watoto waathirika wakuu
Katika baadhi ya matukio, ukatili wa kijinsia umetajwa kuwa sababu ya mwisho ya familia kuhama.
Mashambulizi mengine yamesababisha familia kutengana, ambapo wanawake na watoto hulazimika kuondoka huku wanaume wakibaki kulinda ardhi na mali.
Hofu ya usafishaji wa kikabila
Ripoti hiyo inaeleza kuwa uhamishaji wa watu katika Ukingo wa Magharibi, sambamba na ule unaoendelea katika Ukanda wa Gaza, unaashiria sera pana ya kulazimisha uhamishwaji wa Wapalestina.
“Hali hii inaashiria uwezekano wa sera ya uhamishaji wa kudumu, jambo linalozua hofu ya usafishaji wa kikabila,” imeonya ripoti hiyo.
Jamii za Bedouin kaskazini mashariki mwa Yerusalem Mashariki zimetajwa kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kufukuzwa kutokana na mipango ya upanuzi wa makazi.
Masuala ya Kisheria na Uhalifu wa Vita
Ripoti hiyo inaonya kuwa uhamishaji wa watu waliolindwa ni ukiukwaji wa mkataba wa Nne wa Geneva na unaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Pia inaeleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha uwajibikaji wa jinai binafsi, na katika baadhi ya mazingira vinaweza kufikia kiwango cha uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Zaidi ya hayo, ripoti hiyo inahitimisha kuwa sera za Israel zimeunda mfumo wa taasisi wa ubaguzi, ukandamizaji na vurugu za kimfumo dhidi ya Wapalestina, kinyume na sheria za kimataifa zinazokataza ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa kimfumo .
Msichana mdogo akikimbia kwenye vifusi vya majengo yaliyoharibiwa baada ya uvamizi wa jeshi la Israeli katika kambi ya wakimbizi ya Nur Shams iliyoko Ukingo wa Magharibi mnamo Agosti 2024.
Wito wa kusitishwa mara moja kwa makazi ya Walowezi
Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ameitaka Israel:
- Kusitisha mara moja upanuzi wa makazi ya walowezi
- Kubomoa makazi yaliyojengwa kinyume cha sheria
- Kuondoa Walowezi katika maeneo yaliyokaliwa
- Kumaliza uvamizi wa ardhi ya Wapalestina
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa pia imesisitiza kuwa Israel inapaswa kuruhusu kurejea kwa Wapalestina waliokimbia makazi yao na kusitisha unyakuzi wa ardhi, ubomoaji wa nyumba na uhamishaji wa kulazimishwa.
Rekodi ya upanuzi wa makazi
Ripoti inaonyesha kuwa mamlaka za Israel zimeidhinisha au kuendeleza ujenzi wa:
- Nyumba 36,973 katika makazi ya walowezi Yerusalem Mashariki
- Takriban nyumba 27,200 katika maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi
Aidha, vituo vipya 84 vya walowezi vimeanzishwa idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa bila hatua za haraka za kisiasa na kisheria, hali ya uhamishaji wa shuruti na ukiukwaji wa haki za binadamu itaendelea kuongezeka katika maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kimabavu na Israel.