“Mlipuko unaoripotiwa kutokea usiku kucha katika Kituo hicho cha Omid mjini Kabul, kinachosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, umeua zaidi ya watu 400 na kujeruhi wengine 250 waliokuwa wakipatiwa matibabu ya matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Tangu mapigano kati ya Pakistan na Afghanistan yashike kasi kuanzia mwishoni mwa mwezi uliopita, mamia kadhaa ya raia wa Afghanistan – wakiwemo watoto 104 na wanawake 59 wameuawa au kujeruhiwa.

Makumi ya maelfu ya watu, hasa kusini na kusini-mashariki mwa nchi, wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano.

Pakistani nako hali si hali

Nchini Pakistan, wengi pia wamelazimika kukimbia makazi yao, na kusababisha shule kufungwa.

“WHO inafanya kazi kuthibitisha tukio la jana usiku,” amesema Tedros, lakini kuongezeka kwa mapigano kunaweka mzigo zaidi kwa mifumo ya afya na kuongeza hatari kwa afya na ustawi wa makundi yaliyo hatarini.

Kuongezeka kwa mapigano kati ya Afghanistani na Pakistani kumesababisha “takribani vituo sita vya afya kuripotiwa kuharibiwa nchini Afghanistan tangu mwishoni mwa Februari,” amesema.

Tedros amesema “Ninatoa wito kwa pande zote kupunguza mvutano na kuweka kipaumbele kwa amani na afya. Amani ndiyo dawa bora zaidi.”

Eneo la ‘uharibifu mkubwa’

Thameen Al-Kheetan, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, amesema mashahidi walieleza kuwa eneo hilo lilikuwa “mahali penye uharibifu mkubwa kabisa,” huku mamia ya watu wakitafuta ndugu zao.

Wito wa fidia

Msemaji huyo wa OHCHR amesema tukio hilo lazima lichunguzwe haraka, kwa uhuru na kwa uwazi, huku wahusika wakiadhibiwa kulingana na viwango vya kisheria na haki za kimataifa.

Bwana Al-Kheetan  amesisitiza kuwa “Matokeo hayo lazima yawekwe wazi kwa umma,” amesema. “Waathiriwa na familia zao wanastahili fidia.”

Kupitia msemaji huyo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk anasisitiza tena wito wake kwa pande zote kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ulinzi wa raia, kulingana na sheria za kimataifa. Amesisitiza haja ya kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuruhusu msaada wa kibinadamu kufika kwa wale wanaouhitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *