Uchambuzi mpya wa WFP uliochapishwa leo mjini Roma Italia unaonesha kuwa karibu watu milioni 45 zaidi wanaweza kuingia katika hali ya njaa kali ya viwango vya faraja la 3 la thatmini ya uhakika wa chakula IPC au zaidi, mwaka huu iwapo mgogoro utaendelea na bei ya mafuta kubaki juu ya dola 100 kwa pipa.
WFP imesema idadi hii itaongezeka juu ya watu milioni 318 ambao tayari wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula duniani.
Takwimu hizi zinafanana na hali iliyoshuhudiwa wakati wa vita ya Ukraine, ambapo njaa ilifikia watu milioni 349 duniani.
“Iwapo mgogoro huu utaendelea, utasababisha mtikisiko mkubwa duniani, na familia ambazo tayari haziwezi kumudu mlo wao ujao ndizo zitakazoathirika zaidi,” amesema Carl Skau, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP.
“Bila ufadhili wa kutosha wa misaada ya kibinadamu, hali hii inaweza kuwa janga kwa mamilioni ya watu ambao tayari wako ukingoni.”
Asilimia 70 ya watoto nchini Ukraine wanakosa huduma za kimsingi.
Mshtuko wa nishati unavyochochea mgogoro wa chakula
Tofauti na mgogoro wa Ukraine uliovuruga usambazaji wa nafaka, mgogoro wa sasa unahusisha kitovu muhimu cha nishati duniani.
Hata hivyo, WFP inaonya kuwa athari zake zinaweza kuwa kubwa sana kutokana na uhusiano wa karibu kati ya masoko ya nishati na chakula.
Usumbufu wa usafirishaji katika maeneo muhimu kama Mlango wa Hormuz na Bahari ya Shamu tayari unaongeza gharama za mafuta, mbolea na usafiri hali inayochangia kupanda kwa bei ya chakula duniani.
“Mgogoro huu unasambaa mbali na kuathiri maeneo mengi na watu walio hatarini zaidi duniani ndio watakaokumbwa zaidi na athari zake,” imeeleza WFP.
Chakula kinasambazwa kwa familia za wakimbizi katika shule ya Tariq Jdide, Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
Afrika na Asia zakabiliwa na ongezeko kubwa la njaa
Nchi zinazotegemea uagizaji wa chakula na mafuta, hasa katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia, zinatarajiwa kuathirika zaidi.
Makadirio ya WFP yanaonesha:
- Ongezeko la asilimia 24 ya ukosefu wa chakula Asia
- Ongezeko la asilimia 21 Afrika Magharibi na Kati
- Ongezeko la asilimia 17 Afrika Mashariki na Kusini
Katika nchi zilizo katika mazingira magumu, athari tayari zinaonekana. Nchini Sudan, ambayo huagiza takriban asilimia 80 ya ngano, kupanda kwa bei kunatarajiwa kusukuma familia zaidi kwenye njaa.
Wakati huo huo, Somalia inayokabiliwa na ukame mkali imeshuhudia bei ya bidhaa muhimu ikipanda kwa angalau asilimia 20 tangu mgogoro uanze.
Upungufu wa fedha watishia kuongeza janga
Mgogoro huu unakuja wakati WFP ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha, hali iliyolazimisha kupunguza baadhi ya programu zake duniani. Hii ina maana kuwa watu wengi wanaohitaji msaada wanaachwa bila kusaidiwa.
“Ongezeko la ukosefu wa chakula bila kuongezeka kwa rasilimali linaweza kusababisha janga kubwa katika baadhi ya nchi zilizo hatarini zaidi duniani,” imeonya WFP.
Jengo moja huko Beirut, Lebanon, liko katika magofu baada ya kugongwa na makombora.
Mfumo wa chakula duniani uko hatarini
Wachambuzi wa WFP wanasema makadirio haya yanatokana na kupanda kwa bei ya mafuta na athari zake katika mifumo ya chakula duniani. Kadri gharama zinavyoongezeka, mamilioni ya familia zinazoweza kumudu chakula leo zinaweza kushindwa kabisa kumudu lishe ya msingi.
Kwa kuwa njaa duniani tayari iko katika viwango vya juu, shirika hilo linaonya kuwa bila hatua za haraka za kupunguza mgogoro na kuongeza ufadhili wa kibinadamu, dunia inaweza kushuhudia tena au hata zaidi mgogoro mkubwa wa njaa kama ule wa mwaka 2022.