Yanga imeshindwa kuongeza pengo la pointi baina yake na Azam iliyo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kufikia 11 baada ya leo Jumatano, Machi 18, 2026 kulazimishwa sare tasa na TRA United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Sare hiyo ya leo imefanya Yanga iendelee kuongoza msimamo wa ligi ikifikisha pointi 37 huku Azam ikiwa na pointi 28.

Licha ya TRA United kucheza pungufu kwa dakika 16 baada ya Mzamiru Yassin kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 76, Yanga imeshindwa kutumia vyema fursa hiyo kupata ushindi ambao ungeifanya ifikishe pointi 39 kileleni mwa msimamo wa ligi.

Mzamiru ameonyeshwa kadi hiyo nyekundu na Refa Nassoro Mwinchui kutoka Tanga baada ya kuonyeshwa kadi ya njano ya pili kwa kumchezea faulo, Mohamed Hussein huku ya kwanza akionyeshwa kwa kumfanyia faulo Sheikhan Ibrahim.

Ni mchezo ambao haukuwa na nafasi nyingi za mabao zilizotengenezwa na timu zote mbili huku chache zilizopatikana zikishindwa kutumiwa vizuri.

Miongoni mwa nafasi nzuri ambayo Yanga wamepata ni ile ya dakika ya 14 ambapo Sheikhan alipiga shuti kali la mguu wa kushoto lililotoka nje kidogo ya lango la TRA United baada ya kiungo huyo kupokea pasi ya Mohamed Damaro.

Katika dakika za lala salama za mchezo, TRA United nao walipata nafasi nzuri ya kufunga baada ya Joseph Akandwanao kupokea pasi  nzuri ya Valentin Nouma lakini akiwa anatamazana na kipa Djigui Diarra, alipiga shuti la wastani ambalo kipa huyo aliliokoa.

Hadi Refa Mwinchui anapuliza filimbi ya kumaliza mchezo, timu hizo zilishindwa kufungana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *