
MASHINDANO ya Masauni & Seif Cup, yamemalizika kwa timu ya Kwahani kuibuka kidedea na kuondoka na Sh5 milioni baada ya ushindi uliotokana na penalti.
Fainali ya michuano hiyo ilichezwa Machi 18, 2026 kwenye Uwanja wa Maisara uliopo Mjini Unguja na Kwahani iliifunga Mwembeladu kwa penalti 1-0 iliyofungwa na Mundhir Omar Hassan, huku wachezaji wengine wote wakikosa katika changamoto hiyo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Wakati Kwahani ikiondoka na Sh5 milioni, Mwembeladu alikabidhiwa Sh2 milioni kwa kushika nafasi ya pili.
Katika dakika tisini, Abdalla Himidi alianza kuifungia Kwahani, kisha Tariq Mzee akasawazisha na kufanya matokeo kuwa 1-1, ndipo mikwaju ya penalti ikaamua mshindi.
Timu hizo zilicheza fainali baada ya Mwembeladu kuitoa Kisiwandui kwa penalti 3-1 hatua ya nusu fainali ambapo dakika 90 hazikufungana, huku Kwahani ikiichapa Kwalinatu mabao 2-1.
Akizungumza katika fainali hiyo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma alisema mashindano hayo ni chachu ya kuibua vipaji kwa vijana na kupata ajira kupitia mpira wa miguu.
“Natoa wito kwa viongozi wengine wa majimbo kutengeneza timu za mpira ili kutoa timu itakayoliwakilisha jimbo hilo na kushindanisha baina ya Mjini na vijijini,” alisema Pembe.
Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Hamad Masauni alisema hiyo ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo kushirikisha timu za majimbo mengine ili kutoa hamasa.
Alisema, baada ya timu zilizoshiriki kufanya vizuri, watakaa pamoja baina ya wabunge na Wawakilishi wa Mkoa wa Mjini kwa lengo la kuandaa mashindano ya Mkoa na si jimbo pekee.
Aliongeza, endapo watafanya hivyo mashindano hayo yatakuwa makubwa zaidi kwani wachezaji wanaocheza ligi kubwa hapa nchini wameanza kwa kucheza ligi za aina hiyo.
Mashindano hayo yameshirikisha timu 20 ambazo Kundemba, Vuga, KISC FC, Ujamaa, Urusi, Misyuu, Aston Villa, Malindi, Mlandege, Mladu, Villa Coast, Muungano, Medson, Black Fighter, Kwahani, Kilimani, Mafunzo, Real Zanzibar, Rio na Galilaya.