
Mtwara. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekabidhiwa rasmi miundombinu ya majengo ya Kampasi ya Mtwara ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kutoka kwa mkandarasi aliyetekeleza ukarabati huo.
Ukarabati huo ulihusisha majengo ya vyuo vya ualimu, ufundi na maendeleo ya jamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuyaendeleza na kuyapandisha hadhi hadi kufikia kiwango cha chuo kikuu.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha elimu ya ufundi na kuongeza uzalishaji wa walimu wa amali, ili kuzalisha wataalamu watakaofundisha katika shule na vyuo vya ufundi nchini, hususan katika stadi za maisha.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika leo Machi 19, 2026, Makamu Mkuu wa MUST, Profesa Aloys Mvuma, amesema mradi huo umetokana na mapitio ya sera ya elimu na mafunzo ya ufundi ya mwaka 2014 (toleo la 2023), ambapo serikali imeweka mkazo katika kuwajengea wanafunzi ujuzi na maarifa ya vitendo.
Profesa Mvuma amesema serikali imetoa shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ukarabati na kuinua hadhi ya chuo hicho, ambacho tayari kimeanza kupokea wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2025/2026, huku masomo yakianza rasmi Novemba 2025.
Ameongeza kuwa kampasi hiyo inatarajiwa kupokea wanafunzi kati ya 800 hadi 1,000 kuanzia mwaka wa masomo 2026/2027, huku mipango ikiendelea ya kupanua wigo wa taaluma ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Zoezi la ukarabati ni endelevu, na katika miaka ijayo tuna mpango wa kujenga majengo mapya ili kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi wengi zaidi,” amesema Profesa Mvuma.
Kwa upande wake, mkandarasi wa mradi huo, Bosco Kavishe wa kampuni ya Kawishe Contractor, amesema kabla ya ukarabati huo, miundombinu ya chuo hicho ilikuwa chakavu na isiyokidhi hadhi ya chuo kikuu.
Ameeleza kuwa maboresho yaliyofanyika yameendana na hadhi ya mazingira yanayokidhi viwango vya elimu ya juu.
“Tumekarabati majengo, vyoo, madarasa na ofisi kwa viwango vya kisasa. Pia tumeboresha miundombinu ya barabara za ndani ya chuo ili ziwe rafiki hata kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,” amesema Kavishe.
Aidha Mkandarasi huyo ameishukuru Serikali kwa kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi ya hiyo ya maendeleo.
Kukamilika kwa ukarabati na kukabidhiwa kwa miundombinu hiyo kunatarajiwa kuchochea upatikanaji wa elimu ya juu katika ukanda wa mikoa ya kusini, na kuendeleza elimu ya ufundi na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa.