
Dkt. Robert Waldinger, mtaalamu wa magonjwa ya akili na profesa katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani anaongoza moja ya tafiti ndefu zaidi katika historia zinazolenga ustawi wa binadamu. Katika mahojiano na UN News kuadhimisha siku hiyo, ameeleza kuwa furaha ni jambo changamano zaidi na wakati huo huo linaweza kufikiwa zaidi kuliko watu wengi wanavyodhani.
Aina mbili za furaha
“Utafiti unaonesha kwamba kuna aina mbili kuu za furaha,” anasema Dkt. Waldinger. Moja ni ustawi wa kihisia (hedonic) hisia ya raha na kufurahia wakati uliopo.
“Wakati wewe na mimi tunazungumza vizuri, nina furaha kabisa,” ameeleza, akibainisha kuwa hisia kama hizi zinaweza kubadilika siku nzima.
Aina ya pili furaha ya kina (eudaimonic) inaenda mbali zaidi. Ni hali ya kudumu ya kuhisi kuwa maisha yana maana na ni mazuri kimsingi, hata kama baadhi ya siku ni ngumu. Kulingana na mtafiti huyo, watu wengi hutafuta yote mawili: furaha ya papo hapo na utimilifu wa muda mrefu.
Hata hivyo, jamii mara nyingi huelewa vibaya chanzo cha ustawi wa kweli.
Dhana potofu ya mafanikio
Watu wengi bado wanaamini kuwa furaha huja na mafanikio, utajiri au umaarufu. Lakini, kama Dkt. Waldinger anavyosisitiza, ushahidi wa kisayansi unaonesha hadithi tofauti.
“Naweza kuwa na mafanikio, naweza kuwa tajiri, na naweza kuwa na furaha hiyo ni kweli. Lakini vitu hivyo havitufanyi kuwa na furaha,” amesema. “Watu wengi wanaoshinda tuzo kubwa, hata Tuzo ya Nobel, huingia katika hali ya huzuni baada ya muda kwa sababu wanagundua: hilo halikunifanya kuwa na furaha. Hilo halikuwa lengo pekee ambalo lingeifanya maisha yangu kuwa mazuri milele.”
Kwa mujibu wake, kuna dhana ya kitamaduni inayodumu: “Nikitajirika, nikawa maarufu, nikashinda tuzo nyingi, basi nitakuwa na furaha.” Kwa uhalisia, anasema, hilo mara chache hutokea.
Tabia ndogo, mabadiliko ya kudumu
Wakati huo huo, furaha si kitu tunachozaliwa nacho tu, wala si kitu kilicho nje ya uwezo wetu.
“Furaha inaweza kujifunzwa kwa sababu inaweza kujengwa,” anasema Dkt. Waldinger. “Mmoja wa walimu wangu alisema furaha ni ajali, lakini tunaweza kujifanya kuwa karibu zaidi na ajali hiyo.”
Kwa maneno mengine, ingawa hatuwezi kuhakikisha tutakuwa na furaha kila wakati, tunaweza kuunda mazingira yanayoongeza uwezekano wa kuwa na furaha.
“Hatuwezi kuhakikisha kuwa tutakuwa na furaha kila wakati, lakini tunaweza kuweka vitu katika maisha yetu vinavyoongeza nafasi ya kuwa na furaha mara nyingi zaidi,” anaeleza. “Hii ni pamoja na yale tuliyozungumzia kujihusisha zaidi na watu wengine, na kukuza mahusiano yetu.”
Mazoea kama kutafakari (meditation), kukuza shukrani, na tafakuri ya kiroho pia yanaweza kusaidia watu kuthamini maisha yao zaidi na kuimarisha uhusiano wao na wengine.
Furaha na mahusiano: mtazamo mpya kuhusu wazo la kale
Hata mawazo ya kale kuhusu furaha, anasema Dkt. Waldinger, si mara zote yanaendana na utafiti wa kisasa wa kisayansi. Akijibu mstari maarufu wa mwanzo wa riwaya ya Anna Karenina ya Leo Tolstoy – “Familia zote zenye furaha zinafanana; kila familia isiyo na furaha ina huzuni kwa njia yake” alitoa mtazamo tofauti.
“Sikubaliani. Nafikiri Tolstoy alikuwa amekosea,” anasema. “Kwa kweli, ni kinyume chake.”
Anarejelea kazi ya mwanasaikolojia wa Marekani, Dkt. John Gottman, aliyesoma mahusiano ya familia na wanandoa. “Tunachokiona ni kwamba familia na wanandoa wasio na furaha huonesha mifumo ya tabia inayojirudia. Hisia zao hasi zinatabirika, na miitikio yao inafanana. Kwa hiyo kwa mtazamo wangu, kukosa furaha mara nyingi hufuata mifumo inayofanana,” alieleza.
Dunia yenye upweke zaidi
Maisha ya kisasa yanaleta changamoto mpya. Janga la coronavirus“>COVID-19, alisema Dkt. Waldinger, halikubadilisha asili ya furaha yenyewe, lakini lilidhoofisha mahusiano ya kijamii kwa kuwatenga watu.
Mgawanyiko wa kisiasa na namna fulani ya matumizi ya mitandao ya kijamii pia umechangia kuongezeka kwa kutoaminiana. Mitandao ya kijamii inaweza kusaidia watu kubaki wameunganishwa, ambayo ni jambo chanya. Lakini kufuatilia maisha ya wengine bila kushiriki kikamilifu kunaweza kuwa na athari tofauti, kwani watu huonesha nyakati zao za furaha tu, na hivyo kuunda taswira ya maisha makamilifu.
“Ni rahisi kuanza kufikiria kwamba watu wengine wana furaha kila wakati na sisi hatuna,” alisema, akihimiza watu kutumia majukwaa ya kidijitali kwa ajili ya kuunda uhusiano wa kweli.
Ushauri kwa kizazi kipya
Vijana wa leo wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kuanzia gharama kubwa za makazi hadi soko la ajira lisilo na uhakika hali inayoongeza wasiwasi kuhusu siku zijazo. Hapa tena, jamii ina jukumu muhimu.
“Ni rahisi zaidi kuishi maisha mazuri ukiwa na watu wengine kuliko kujaribu kufanya kila kitu peke yako,” anasema Dkt. Waldinger, akibainisha kuwa mahusiano ya kijamii mara nyingi husaidia watu kupata kazi, makazi na msaada.
Nafasi ya Umoja wa Mataifa: furaha kama lengo la kimataifa
Kwa kukuza furaha kama kipimo cha maendeleo, Umoja wa Mataifa unasaidia kubadilisha namna maendeleo yanavyoeleweka. Kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu, misaada ya kibinadamu, na juhudi za kupunguza umaskini, kupanua upatikanaji wa elimu na huduma za afya, na kulinda haki za binadamu, UN inafanya kazi kuunda mazingira ambayo watu wanaweza kuhisi salama zaidi, kuwa na uhakika zaidi, na hatimaye kuwa na furaha zaidi.
Hii si kuhusu hisia za muda mfupi, bali ni kujenga jamii zenye haki zaidi ambapo kila mtu ana nafasi ya kuishi kwa heshima na ustawi.
Siku ya Kimataifa ya Furaha
Kwa Dkt. Waldinger, Siku ya Kimataifa ya Furaha si ishara tu. Inahamasisha serikali na jamii kufikiria upya maana halisi ya maendeleo.
“Inatukumbusha kwamba furaha ni jambo tunalopaswa kulifikiria na kwamba tunaweza kuboresha uwezo wetu wa kuwa na furaha,” anasema.
Katika dunia iliyojaa migogoro na mgawanyiko, ujumbe huu ni muhimu sana.
Ushauri wake kwa jamii ya kimataifa ni rahisi: sikiliza sauti zinazotukumbusha mambo tunayofanana, na jiepushe na zile zinazosambaza hofu na mgawanyiko. Kwa sababu, hatimaye, furaha ni jambo tunalojenga pamoja.