
Ndege ya kivita ya kimkakati aina ya F‑35 ya Jeshi la Marekani imelengwa kwa kombora na kuharibiwa vibaya ikiwa inaruka katika anga ya kati mwa Iran kwa lengo la kutekeleza mashambulizi.
Kwa mujibu wa Pars Today, Idara ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imetangaza katika taarifa kuwa: Alhamisi asubuhi, ndege ya kivita ya kimkakati aina ya F‑35 ya Jeshi la Marekani ililengwa na kupigwa na mfumo mpya wa kisasa wa ulinzi wa anga wa Kikosi cha Anga cha IRGC katika anga ya Iran ya kati, na kuharibiwa vibaya.
Taarifa ya IRGC inaongeza kuwa: Kufuatia kuangushwa kwa mafanikio kwa zaidi ya ndege zisizo na rubani 125 za Marekani na Israel zilizokiuka anga ya Iran, operesheni hii ya kuzuia inaonyesha mabadiliko madhubuti na yaliyolengwa katika mifumo jumuishi ya ulinzi wa taifa.
Wakati huo huo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imekiri kulengwa ndege ya kivita aina ya F‑35 ambayo ilikuwa ikitekeleza operesheni angani juu ya Iran wakati wa tukio hilo.
Mtandao wa CNN uliandika, ukinukuu vyanzo viwili vyenye taarifa za ndani, kwamba ndege ya kivita ya Marekani aina ya F‑35 ililazimika kufanya kutua kwa dharura katika kambi moja ya anga ya Marekani huko Mashariki ya Kati baada ya kulengwa na vikosi vya Iran.
Msemaji wa CENTCOM Kapteni Tim Hawkins amesema kuwa ndege hiyo ya kivita ya kizazi cha tano yenye uwezo wa kujificha kwenye rada ilikuwa ikitekeleza kile kilichoelezwa kuwa “operesheni ya kivita juu ya Iran”, hali iliyosababisha ilazimike kutua kwa dharura.
Hawkins, amedai kuwa ndege hiyo imefanikiwa kutua salama na tukio hilo linaendelea kufanyiwa uchunguzi.
Msemaji wa CENTCOM pia amedai kwamba rubani yuko salama, na uharibifu uliopata ndege hiyo ni mdogo. Hata hivyo, imeelezwa kuwa hii ndiyo mara ya kwanza kabisa katika historia kwa ndege ya F-35 kulengwa vitani jambo linaloonyesha uwezo mkubwa wa majeshi ya Iran.