
Musoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara imebaini kasoro mbalimbali katika miradi 68 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh37 bilioni, kati ya miradi 230 iliyokaguliwa yenye thamani ya zaidi ya Sh604 bilioni.
Ukaguzi huo ulifanyika kuanzia Julai 2021 hadi Septemba 2025, ukihusisha sekta za afya, maji, elimu, umeme, usafirishaji, miundombinu na utawala wa umma.
Akizungumza Machi 19, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, aMEsema ushirikiano kati ya ofisi yake na Takukuru umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo.
AMEsema Takukuru imekuwa na mchango chanya kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha na maslahi ya wananchi.
“Dosari zilizobainika ni pamoja na ucheleweshaji wa miradi, kutokuzingatiwa kwa michoro ya ujenzi, matumizi ya vifaa hafifu, wazabuni kutokuwa na sifa na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi,” aMEsema.
Katika kipindi hicho, Takukuru ilifungua kesi 99 mahakamani, ambapo kesi 81 zilishatolewa hukumu na Serikali kushinda kesi 67. Zaidi ya Sh216.2 milioni ziliokolewa kupitia juhudi hizo.
Mtambi amesema ufuatiliaji wa Takukuru umewezesha kurekebishwa kwa kasoro zilizobainika na kusaidia kuokoa fedha za umma.
Ametoa mfano wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Chifu Sarota wilayani Serengeti, ambapo Takukuru ilidhibiti wizi wa mabati yenye thamani ya zaidi ya Sh4.7 milioni uliodaiwa kufanywa na mzabuni na msimamizi wa mradi.
Aidha, amewataka wasimamizi wa miradi ya Serikali na wadau kuzingatia maadili, akisisitiza kuwa rushwa inadhoofisha ubora wa miradi na kuwanyima wananchi huduma stahiki.
Ameonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuchezea fedha za miradi ya maendeleo, akieleza kuwa vitendo hivyo ni kuhujumu juhudi za maendeleo.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wameitaka Takukuru kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu dhidi ya watumishi wanaobainika kukiuka taratibu.
Imani Joshua amesema kuna haja ya kuwafikisha mahakamani wote wanaohusika na ubadhirifu wa fedha za umma badala ya kuishia kutoa maelezo.
Naye Baraka Nyiramba amesema muda wa kuvumilia uzembe wa makusudi umefika mwisho na watumishi wanaokiuka sheria wanapaswa kuwajibishwa ipasavyo.
Amesisitiza kuwa wananchi wanaendelea kuteseka kutokana na baadhi ya watumishi kutotekeleza majukumu yao kwa uadilifu, hivyo hatua kali zinahitajika ili kurejesha nidhamu na uwajibikaji.