Akizungumza katika mahojiano na UN News  Arunabha Ghosh, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Nishati, Mazingira na Maji, amesema kuwa mgogoro huu unapaswa kueleweka kwa kuzingatia pande mbili ambazo ni mahitaji na upatikanaji wa maji.

“Karibu watu bilioni mbili wanakabiliwa na changamoto ya kupata maji safi, salama na ya gharama nafuu,” amesema, akisisitiza ukubwa wa tatizo hilo. Wakati huo huo, amesema mabadiliko ya tabianchi yanaathiri mzunguko wa maji, na kufanya upatikanaji wake kuwa mgumu zaidi kutabirika.

Kuziba ndoo inayovuja

Ghosh amesisitiza kuwa moja ya suluhisho la haraka na la vitendo ni kupunguza upotevu wa maji.

“Duniani kote, katika maeneo mengi, asilimia 30 hadi 50 ya maji yanayosafirishwa hupotea kutokana na uvujaji na hasara zisizodhibitiwa,” ameeleza. “Hii ni ndoo inayovuja ambayo lazima izibwe haraka.”

Ameongeza kuwa kuboresha miundombinu na kurekebisha mifumo ya usambazaji wa maji kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa maji mijini na vijijini.

Mvulana mchanga wa India akinywa maji kutoka kwenye kikombe cha chuma, akiwakilisha athari za mipango ya usalama wa maji.

© UNICEF/UNI953100/ . All right

Safari ya kutatua changamoto za maji na mnepo wa mabadiliko ya tabianchi Rajasthan India

Kubadili kilimo, mapinduzi ya maji yanayojali mazingira

Mbali na miundombinu, mtaalam huyo ametoa wito wa mabadiliko makubwa katika matumizi ya maji kwenye sekta ya kilimo.

Ameeleza kuwa ingawa watu wengi hufikiria mito na maziwa yanayojulikana kama “maji ya buluu” asilimia kubwa ya maji ipo kwenye unyevu wa udongo, unaoitwa “maji ya kijani.”

Amesema “Asilimia 60 ya maji yote ni maji ya kijani. Yapopo kwenye udongo wetu”.

Ili kutumia rasilimali hii vizuri, amehimiza nchi kuhamia kwenye mazao yanayotumia maji kwa ufanisi zaidi na yenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Ameyataja mazao hayo kuwa ni mtama kwa mfano, akisema una faida ya kustahimili ukame, kutumia maji kidogo, na kuwa na lishe bora.

“Unapata faida tatu mnepo dhidi ya tabianchi, matumizi bora ya maji, na lishe bora,” ameongeza, akirejelea juhudi za kimataifa kama Mwaka wa Kimataifa wa Mtama wa 2023 uliotangazwa na Umoja wa Mataifa.

Kurejeleza maji taka kwa mustakabali endelevu

Ghosh pia amesisitiza umuhimu wa kuchakata na kutumia tena maji taka, hasa katika miji inayokua kwa kasi na maeneo ya viwanda.

“Maji taka mengi hayawekwi kwenye mifumo ya usafishaji na matokeo yake, kila tone la maji linatumika mara moja tu,” alisema.

Alieleza kuwa kusafisha maji taka kunaweza kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya kilimo na viwanda, pamoja na kuzalisha nishati kupitia gesi ya methane.

“Ukisafisha maji, hupati tu maji mapya ya kutumia… pia unapata nishati,” alibainisha.

media:entermedia_image:0e2aeaa2-d03f-4aff-b76e-5b8fd5a167e9

Miundombinu mipya ya maji inabadili maisha ya wakulima Pakistan

Wito wa hatua za haraka na shirikishi

Kadri shinikizo la tabianchi linavyoongezeka na idadi ya watu kuongezeka, Ghosh alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja na za haraka duniani kote.

Kuanzia kuziba uvujaji wa maji, kubadilisha kilimo, hadi kuwekeza katika matumizi tena ya maji, alisema suluhisho zipo lakini zinahitaji dhamira ya kisiasa na mabadiliko ya mifumo.

“Swali ni jinsi gani tutapunguza idadi ya watu wanaoishi katika maeneo yenye uhaba wa maji,” amesema, akionya kuwa kushindwa kuchukua hatua sasa kunaweza kusukuma mifumo ya maji “kupita kiwango cha kurekebishika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *