Dar es Salaam. Staa wa Bongo Fleva na mwanzilishi wa Next Level Music (NLM), Rayvanny (32), pengine ameamua kufuata utararibu wake kwa jinsi anavyotambulisha wasanii wapya katika lebo hiyo ikiwa ni takribani miaka minne tangu kuanza kwa mpango huo.
Rayvanny, mshindi wa BET 2017, mnamo Machi 2021 ndipo alitangaza kuanzishwa kwa NLM baada ya kupata mafanikio makubwa chini ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz, ambayo ilimtambulisha mwaka 2016 baada ya kusota sana ndani ya Tip Top Connection.
Ni hivi karibuni Rayvanny amemtambulisha msanii mpya ndani ya NLM ambaye ni Kuss Love, kipaji kipya ndani ya Bongofleva ambacho mashabiki wengi wana kiu ya kukisikiliza baada ya ukimya mrefu wa lebo hiyo tangu waliposimama kufanya kazi na Mac Voice.
Kuss Love anatarajiwa kutambulishwa rasmi katika soko la muziki kupitia Extended Playlist (EP) yake, Gold (2026) ambayo ipo mbioni kuachiwa ikiwa na nyimbo sita huku msanii aliyeshirikishwa akiwa ni Rayvanny peke yake ambaye amesikika katika nyimbo mbili.
Rayvanny, mshindi wa tuzo tano za Entertainment Arts Excellence Awards (EAEA) 2024, ameonyesha dhamira ya kumfanya Kuss Love kuwa msanii mkubwa ndani na nje ya NLM akimtaja kama ‘Mfalme Mpya’ ndani ya Bongofleva.
Huyu anakuwa mwanamuziki wa pili kusainiwa na kutambulishwa na NLM baada ya Mac Voice ambaye sasa hayupo katika lebo hiyo kwa kile kinachodaiwa ameondoka kutokana na kutotimiziwa mahitaji yake muhimu hasa kiuchumi, ingawa lebo bado haijatoa taarifa rasmi kuhusiana na madai hayo.
Ikumbukwe Mac Voice alitambulishwa mnamo Septemba 2021, naye alikuja na EP, My Voice (2021) yenye nyimbo sita, ukiwemo ule uitwao ‘Nenda’ ambao ndio hasa uliofanya vizuri zaidi na kulibeba jina lake ukimtambulisha kama staa ajaye wa muziki wa kizazi kipya, yaani Bongofleva.
Hivyo tangu Septemba 2021 hadi Machi 2026, ni wasanii wawili pekee ndio Rayvanny kawasaini katika lebo yake ya NLM. Ni kipindi kirefu kidogo, zaidi ya miaka minne, kitu ambacho ni tofauti na lebo nyingi Bongo hasa zile zinazosimamiwa na wanamuziki wenzake.
Pengine hiyo ndio njia aliyoamua kuipitisha NLM au kuna mazingira yaliyomlazimu kufanya hivyo ikiwemo mkwamo wa kibiashara kati yake na Mac Voice tangu Mei 2024, ambapo ndipo msanii huyo alitoa wimbo wa mwisho chini ya lebo hiyo.
Kuss Love, msanii mpya wa NLM
Hata hivyo, hii ni tofauti kabisa na kule alipokulia kimuziki, yaani WCB Wasafi kwa Diamond, ambapo hawakuchukua muda mrefu hivyo katika kuwatambulisha wasanii wao wapya akiwemo Rayvanny mwenyewe.
Kwa WCB Wasafi, ndani ya miaka miwili tayari walishatambulisha wasanii wanne ambao Rayvanny kachukua miaka zaidi ya minne kufanya hivyo. Na hadi kufikia miaka minne, WCB tayari walikutana na wasanii sita, na wote walikuwa wakifanya vizuri.
Mtiririko wa WCB Wasafi kutambulisha wasanii ulikuwa kama ifuatavyo, Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lava Lava (2017) na Mbosso (2018).
Hivyo kati ya 2015 hadi 2018, kila mwaka WCB Wasafi ilimtambulisha msanii mpya, na 2016 iliwatambulisha watatu (Rayvanny, Rich Mavoko & Queen Darleen), rekodi ambayo hadi sasa haijajirudia ndani ya lebo hiyo.
Baada ya Mbosso (2018), WCB Wasafi ilipumzika kwa miaka miwili hadi walipokuja kumtambulisha Zuchu (2020) ambaye alipokelewa vizuri na mashabiki na hadi sasa akiwa ameshinda tuzo saba za muziki Tanzania (TMA) tena ndani ya misimu miwili pekee aliyowania.
Kisha wakangoja kwa miaka mitatu na ndipo wakamtambulisha D Voice (2023) ambaye hivi karibuni kufikisha streams (idadi ya nyimbo kusikilizwa) milioni 100 katika mtandao wa Boomplay Music akiwa ni msanii wa 14 Tanzania kufanya hivyo, na wa kwanza kufikia rekodi hiyo akiwa chini umri wa miaka 25.
Hii ndio njia aliyochagua Diamond kuipitisha lebo yake ya WCB Wasafi, lakini Rayvanny naye ana yake kulingana na malengo yake na mazingira yake ya kikazi, kiuchumi, kibiashara na hata kichapa (brand), yaani vile anavyotaka jambo lake litambulike mbele ya umma.
Na sasa mashabiki wanangoja kuona mpango kazi mpya wa NLM kwa Kuss Love, ni kwa namna gani watamfanya kuwa msanii mkubwa, na ushirikiano wao utakuwa na picha gani ukilinganisha na yale yalitokea kati yao na msanii wao wa zamani.