Taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA imeeleza kuwa mashambulizi ya anga, mizinga na operesheni za kijeshi zimeathiri kwa kiasi kikubwa raia na miundombinu muhimu.

Taarifa hiyo imeeleza zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine 2,584 kujeruhiwa, huku watoto wakiathirika zaidi.

Vifo

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF, Ted Chaiban, amesema ongezeko hilo la vurugu linasababisha “idadi ya watoto wanaouawa au kujeruhiwa kufikia sawa na darasa moja kila siku.”

Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya na misaada yameongezeka, ambapo wahudumu wa afya 31 wameuawa tangu tarehe 2 Machi.

Hospitali tano na vituo 49 vya afya vimefungwa kutokana na uharibifu, hali inayozuia upatikanaji wa huduma muhimu. Pia, mfanyakazi wa misaada na watoto wawili waliuawa katika shambulio moja, huku mwandishi wa habari na mke wake wakipoteza maisha katika tukio jingine.

Moshi ukiongezeka kutokana na mashambulizi ya ndege juu ya mji wa Beit Mery, Lebanoni, na Bahari ya Mediterania nyuma.

© World Vision

Mashambulio ya anga kwa Beit Mery, Lebanon.

Wakati huohuo, zaidi ya watu milioni 1.2 wamelazimika kuyahama makazi yao, huku 134,439 wakihifadhiwa katika makazi ya muda 636, hasa katika maeneo ya Beirut na Mount Lebanon. Makazi hayo yanakabiliwa na msongamano mkubwa na upungufu wa huduma muhimu kama maji, umeme na faragha.

Elimu

Sekta ya elimu pia imeathirika vibaya, ambapo shule 472 zinatumika kama makazi ya wakimbizi, na kuwanyima maelfu ya watoto haki ya elimu.

Mashirika ya kibinadamu yanatoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, yakisisitiza ulinzi wa raia, wahudumu wa afya na waandishi wa habari ili kuzuia kuongezeka kwa maafa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *