Marekani. Mwimbaji wa zamani wa kundi la Destiny’s Child, Farrah Franklin (44), amekanusha madai ya mwigizaji, Terrence Howard aliyedai kwamba waliwahi kuwa kwenye uhusiano baada ya kumkataa Beyonce Knowles.

Farrah akizungumza na People Magazine katika mahojiano ya kipekee, ameweka wazi kuwa yeye na Terrence hawakuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi bali walikuwa marafiki tu tena waliokutana mara chache.

“Naweza kuthibitisha kuwa mimi na Terrence tuliwahi kutoka mara chache kwa ajili ya matembezi ya kawaida kama marafiki, hakukuwa na uhusiano wa kimapenzi,” alisema Farrah.

Kauli hiyo imekuja baada ya Terrence kupitia Podcast ya PBD kudai aliwahi kupata nafasi ya kumtongoza Beyonce na hata kuwa naye lakini akaamua kuwa na msanii mwingine wa Destiny’s Child ambaye ni Farrah.

“Unajua, nilikuwa na nafasi ya kuwa na Beyonce kile kipindi cha mwanzoni kabisa. Tuliwahi kuzungumzia hilo, lakini mwisho wa siku nikaenda kwa msichana mwingine ndani ya Destiny’s Child. Yule msichana mwenye macho ya blue,” alieleza Terrence.

Hata hivyo, Franklin akikanusha madai hayo, anasema hakuna ukweli wa jambo hilo kwani ukaribu wao ulikuwa ni wa kikazi pekee, na sasa amejikita katika mambo yake baada ya kuachana na kundi hilo.

“Tulikwenda studio mara kadhaa, na ninaweza kusema kwamba Terrence ana kipaji kikubwa sana!. Sitajibu mambo mengine yaliyosemwa, na kama kawaida, nawatakia kila la heri wote na ninaendelea kujikita kwenye safari yangu mwenyewe,” alisema Farrah.

Ikumbukwe kundi la Destiny’s Child ambalo lilianza kuvuma miaka ya 1990 hadi mapema 2000, lilikuwa na wasanii kama Beyonce, Kelly Rowland, LeToya Luckett na LaTavia Roberson.

Baadaye ndipo Michelle Williams na Farrah wakajiunga na kundi hilo baada ya wanachama wawili kujitoa. Hata hivyo, Farrah aliondoka muda mfupi baadaye huku kundi hilo likiendelea na wanachama watatu.

Katika hatua nyingine, Farrah amesema anaendelea kufanya kazi zake mpya za muziki na filamu ambazo zipo mbioni kuwafikia mashabiki wake wote duniani.

“Nimekuwa nikifanya kazi nikiandaa muziki mpya na miradi mipya katika filamu, na kwa kweli nimefanya kazi hizo kwa kiwango cha juu zaidi,” amesema Farrah.

Na kwa upande wake, Terrence alikumbushia tukio la kucheza jukwaani na Beyonce kwenye tuzo za BET 2005, akisema anahisi Beyonce alimchagua ili kumuonyesha tu kile alichokikosa!.

Wakati huo, tayari Beyonce alikuwa kwenye uhusiano na rapa Jay Z ingawa walikuja kufunga ndoa mwaka 2008, na kwa sasa wamejaliwa kupata watoto watatu, Blue Ivy (2012) na pacha Rumi na Sir Cater (2017).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *