Dar es Salaam. Kadri tasnia ya urembo inavyozidi kukua watu wenye ugonjwa wa ngozi ufahamikao kama ‘Vitiligo’ wanazidi kung’ara na kuonyesha kuwa tofauti si kasoro bali ni zawadi toka kwa Mungu. 

Wakiwa na ujasiri na kujiamini, wanamitindo wenye vitiligo wamejikuta wakibadilisha mitazamo hasi ya jamii na kuwa hamasa ya kujikubali kwa baadhi ya watu wanaokata tamaa kutokana na mionekano yao. 

Wanamitindo hao wakubwa kama Yvesmark Chery, Winnie Harlow na wengineo  wanadhihirisha kuwa kujiamini na kujikubali ni moja ya sababu ya mafanikio kwa mtu yeyote yule.

Hili linajionesha katika tasnia ya urembo na mitindo ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la watu hao, huku wakitumia sanaa  kupaza sauti na kuelimisha jamii namna ya kujikubali. Twende pamoja

Wakiwa tayari wameuteka ulimwengu wa fasheni wanasimulia mikasa ya dhihaka na kejeli ambazo wamewahi kukutana nazo tangu enzi za utoto wao. Lakini licha ya hayo wanaonesha kuwa hazikuwarudisha nyuma.

Winnie Harlow 

Chantelle Young-Brown maarufu kama  Winnie Harlow ni moja ya wanamitindo wakubwa duniani mwenye ugonjwa wa Vitilio aliyebadili mitazamo ya jamii kuhusiana na ugonjwa huo

Winnie alizaliwa Julai 27, 1994, nchini Kanada. Akiwa na umri wa miaka minne, aligundulika kuwa na ugonjwa wa ngozi ‘Vitiligo’, hali inayosababisha kupotea kwa rangi ya ngozi katika baadhi ya maeneo ya mwili. Tangu akiwa mdogo, hali hiyo ilimtofautisha na wenzake tofauti ambayo haikukubaliwa kirahisi.

Akiwa shuleni, alikumbana na unyanyapaa mkali. Aliitwa majina kama “punda milia” na “ng’ombe”, kejeli zilizomuumiza kisaikolojia na hata kumfanya abadilishe shule mara kadhaa.

Wakati mwingine alifikia hatua ya kutaka kukata tamaa kabisa. Lakini ndani yake kulikuwa na nguvu ambayo sasa imebadilisha maisha yake.

Mungu si Athumani kupitia mitandao ya kijamii mtangazaji maarufu Tyra Banks, alikumbana na Winnie akampata nafasi ya kushiriki katika kipindi maarufu cha America’s Next Top Model mwaka 2014.

Ingawa hakushinda shindano hilo, alijijengea jina na kuonekana tofauti kabisa na washiriki wengine. Muonekano wake wa kipekee uliwavutia wabunifu na wapiga picha wa mitindo.

Baada ya kipindi hicho, milango ilianza kufunguka. Winnie alichaguliwa kuwa model wa kampeni ya chapa ya Desigual, na pia akaonekana katika matangazo ya kampuni ya Diesel.

Kuanzia hapo, alitembea kwenye majukwaa makubwa ya mitindo, akafanya kazi na wabunifu wakubwa, na kuonekana kwenye majarida maarufu duniani ikiwemo hili la Starehe. 

Amekuwa akipaza sauti kila siku kwa watu wenye vitiligo, akihamasisha kujikubali.“Nilijipenda, na hapo ndipo fursa zilipoanza kunifuata,” Moja ya maneno yake.

Yvesmark Chery

Yvesmark Chéry naye ni mwanamitindo amezaliwa Brooklyn na kukulia Philadelphia, mwanamitindo huyu mwenye asili ya Haiti na Marekani ana shahada ya Teknolojia ya Sayansi ya Habari (Information Science Technology) kutoka Pennsylvania State University kabla ya kuanza rasmi kazi yake ya uanamitindo.

Kutokana na wa muonekano wake wa kipekee ambao anauita “baraka iliyojificha” akaamua kujikita kwenye mitindo.  

Amejijengea jina katika tasnia ya mitindo na huku akitumiaka na chapa maarufu kama Calvin Klein na H&M.

Akiwa miongoni mwa wanamitindo wanaofanya kazi wakiwa na vitiligo, ameonekana katika majarida makubwa na kutembea kwenye majukwaa ya makubwa ya  Wiki za Mitindo (Fashion Week).

“Ilikuwa karibu haiwezekani kuchanganyika na wengine ukiwa na vitiligo, hasa kuishi mjini. Nilipokuwa mdogo, niliona sura tofauti za watu kila nilipotoka na wazazi wangu baadhi walionekana kuchukizwa, wengine kuchanganyikiwa. 

“Watoto walikuwa changamoto zaidi walipiga kelele wakisema, ‘Angalia! Hiyo ni nini usoni kwake?’ Nilijificha kwa aibu. Lakini vitiligo imenibadilisha kuwa bora. Maisha yana changamoto, lakini ni bora kuzikubali kuliko kuzikimbia.

“Nilipojikubali, maisha yalibadilika. Nilianza kujiamini na watu wakaanza kunikubali. Ingawa bado watu huangalia kwa mshangao au dharau, nimejikubali na nina mtazamo chanya. Kama alivyosema Ralph Waldo Emerson, ‘Kuwa wewe mwenyewe katika dunia inayokutaka uwe mtu mwingine ni mafanikio makubwa,’ amewahi kusema Yvesmark katika moja ya mahojiano yake

Mbali na hao kuna wanamitindo wengine wenye vitiligo  wanaofanya vizuri katika sanaa hiyo kama vile Bailey Ramirez, Deborah Giselle Elisabeth, Terence Munzemba, Kirtus Thibodeaux na wengine wengi.

Clementina Chalamila

Huyu ni binti wa Kitanzania, mwanzilishi wa taasisi isiyo ya kiserikali Beyond Skin inayojihusisha na kueneza uelewa juu ya ngozi kama vile Vitiligo.

Akizungumza na Mwananchi Clementina amesema taasisi hiyo inatoa uelewa kupitia mitandao ya kijamii, mikutano, na kupitia fasheni

“Taasisi hii imetokana na stori yangu, kutokana na jinsi ambavyo nilikuwa napitia dhihaka katika kukua kwangu hadi sasa ninavyojielewa. Nimekuwa naona kuna ‘gap’  kupata msaada wa kisaikolojia kwasababu mtu  mwenye ngozi kama yangu mara nyingi kisaikolojia anakuwa hayupo sawa.  Pia jamii inakuwa haimuelewi.

“Nikawa nimekaa najiuliza kama Tanzania kuna taasisi yoyote tunaweza kwenda kupata msaada. Lakini hapa nyumbani hakuna ukitembea watu wanakuuliza, nikasema nitatoka niongee kwa niaba ya watu wengine,”amesema Clementina 

Tangu afungue taasisi hiyo mwaka 2025 amesema muitikio ni mkubwa.

“Watu wanakuja hata waliokuwa hawajikubali wanaanza kujikubali. Tunafundisha watu wanaelewa, shida kubwa hapa Tanzania watu  wenye Vitiligo wanatafuta dawa na duniani bado watafiti wanatafuta.amesema.

Akizungumzia upande wa fasheni Clementina amesema jinsi muonekano wao ulivyo ni sanaa.

“Tulivyokaa ni saa ya Mungu, tumejichora kama maua fulani kuna namna unakuwa unavutia. Ukitembea sehemu watu wote wanakuwa wanakuangalia. Tunatumia fasheni kutoa uelewa hata kesho mtu mwenye vitiligo akimuona mwenzie amevaa nguo fulani  ataona nii kitu cha kawaida. 

“Pia fasheni tumejikita na uelewa wa chapa.  Tunafanya kazi na modeling agencies ukija pale wanahamasisha  kujiamini, mtu ajikubai muonekano wake. Tutegemee kuwa na vitiligo models ambao watakuwa wanafanya fashion show Tanzania,”amesema Clementina 

Hata hivyo ametoa ushauri kwa watu wenye vitiligo kujitokeza na akuacha kujificha.

“Haupo pekeyako, kuna utolewaji wa elimu kwa akili mnemba watu wanatengeneza picha kama wana vitiligo kuonesha tu kwamba hiki kitu ni kizuri hauwezi ukajificha.

“Tunatafuta sasa hivi watu wenye vitiligo, tuungane wasijione kama wapo pekeyao. Lakini pia wazazi ni ngumu kumlea pekeyako mtoto mwenye vitiligo unahitaji sapoti sisi tupo kwa ajili ya hili suala,”amesema

Clementina ambaye ni muhitimu wa Diploma ya Sheria Tumaini University. Na pia  mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Sahahada ya Sheria katika chuo hiko ameeleza changamoto ambazo anazokutana nazo

“Kwanza mimi ni mwanafunzi natamani kusaidia jamii lakini natamani wadau ambao wanaweza wakaunga  mkono taasisi yetu. Kwa sababu ni suala la kijamii na linahitaji pesa,  nguvu kubwa ya jamii. pia serikali kuna haja ya kuweka nguvu,” amesema Clementina ambaye pia ana Vitiligo.

Alichosema daktari

Akizungumzia ugonjwa huo daktari wa ngozi Peter Chapa, kutoka  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma amesema vitiligo ni ugonjwa wa ngozi ambao mtu anapata baada ya kuzaliwa. Anapoteza rangi inaweza kuwa kwenye ngozi ,  nywele au sehemu zenye utelezi kama za siri, mdomo 

“Vitiligo visababishi vyake bado havijajulikana vizuri. Lakini kuna dhana mbalimbali  tumekuwa tukizungumza kwamba inawezekana  zinasababisha kutokea kwa ugonjwa huu. Miongoni mwa ambazo zinaendelea kufanyiwa utafiti ni pamoja na  ugonjwa wa kurithi kwa  sababu imeonekana asilimia 50 ya watu  ambao wana ugonjwa huu kwenye familia yao kuna mtu aliwahi kupata.

“Nyingine ambayo tumekuwa tukiitumia hasa kwenye matibabu  ni miongoni mwa magonjwa ambayo kinga ya mwili inashambulia chembe fulani za mwili. Inadhaniwa ya kwamba kinga ya mwili ya mtu inashambulia chembe ambazo zinatengeneza rangi kwanini inatokea baadhi ya maeneo bado haijajulikana,”amesema Chapa

Ameogeea kuwa ipo dhana inayohusisha chembe za fahamu, chembe za kutengeneza rangi zinajiharibu zenyewe lakini sababu halisi bado tafiti zinaendelea

Akitaja dalili za ugonjwa huo amesema ni kupungua kwa rangi au kupotea katika eneo fulani  la ngozi . Inaweza kutokea kama kiduara au shepu yoyote kisha baadaye ikawa inaongezeka. 

Akizungumzia mambo ya kuepukakwa magonjwa wa vitiligo amesema inategemeana an ukubwa.

“Mtu akipata inategemea na ukubwa wa tatizo, mara nyingi wanakuwa wanapata changamoto ya kuungua na jua . Maana yake epuka jua la mchana hasa kwa kupaka mafuta ya kukinga mionzi ya jua,”amesema mtaalamu huyu

Je ugonjwa unatibika?

“Uwezekano wa kupona naweza kusema upo kwa maana kwamba vitiligo ina matibabu tofauti, ikitegemea ukubwa wa tatizo. Kuna matibabu yanahusisha spidi ya kupoteza rangi mara nying huwa  tunaanza na hatua ya kwanza ya kuzuia kuendelea kwa tatizo la spidi. Tutampa dawa za kuzuia kinga ya mwili isiendelee kushambulia chembe zinazotengeneza rangi.

“Kisha tutaanza matibabu ya kuziwezesha chembe kutengeneza rangi na ni zile zinazobaki kwenye vinyweleo. Kuna dawa za kupaka lakini kwenye eneo kubwa kuna dawa kama mionzi ya jua bandia inatumika. Mtu anapewa kwa vipindi kadhaa baadaye rangi inaweza kurudi,”amesema Chapa.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *