Akitoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa shambulio hili limesababisha vifo vya takriban watu 64.
“Waliofariki ni pamoja na watoto 13, wauguzi wawili wanawake, daktari mmoja mwanaume na wagonjwa kadhaa. Aidha, watu wengine 89 walijeruhiwa, wakiwemo wahudumu wanane wa afya.” Amesema Dkt. Tedros
Shambulio hilo pia limeharibu vibaya idara za watoto, wazazi na dharura za hospitali hiyo, na kuifanya kushindwa kutoa huduma muhimu za matibabu kwa sasa.
Dkt. Tedros amesema kuwa tukio hilo linaongeza idadi ya vifo vinavyohusishwa na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya tangu kuanza kwa vita nchini Sudan kufikia zaidi ya 2,000. Katika kipindi cha takriban miaka mitatu ya mzozo huo, WHO imethibitisha vifo vya watu 2,036 katika mashambulizi 213 dhidi ya huduma za afya.
Kwa ujumla, zaidi ya watu 720 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo hadi sasa.
Mwanamke wa Sudan aliyehamishwa ndani ya nchi Mona Ahmed anapata ushauri na dawa katika kliniki ya UNFPA.
Mkuu huyo wa WHO ameonya kuwa “mashambulizi dhidi ya huduma za afya yana athari kubwa za haraka na za muda mrefu kwa jamii ambazo tayari zinahitaji kwa dharura huduma za matibabu.”
WHO inaendelea kushirikiana na washirika wa ndani kuimarisha huduma katika vituo vingine vya afya, ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa matibabu ya majeruhi, huduma za watoto na uzazi, pamoja na kusambaza dawa muhimu na vifaa vya dharura.
Dkt. Tedros ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, akisisitiza umuhimu wa kulinda raia, wahudumu wa afya na wahudumu wa misaada ya kibinadamu. “Huduma za afya hazipaswi kuwa shabaha ya mashambulizi. Amani ndiyo tiba bora,” amesema.