
Baada ya Iran kufunga Lango Bahari la Hormuz na kupanda bei ya nishati kwa kiwango kikubwa, Wizara ya Fedha ya Marekani imelazimika kutangaza kuwa imeondoa vikwazo vya kununua mafuta ya Iran kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Jamhuri ya Kiislamu kufunga Lango Bahari la Hormuz na kupanda juu bei ya nishati duniani kote.
Wizara ya Fedha ya Marekani imelazimika kutangaza kuwa imeruhusu kununua mafuta ghafi na bidhaa zinazotokana na mafuta ya petroli zilizoko kwenye meli tangu tarehe 20 Machi. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, ruhusa hiyo itaendelea kutumika hadi tarehe 19 Aprili.
Itakumbukwa kuwa, Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent Alkhamisi iliyopita alikiri kuwa kuondolewa marufuku hiyo kutaruhusu karibu mapipa milioni 140 ya mafuta ya petroli kuingizwa katika soko la kimataifa la bidhaa hiyo na kupunguza mashinikizo makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwenye soko hilo.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Uhusiano wa Umma na msemaji wa Wizara ya Mafuta ya Iran, Saman Qoddusi, amekadhibisha madai ya Marekani kwamba kuna mafuta ya Iran ambayo hayajauzwa yaliyokwama katika meli baharini akisema kwa sasa Tehran haina mafuta ya ziada yaliyokwama baharini kwa ajili ya kuuzwa kwenye masoko ya kimataifa.
Amesisitiza kuwa matamshi ya Waziri wa Fedha wa Marekani yana lengo la kurejesha matumaini kwa wanunuzi wa mafuta na kudhibiti mkanganyiko wa kisaikilojia wa masoko ya bidhaa hiyo.