Duru ya pili ya hujuma za kijeshi za Marekani na utawala wa Kizayuni imekuwa nukta muhimu katika historia ya mikataba na makubaliano ya kijeshi katika ulimwengu wa Magharibi.

Wataalamu wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa vita dhidi ya Iran vinaweza kuathiri sio tu milinganyo ya usalama katika eneo la Asia Magharibi, bali pia mustakabali wa mfumo wa usalama wa nchi za Magharibi. Tangu siku za kwanza za vita vya pili vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Washington imejaribu kupanua wigo wa mzozo huu kutoka vita vya kieneo na kuufanya uonekane kuwa ni tishio kwa usalama wa pamoja wa ulimwengu wa Magharibi. Katika muktadha huo huo, Marekani imetoa wito kwa washirika wake wa Ulaya katika muungano wa kijeshi wa NATO kushiriki katika vita dhidi ya Iran katika Lango-Bahari la Hormuz. Hoja kuu ya Marekani ni kwamba ukosefu wowote wa usalama katika Lango Bahari hilo unaweza kuathiri moja kwa moja uchumi wa dunia na usalama wa nishati wa nchi za Ulaya.

Serikali kama vile za Ujerumani, Ufaransa na Uhispania zimekuwa na shaka tangu mwanzo kuhusu nafasi ya NATO katika mzozo huu, zikisisitiza kwamba hilo haliko katika majukumu ya pamoja ya ulinzi ya Mkataba wa Atlantiki. Hoja ya Ulaya pia ni muhimu katika mtazamo wa kisheria. Kifungu cha 5 cha Mkataba wa Washington kinapaswa kutatekelezwa pale tu mmoja wa wanachama wa mkataba huo anaposhambuliwa kwa silaha kwenye ardhi yake. Hii ni katika hali ambayo vita hivi vya muungano wa Marekani na Israel dhidi ya Iran havikufanyika katika ardhi ya nchi mwanachama wa NATO, wala si matokeo ya shambulio la moja kwa moja dhidi ya mmoja wa wanachama wa muungano huu, bali kinyume chake, mwanachama wa NATO ndiye amekuwa mchokozi katika vita hivi. Kwa kuzingatia ukweli huu, serikali nyingi za Ulaya zinaamini kwamba kuingia rasmi NATO katika vita hivi hakuna msingi wowote wa kisheria.

Udhibiti kamili wa Iran katika Lango Bahari la Hormuz

Wakati huo huo, Lango-Bahari la Hormuz la Iran limekuwa kitovu kikuu cha mgogoro huu. Njia hii ya kimkakati, ambayo sehemu kubwa ya biashara ya nishati duniani inapitia, imekuwa mojawapo ya maeneo nyeti zaidi ya kijiopolitiki wakati wa vita. Washington imejaribu kuonyesha uwezekano wa kutokuwepo usalama katika lango la Hormuz kama tishio la moja kwa moja kwa uchumi na usalama wa Ulaya. Lakini nchi nyingi za Ulaya hazioni hoja hii kuwa sababu ya kutosha ya kuifanya NATO ishiriki katika vita vikubwa zaidi. Matukio haya yote yanakuja wakati ambapo, kwa upande mmoja, watawala wa Marekani hawakudhani kwamba vita hivi vingegeuka kuwa vya kieneo, na kwa upande mwingine, Trump kimsingi hakuamini kwamba Iran inaweza kudumisha udhibiti wake kwenye Lango-Bahari la Hormuz. Matokeo yake ni kuwa sasa amelazimika kunyanyua juu mikono yake na kuomba msaada kutoka kwa washirika wake wa Ulaya katika muungano wa Nato. Pamoja na hayo ukweli ni kwamba, kwa mtazamo wa miji mikuu mingi ya Ulaya, kugeuzwa suala la usalama wa baharini kuwa mzozo kamili wa kijeshi si tu kwamba kunaweza kuzidisha mgogoro wenyewe bali pia kunaweza kuyumbisha eneo zima la Asia Magharibi.

Sababu nyingine muhimu ambayo inaifanya Ulaya kuchukua msimamo wa tahadhari zaidi kuhusiana na ombi la kushiriki katika vita dhidi ya Iran ni uzoefu wa kihistoria wa vita vya Iraq vya mwaka 2003. Wakati huo pia, Washington ilijaribu kuwahamasisha washirika wake washiriki katika vita vikubwa vya Asia Magharibi, lakini tofauti kubwa zilizoibuka kati ya wanachama wa NATO kuhusu suala hilo kulisababisha mpasuko mkubwa katika mahusiano ya Transatlantic. Wasomi wengi wa kisiasa wa Ulaya leo wana wasiwasi kwamba kujikariri kwa suala hilo kuhusu Iran kunaweza kuleta changamoto kubwa kwa itibari ya nchi za Magharibi. Brussels pia ina wasiwasi kwamba uzingatiaji mkubwa wa kijeshi wa Marekani kwenye Ghuba ya Uajemi unaweza kupelekea kupungua kwa mtazamo wa kimkakati wa Washington kwa bara Ulaya. Hili ni muhimu hasa inapotiliwa maanani kwamba vita kati ya Ukraine na Russia vinasalia kuwa moja ya changamoto kubwa zaidi za kiusalama barani Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *