Safari ya Wamisri, Al Ahly na Pyramids katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, 2025-2026 imehitimishwa na Waarabu wenzao, tena kwa aibu kutokana na kuchapika viwanja vya nyumbani.

Miamba hiyo imepoteza mechi zake za marudiano zilizochezwa jana Jumamosi Machi 21, 2026 na kutupwa nje ya michuano katika hatua ya robo fainali.

Pyramids imevuliwa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiondoshwa na AS FAR Rabat ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya mechi ya kwanza kule Morocco kumalizika kwa sare ya 1-1, kisha pale Misri ikashinda 2-1.

Al Ahly ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikishinda kombe hilo mara 12, ikiwa ndiyo timu iliyochukua mara nyingi zaidi. Nayo imepigwa nje ndani jumla ya mabao 4-2 na Esperance ya Tunisia. Mechi ya kwanza nchini Tunisia, wenyeji walishinda 1-0, kisha marudiano pale Misri, wageni wakashinda tena 3-2.

UNBEATEN IMEVUNJWA

Kuzifunga Al Ahly na Pyramids katika viwanja vyao vya nyumbani si kitu ambacho kila timu inaweza kwani miamba hiyo imeweka ngome ngumu hapo wapinzani wakifika wanapata wakati mgumu.

Timu hizo hadi zinakuja kupoteza mechi za Ligi ya Mabinhmgwa Afrika, zilikuwa zimecheza zaidi ya mechi kumi mfululizo bila vipigo. Al Ahly mechi 12 ikishinda sita na sare sita, wakati Pyramids ikiwa na mechi 15, imeshinda kumi na sare tano.

Zimepita siku 427, sawa na mwaka mmoja na miezi miwili na siku tatu tangu mara ya mwisho Al Ahly inapoteza nyumbani kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo pale Misri, ndipo ikaja kupoteza tena Jumamosi iliyopita.

Mara ya mwisho Januari 18, 2025, Al Ahly ilifungwa mabao 2-1 nyumbani na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao ya Relebohile Mofokeng dakika ya 53 na Tshegofatso Mabaso dakika ya 83, yaliacha kilio Cairo. Al Ahly bao lake alifunga Hussein El Shahat dakika ya 63.

Baada ya hapo, Al Ahly licha ya kupoteza mechi hiyo, lakini ikafuzu robo fainali ikaenda kuichapa Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0, ikishinda nyumbani na ugenini kwa matokeo ya 1-0.

Nusu fainali ikakutana tena na Wasauzi ambapo safari hii walikuwa Mamelodi Sundowns. Matokeo ya jumla yaliitupa nje Al Ahly lakini haikupoteza baada ya mechi ya kwanza ugenini kutoka 0-0, marudiano nyumbani ikawa 1-1, bao la ugenini likawang’oa.

Msimu huu 2025-2026, ilianzia raundi ya pili, ikaitoa Aigle Noir ya Burundi kwa jumla ya mabao 2-0, ikishinda 1-0 ugenini na nyumbani. Ikafuzu makundi ambapo ilipangwa Kundi B na Yanga, JS Kabylie na AS FAR Rabat.

Hatua ya makundi ikamaliza kinara kwa kukusanya pointi kumi baada ya kushinda mechi mbili na sare nne. Ilizifunga JS Kabylie (4-1) na Yanga (2-0), zote nyumbani, huku mechi nyingine ya nyumbani dhidi ya AS FAR Rabat ikiisha 0-0.

Sare zingine tatu za ugenini ni dhidi ya AS FAR Rabat (1-1), Yanga (1-1) na JS Kabylie (0-0).

Robo fainali ndipo ikakutana na kisanga, kufungwa ugenini na nyumbani, ni matokeo mabaya zaidi kwa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Walioifanya kazi hiyo ni Espérance ya Tunisia iliyoanza na ushindi wa bao 1–0 nyumbani, kisha ikashinda tena 3-2 pale Cairo.

Kocha wa Al Ahly, Yves Torup, amezungumzia kipigo hicho kilichofanya kutupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akisema: “Hongereni Esperance kwa kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na ninachukua jukumu kamili kwa matokeo ya mechi. Ninaamini tulicheza vizuri katika vipindi vyote viwili na tulitangulia kufunga bao.”

Ameongeza: “Nilikuwa na matumaini ya kuingia kipindi cha pili kwa ari kubwa zaidi, lakini kosa la kizembe lilitugharimu, na dakika chache baadaye kosa lingine lilisababisha penalti. Ninaomba radhi kwa Al Ahly na mashabiki wake kwa kutofikia matokeo yaliyotarajiwa.”

Torup pia anasema: “Lazima tujichunguze na tuone makosa ili tuyarekebishe, na hili ni kosa langu na ninawajibika. Sina udhibiti wa mustakabali wangu; nafanya kazi yangu na kuna uongozi. Ikiwa wataamua niendelee, nitaheshimu hilo, na ninaelewa ugumu wa kipindi hiki.”

Anaongeza: “Mpinzani alitumia vizuri kila nafasi waliyoipata, na tulipoteza mechi ndani ya dakika tatu tu. Tulikuwa na nafasi ya kuongeza mabao kabla ya Esperance kufunga, lakini mabao tuliyoruhusu kwa muda mfupi ndiyo yaliyosababisha kilichotokea.”

Al Ahly iliingia katika mechi hiyo ikiwa na deni la bao 1-0, ilipofungwa nchini Tunisia wiki moja nyuma. Dakika ya kumi tu, nahodha Mahmoud Ahmed Ibrahim Hassan maarufu Trezeguet akaweka mzani sawa kwa kuisawazishia Al Ahly, hadi mapumziko wenyeji walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili dakika ya 68, Florian Danho akaifungia Esperance, kisha dakika ya 78, Mohamed Amine Tougai akaiweka mbele Esperance kwa bao la penalti.

Al Ahly ikarudi kwa kupata bao dakika ya 84, baada ya beki wa Esperance, Hamza Jelassi kujifunga katika harakati za kuokoa kona.

Wakati Al Ahly ikiwa imepoteza matumaini ya kusonga mbele kwa hadi muda huo ilikuwa inahitajika kufunga mabao mawili zaidi ili ifuzu nusu fainali, ikajikuta inashindwa kulinda heshima ilipofungwa bao la dakika ya 90+4 na Jelassi ambaye alienda kusawazisha makosa baada ya kujifunga.

AS FAR RABAT MBABE WA PYRAMIDS

Mara ya mwisho Pyramids kupoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilifungwa 2-0 na AS FAR Rabat, ilikuwa Aprili 8, 2025 hatua ya robo fainali ikiwa ni mechi ya marudiano baada ya ile ya kwanza Wamorocco hao kupasuka 4-1 pale Misri.

Licha ya Pyramids kufungwa 2-0 mechi ya marudiano, lakini ilifuzu nusu fainali kwa jumla ya mabao 4-3, ikaenda hadi fainali na kubeba ubingwa wake wa kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo 2024-2025.

Baada ya kupita 347, sawa na miezi 11 na siku 13, walewale AS FAR Rabat wanakuja kuifunga tena Pyramids hatua ileile ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tena pia ni mechi ya marudiano lakini afari hii ni ugenini kwa ushindi wa 2-1.

Kabla ya kipigo hicho, Pyramids ilicheza mechi 15 za michuano hiyo bila ya kupoteza ikishinda kumi na sare tano.

Katika mechi hizo kumi ilizoshinda Pyramids ni dhidi ya Orlando Pirates (3-2), Mamelodi Sundowns (2-1), APR (2-0), APR (3-0), Ethiopian Insurance (2-0), Rivers United (3-0), Power Dynamos (1-0), RS Berkane (3-0), Rivers United (4-1) na Power Dynamos (3-1).

Sare ni dhidi ya Orlando Pirates (0–0), Mamelodi Sundowns (1–1), Ethiopian Insurance (1–1), RS Berkane (0–0) na AS FAR Rabat (1–1).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *