Moja ya wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa mara kwa mara kwenye usajili wa klabu kubwa za hapa nchini basi ni kiungo Kelvin Nashon.

Kiungo huyo amekuwa akitajwa mara kwa mara kwenye usajili lakini akihusishwa na klabu kubwa za Simba na Yanga kwa miaka kadhaa sasa.

Mara nyingi imekuwa rahisi kusikia kuwa mwisho mwa msimu anajiunga na timu mojawapo, utasikia Simba na wakati mwingine Yanga.

Siyo kwamba Nashon anatajwa kwenye timu hizo kwa kuwa wachambuzi au waandishi wanapenda kumpa sifa hiyo hapana, bali anatajwa kwa kuwa amekuwa na kiwango bora kwenye timu zote ambazo amefanikiwa kuzichezea.

Nashon mmoja kati ya viungo mahiri wakabaji hapa nchini amekuwa akiitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars mara kwa mara pamoja na kwamba nafasi ya kucheza kwake imekuwa finyu, lakini ubora wake umekuwa ikijidhiirisha rasmi.

Kwa sasa taarifa ambazo zipo zinasema kuwa Nashon ameshajiunga na Simba akitokea Pamba ya Mwanza aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo akitokea Singida BS.

Kiungo huyo aliwashangaza wengi baada ya kuomba kuondoka kwenye kikosi cha Singida mwishoni mwa msimu uliopita ikielezwa kuwa anataka nafasi ya kuonyesha ubora wake zaidi kwenye kikosi cha Pamba.

Hata hivyo ndiye mchezaji ambaye alikuwa anapata nafasi karibia kwenye kila mchezo wa timu hiyo lakini aliamini kuwa Pamba anaweza kufanya mambo makubwa zaidi.

Kiungo huyo alikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kwa msimu huu wote na alikosekana kwenye mchezo wa timu hiyo dhidi ya Simba pekee kwa kile kilichoelezwa kuwa alishasaini mkataba wa kuitumikia Simba kwa msimu ujao ndiyo maana klabu yake ikaamua kumweka nje.

Kiungo huyo ambaye alipata umaarufu akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys mwaka 2017, amekuwa akifananishwa na wachezaji wengi wakubwa kwenye aina yake ya kucheza.

Akiwa ameshacheza karibu michezo yote akiwa na Pamba Nashon amefanikiwa kufunga mabao mawili akitokea kwenye nafasi ya kiungo mkabaji ambayo ni adimu sana kwa wachezaji wengi kufunga mabao.

Kuongeza ushindani

Nashon anatarajiwa kutoa ushindani mkubwa kwa viungo wengine wa Simba, akiwemo rafiki yake mkubwa Yusuf Kagoma ambaye amekuwa akipata nafasi ya kutumikia kwenye klabu hiyo katika michezoi mingine msimu huu.

Aidha inaelezwa kuwa Simba wanataka kukamilisha haraka dili la kiungo huyo kwa kuwa Allasane Kante anaweza kuondoka kwenye kikosi hicho mwishoni mwa msimu hiyo wanatafuta mbadala wake.

“Tutakamilisha usajili wake kwa kuwa ni mchezaji ambaye anataka kuitumikia Simba kwa muda mrefu, tuna mpango wa kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni na kuwa na wazawa wengi kwenye timu yetu hivyo huu ni usajili sahihi kabisa kwenye timu yetu kuelekea mabadiliko makubwa ya msimu ujao.

“Nashon ni mchezaji mzuri sana na tumewahi kujaribu mara kwa mara kumsajili lakini ikashindikana, pale Singida kila siku walikuwa wanaleta wageni lakini hakuna aliyekuwa anamweka nje,” alisema kiongozi mmoja kutoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo.

Kiungo huyo anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wazawa wenye mafanikio makubwa akiwa anamiliki mjengo wa kisasa Mbweni jijini Dar es Salaam, Saloon ya kunyoa nywele, pamoja na sehemu maalumu ya kuonyesha magari zote zikiwa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, haitashangaza kama Nashon hatajiunga na Simba mwishoni mwa msimu huu kwa kuwa miaka mingi imekuwa ikielezwa kuwa ameshamalizana na timu hiyo tangu akiwa kwenye kikosi cha Geita Gold ambapo ilielezwa kuwa ameshatua Dar es Salaam na kupewa mkataba wa kuitumikia timu hiyo. Inaaminika kama akipata nafasi Simba atakuwa na nafasi kubwa ya kutumika timu ya Taifa, Taifa Stars.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *