Dar es Salaam. Kila siku tunasikia biti nzuri na za kuvutia katika nyimbo za wasanii, lakini nyuma ya pazia kuna mchakato uliobeba matukio mengi hadi kukamilika kwa utayarishaji wake.

Mathalani, kuna hata wanamuziki ambao wamewahi kuwatengenezea wenzao biti za nyimbo zao na pia kuna mambo mengi kati ya watayarishaji na wasanii wakati wa kuandaa kazi hizo. Fahamu zaidi.

1. Biti ya wimbo wa Joh Makini, Stimu Zimelipiwa (2009), ilitengenezwa na Nahreel kipindi hicho yupo masomoni India katika chuo cha Punjab ambapo alikokuwa akisomea Computer Science.

2. Biti ya wimbo wake Izzo Bizness, Utarudishwa (2012) akimshirkisha Belle 9, imetengenezwa na rapa kutokea Tamaduni Muzik, One The Incredible ambaye alitoka chini ya M Lab (Music Laboratory).

3. Biti ya wimbo wa Mwana FA, Binamu (2008) toleo la pili, ndio ilimtambulisha Marco Chali katika game na hata kupata nafasi ya kufanya kazi MJ Records akitokea Kama Kawa Records.

Mwana FA, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa sasa,tayari alikuwa asharekodi wimbo huo miaka mingi nyuma na ulikuwepo katika albamu yake ya pili, Toleo Lijalo (2003).

4. Biti ya wimbo wake Bushoke, Mume Bwege (2004), ilitengenezwa na Soggy Doggy na Bizman ndani ya Bongo Records, ila upande wa mixing na mastering akafanya P-Funk Majani, zamani DJ Skills of Pain.

5. Biti ya wimbo wa Nini, Niwe Dawa (2018) akimshirikisha Nay wa Mitego, imetengenezwa na rapa huyo tena ndani ya studio yake ya Free Nation, chapa inayosimama kama rekodi lebo yake pia.

Hata hivyo, awali Nay alipanga kushirikiana na Vanessa Mdee katika wimbo huo ila akaja kubadili mawazo na kumpa nafasi Nini ambaye alikuwa ametoka kuachana na MJ Records.

6. Biti ya wimbo wa D Knob, Sauti ya Gharama (2004) ilikuwa kwa ajili ya kutumika kwenye wimbo wa Mhe. Temba, Nampenda Yeye (2004), ila P-Funk Majani aliposikiliza kwa makini akaamua nyimbo hizo zibandilishane biti, na zilipotoa zote zikafanya vizuri.

7. Biti ya wimbo wa Joh Makini, Don’t Bother (2015) akimshirikisha AKA kutokea Afrika Kusini, ilitengenezwa na Nahreel kwa muda wa dakika 10 tu ndani ya studio yake ya The Industry.

8. Biti ya wimbo wa Dudu Baya, Mwanangu Huna Nidhamu (2000) ilitengenezwa na Master J ndani ya MJ Records ila msanii huyo alienda kuirekodia studio za Sound Crafters kwa Enrico Figueiro.

9. Biti ya wimbo wa kundi la Weusi, Swagire (2018), ni miongoni mwa biti ambazo mtayarishaji kutokea studio za Pluto Republic, S2kizzy alipanga kuzifuta kabisa ila Weusi walipokuja kuirekodi ngoma ikatoka kali na kuvuma.

10. Biti zote za nyimbo zinazopatika katika albamu ya  kundi la Hard Blasters Crew (HBC), Funga Kazi (2000), Professor Ludigo alizitayarisha akiwa Marekani, na alipokuja nazo Bongo ndipo wasanii hao wakazirekodia MJ Records.

Ikumbukwe kundi la HBC liliundwa na wasanii kama Fanani, Big Willy, Frank Korassa, Ngida, Taff Jam na Profesa Jay ambaye alijiunga nalo mwaka 1995, wakati huo akiwa kidato cha tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *