
Casablanca, Morocco. Katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliozikutanisha timu mbili za Morocco, Wydad Athletic Club na Olympique Club de Safi, ilishuhudiwa maajabu katika mchezo huo baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 na Wydad kutupwa nje ya mashindano hayo.
Wydad ambayo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufika mbali imetolewa katika michuano hiyo baada ya kulazimishwa matokeo hayo ya sare katika Uwanja wao wa nyumbani dhidi ya timu hiyo inayobuluza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Morocco ‘Botola Pro’.
Katika mechi ya kwanza ambayo Wydad ilikuwa ugenini iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, ilitangulia mbele kwa bao moja ambalo lilisawazishwa baada ya kipa wake, El Mehdi Benabid kufanya makosa na kujifunga mwishoni mwa mchezo.
Hata hivyo, katika mechi ya jana Olympique de Safi ilionekana kuja kivingine kabisa na kuwavuruga vigogo hao wa Casablanca hasa baada ya golikipa, Benabid kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 24 iliyowagharimu wenyeji kwa kucheza pungufu.
Zilipita dakika 16 tu Olypique de Safi wakaandika bao la kuongoza kupitia mkwaju wa penalti uliowekwa kambani na kiungo, Sofian El Moudane. Lakini kabla ya mapumziko Mohamed Moufid alisawazisha na kuipeleka mapumziko Wydad ikiwa na matumaini ya kufanya makubwa kipindi cha pili.
Dakika 45 za kipindi cha pili zilikuwa ngumu kwa wenyeji Wydad walioonekana kutafuta zaidi bao la kuongoza ambalo pengine lingebadilisha mchezo. Lakini safu ya ulinzi ya wapinzani wao ilionekana kuimarika kwa kuzuia mashambulizi ya wenyeji hao huku wenyewe wakishambulia kwa kushtukiza.
Mchezo huo uliendelea hivyo hadi ilipofika dakika za majeruhi ambapo Olympique de Safi walipata bao la pili kupitia kwa mshambuliaji, Moussa Kone ambaye alipeleka shangwe kwa mashabiki wao wachache waliokuwa wamejitokeza kwenye Uwanja wa Mohamed V wakati mashabiki wa Wydad wakiwa wamebaki wanashangaa na wengine wakishika vichwa baada ya kutandikwa bao hilo.
Kone ambaye ni raia wa Senegal, alifunga bao hilo baada ya kupenyezewa pasi na Salaheddine Errahouli, ambaye alitumia vizuri makosa yaliyofanywa na nyota, Hakim Ziyech baada ya kupoteza umiliki wa mpira huo.
Baadaye katika dakika hizo za nyongeza, Wydad walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Ziyech lakini halikutosha kuwavusha kwenda nusu fainali kutokana na Olympique de Safi kunufaika na sheria ya bao la ugenini.
Wydad imetupwa nje ya mashindano hayo kwa sheria ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 kufuatia matokeo ya sare katika mechi zote mbili ikitoka 1-1 ugenini na kulazimishwa sare nyingine ya 2-2 katika Uwanja wake wa nyumbani.
Olympique de Safi sasa itakutana na USM Alger ya Algeria katika hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo. USM Alger ilifanikiwa kufuzu baada ya kuitoa AS Maniema ya DR Congo.
Katika nusu fainali nyingine CR Belouizdad ya Morocco itavaana na Zamalek ya Misri. CR Belouizdad imefuzu baada ya kuitupa nje Al Masry wakati Zamalek ikiiondoa AS Otoho ya Congo Brazaville.