
Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limewasilisha rasmi rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wa kuipokonya nchi hiyo ubingwa wa Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CAS, rufaa hiyo imesajiliwa rasmi jana Jumatano Machi 25, 2026, ikiwa ni hatua ya kwanza ya Senegal kupinga hukumu iliyotolewa Machi 17 na bodi ya rufaa ya CAF.
CAF ilibaini kuwa mwenendo wa timu ya Senegal ulikiuka vifungu vya 82 na 84 vya kanuni za AFCON, hatua iliyosababisha kutangazwa kwa Senegal kupoteza mechi hiyo kwa njia ya mezani kwa mabao 3-0 dhidi ya Morocco.
Kifungu cha 82 kinasema, ikiwa timu kwa sababu yoyote ile inakataa kucheza au inaacha uwanja kabla ya mwisho wa mechi bila idhini ya mwamuzi, itachukuliwa kuwa imeshindwa na itatupwa kwenye mashindano yote.
Kifungu cha 84, kinakamilisha kifungu cha 82 kwa kusema, timu inayokiuka kifungu cha 82 itatupwa kabisa kwenye mashindano na itapoteza mechi kwa mabao 3–0.
Kupitia rufaa hiyo, Senegal inataka uamuzi huo ubatilishwe na kutambuliwa tena kama mabingwa halali wa Afrika kwa mwaka 2025. Aidha, imeiomba CAS kusimamisha muda wa kuwasilisha hoja kamili za rufaa hadi watakapopatiwa maelezo ya kina ya hukumu ya CAF.
CAS imeeleza kuwa jopo la waamuzi litaundwa kusikiliza kesi hiyo, na baada ya hapo ratiba rasmi ya mwenendo wa shauri itawekwa. Kwa mujibu wa taratibu za mahakama hiyo, upande wa mlalamikaji una siku 20 kuwasilisha hoja za kisheria, huku upande wa utetezi ukipewa siku nyingine 20 kujibu.
Hata hivyo, CAS imesisitiza kuwa bado ni mapema kuainisha muda kamili wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, hasa kutokana na ombi la Senegal la kusimamisha baadhi ya muda wa kisheria.
Mahakama hiyo imehakikisha kuwa mchakato wa usuluhishi utafanyika kwa haraka iwezekanavyo, huku ikizingatia pande zote kupata usikilizwaji wa haki na wa uwazi