Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameripoti kuwa makumi ya maelfu ya watu wanaokimbia Lebanon wameingia Syria wakiwa “wamechoka, wameathirika kisaikolojia na wakiwa na mali chache sana,” huku mashambulizi mapya dhidi ya meli katika Mlango Bahari wa Hormuz yakiongeza hofu ya kucheleweshwa kwa misaada ya kibinadamu.
Jean-Pierre Lacroix, naibu katibu mkuu wa shughuli za amani, aakihutubia kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Lebanon.
Walinda amani wa UN wauawa wakati wa mashambulizi
Akilihutubia Baraza hilo, Jean-Pierre Lacroix Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa ameonya kuwa “hali imezorota kwa kiwango cha hatari kubwa kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya Hezbollah na Israel katika na nje ya msitari tenganishi baina ya Lebanon na Israel ujulikanao kama Blue Line”.
Ameeleza kuwepo kwa mapigano makali ya ardhini na mashambulizi ya angani “yasiyo na kifani,” huku vikosi vya Israel vikisonga mbele hadi kilomita 11 ndani ya Lebanon na kudhibiti maeneo karibu na mpaka huo.
Ghasia hizo pia amesema zimeua walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu chini ya Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mpito nchini Lebanon UNIFIL.
Lacroix amethibitisha kuwa walinda amani watatu waliuawa katika matukio tofauti, wakiwemo wanajeshi wawili wa Indonesia waliouawa baada ya gari lao kulipuliwa karibu na Bani Hayyan, na mwingine aliyeuawa ndani ya kambi ya Umoja wa Mataifa huko Ett Taibe. “Matukio haya ya kusikitisha hayakupaswa kutokea,” amesema.
Muonekano mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Lebanon.
Raia wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu
Akitoa taarifa kwa njia ya video kutoka Beirut, Tom Fletcher Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza hali ya hofu na kukata tamaa iliyotanda.
“Nilipowasili nilikuta wasiwasi, mvutano na huzuni kwa kiwango ambacho sijawahi kushuhudia kwa miaka mingi,” amesema baada ya kukutana na viongozi wa Lebanon.
Ameonya kuwa “mamia ya maelfu ya raia bado wako hatarini,” huku operesheni za kijeshi zikiendelea kusini mwa Lebanon, vitongoji vya kusini mwa Beirut na Bonde la Bekaa, na vijiji vingi vikiharibiwa kabisa.
Onyo la mzunguko wa watu kufurushwa
Fletcher ameonya kuwa ghasia zinazoendelea zinaweza kusababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu, huku watu wengi wakilazimika kukimbia makazi yao pande zote za Blue Line.
“Mzunguko wa ufurushwaji wa watu unaendelea,” amesema, akibainisha kuendelea kwa mashambulizi ya makombora kuelekea kaskazini mwa Israel pamoja na kuongezeka kwa operesheni za kijeshi Lebanon.
Amehimiza Baraza la Usalama kuchukua hatua za pamoja haraka ili kuzuia hali ambayo tayari ni mbayá isiwe mbaya zaidi na kulinda raia.