Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na Msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema wawili hao wamekuwa na mazungumzo ambapo Katibu Mkuu amemshukuru Meya Mamdani kwa uhusiano imara na msaada mkubwa ambao Umoja wa Mataifa umekuwa ukipokea kutoka kwa jiji hilo mwenyeji.

“Ushirikiano huu umekuwa muhimu katika kuwezesha shughuli mbalimbali za kimataifa kufanyika kwa ufanisi,” imesema taarifa hiyo ikimnukuu Guterres.

Majiji na miji ina mchango mkubwa kwenye maendeleo

Aidha, Katibu Mkuu amesisitiza nafasi muhimu ya miji katika dunia ya sasa, akibainisha kuwa miji ni kitovu cha maendeleo, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa.

Ni katika muktadha huo, viongozi hao wamejadili njia mbalimbali za kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Jiji la New York.

Katika majadiliano hayo, Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake ya kuendeleza mazungumzo na ushirikiano wa karibu kati ya vyombo hivyo viwili kwa lengo la kukuza ajenda za maendeleo na kukabiliana na changamoto za kimataifa kwa pamoja.

Tarehe 14 mwezi Desemba mwaka 1946 Umoja wa Mataifa uliamua rasmi makao yake ya kudumu yawe jijini New York. Ingawa ujenzi ulianza mwaka 1947-1948 na wafanyakazi wakaanza kuhamia kwenye jengo la Makao Makuu Agosti 1951, jengo kamilifu la sasa lililoko kwenye eneo liitwalo TurtleBay lilikamilika na kufunguliwa rasmi mwaka 1952.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *