
Mbeya. Mbeya City imetenga kiasi cha Sh10 milioni kwa wachezaji wake ili kuwahamasisha waibuke na ushindi katika mchezo unaofuata wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC, Ijumaa, Aprili 3, 2026 katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Manyara.
Katibu Msaidizi wa Mbeya City, Joseph Mlundi amesema kuwa lengo la kutenga kiasi hicho ni kuongeza morali zaidi kwa kikosi chao.
“Japokuwa ndio kawaida yetu kutoa bonasi kwa wachezaji wanaposhinda au kutoa sare lakini kwa mchezo huu na KMC huenda hali ikabadilika zaidi kwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji ametangaza kwa ujumla”
“Kawaida hatupungui Sh 5 million ila kwa hii itafika hadi Sh 10 milioni, lengo ni kuwapa motisha vijana kupigania nembo ya Jiji la Mbeya, tunaamini kuanzia mechi hiyo City haitakamatika,” amesema Mlundi.
Beki wa timu hiyo, David Mwasa amesema wanafahamu ugumu wa mchezo huo kutokana na hali ya wapinzani wao, lakini kwa matokeo waliyonayo hawana sababu ya kukosa pointi tatu muhimu.
“Tunajua mechi itakuwa ya ushindani kwa kuwa kila mmoja anataka pointi tatu, niwaombe mashabiki kutuombea na kutusapoti na sisi wachezaji tutapambana kubaki salama Ligi Kuu, tuko tayari kwa kila mchezo,” amesema Mwasa.
Mbeya City inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 13 ilizokusanya katika mechi 16, ikipata ushindi katika mechi tatu, kutoka sare nne na kupoteza michezo tisa.